HISIA ZANGU: Kwa Fredy Michael utachukua namba au unachokiona?

FREDY Michael, rafiki yangu Ahmed Ally wakati akijitamba na vifaa ambavyo vilitua Januari alimpachika jina la ‘Fungafunga’. Wakati huo tulikuwa hatujamuona uwanjani. Jina lilitokea mazoezini. Kama sio mazoezini basi alikuwa amelichukua kutokana na mabao aliyofunga Zambia.

Baada ya hapo Fredy ametuchanganya akili. Kila tulipomuona uwanjani alituchanganya akili. Mpaka nyakati hizi nikiwasikiliza Wanasimba wenyewe wanajikuta wamechanganyikiwa kwa Fredy, hasa nyakati hizi ambazo Simba inataka kutoa ‘Thank You’ kwa wachezaji wake.

Fredy aondoke au abaki? Kuna Wanasimba wanasema aondoke kuna ambao wanataka abaki. Tunaishi katika dunia ya namba. Kule alikoondoka amebakia kuwa mfungaji bora na hapa nchini tangu afike amefikisha mabao kumi katika michuano yote. Sio haba. Kuna washambuliaji walioanza msimu na hawajafikisha idadi hii ya mabao.

Mara ya kwanza nilipomuona Fredy sikuona kama mshambuliaji wa maana. Lakini anafunga. Hapo ndipo anaponifunga mdomo. Mara ya pili nilipomuona sikuona kama alikuwa mchezaji tishio lakini alifunga. Kuna mechi anacheza ovyo anatukanwa kuliko mchezaji yeyote uwanjani lakini mechi inayofuata anafunga.

Wakati mwingine nilikuwa namtazama na kuanza kuhoji ubora wa Ligi ya Zambia. Ilikuwaje akawa anacheka na nyavu pale Zambia mpaka ikafikia hatua ya kuwa mfungaji bora wakati Simba ilipokuwa inamchukua. Na hapo hapo unawaza namna ambavyo hata washambuliaji wengine wa Ligi hiyo walishindwa kumfikia wakati alipoondoka. Tumeanza kuwaacha Wazambia kiuwezo?

Kati yake na Pah Omary Jobe unaona wazi kwamba tofauti yao ni mabao. Hauwezi kuwaamini kama washambuliaji lakini kinachomtofautisha Fredy na Jobe ni kwamba Fredy anafunga. Na sasa ametuachia mtihani wa kukata jina lake. Unajaribu kuangalia na kujiuliza, Simba wapo tayari kuusaka ubingwa wa Afrika huku mshambuliaji akiwa Fredy?

Unajaribu kuwaza namna ambavyo hapo kati wamepita washambuliaji walio bora zaidi yake. John Bocco, Chris Mugalu na Meddie Kagere. Kupitia viwango vile Simba wanaamini Fredy yupo katika anga zao au? Lakini pia kupitia kwa kiwango cha mshambuliaji kama Fiston Mayele Simba wanahisi Fredy anapaswa kuaminiwa na kufanya yale ambayo Mayele alifanya kwa watani?

Washambuliaji wakati mwingine wana tabia mbili. Kuna wale ambao wana purukushani za kutosha lakini hawajui kuziona nyavu ipasavyo. Kuna wengine ambao hawana purukushani lakini wana uwezo wa kuziona nyavu. Halafu kuna wenye kila kitu kama Ronaldo de Lima. Na hapa nchini kwa viwango vyetu tulikuwa na Fiston Mayele hapa majuzi.

Halafu juu ya hapa kuna Fredy. Hana purukushani anafunga lakini kadri mechi inavyoendelea hakupi ahadi kama anaweza kufunga. Simba wataangalia namba au wataangalia wanachokiona katika macho? Inakuwa mtihani mkubwa katika soka la kisasa. Hata wazungu huwa wanasumbuliwa na tatizo hili. Tatizo la namba na unachokiona uwanjani.

Inanikumbusha wakati Yannick Bangala alipochaguliwa kuwa mchezaji bora wa msimu katika msimu wake wa kwanza Yanga. Hakuwa na pasi za mabao, hakufunga walau mabao mawili katika msimu mzima lakini ulichokiona kutoka kwake kilikuwa kinavutia hasa na kila mtu alikiri kwamba Bangala alikuwa anastahili. Fredy yupo tofauti. Mpira hauuoni lakini anafunga.

Tatizo la kuachana na Fredy ni kubwa. Kwanza ni gharama kubwa iliyotumika kumsajili katika dirisha la Januari. Unawezaje kuvunja mkataba wake. Hapo hapo unalazimika kuvunja mkataba wa Jobe. Lakini pia unaweza kuingia katika hatari nyingine mbele ya safari.

Lakini kwa kadri ninavyoifahamu Afrika kuna uhaba mkubwa wa washambuliaji. Yanga wanajaribu kutulia kwa Joseph Guede lakini si unaona namna walivyoingia chakani kwa Ustaadhi Hafiz Konkoni? Afrika ina uhaba mkubwa wa wafungaji. Dunia pia ina uhaba huo. Labda ni kitu ambacho kinaweza kuwakabili Simba hata kama wakiamua kuachana na Fredy.

Nini kifanyike? Nadhani Fredy abakie klabuni lakini aletewe mshambuliaji aliye bora zaidi yake. Kufikiria kwamba Simba wanaisaka nusu fainali ya Afrika huku eneo la ushambuliaji likiongozwa na Fredy ni kitu ambacho hakiingii akilini kwa sasa. Labda abadilike hasa. Unahitaji mshambuliaji ambaye anakuahidi kufunga mabao.

Zamani kulikuwa na Mohamed Hussein ‘Mmachinga’. Sifa zake zilikuwa kama John Bocco. Sawa, hakuwa na uwezo mkubwa wa kukokota sana mpira wala kupiga sana chenga. Hata hivyo, wakati anaingia uwanjani ungejua wazi kwamba muda wowote bao linakuja. Ukakamavu wake na namna anavyofungua nafasi vingekupa picha kwamba bao linakuja muda wowote.

Rafiki yangu Jobe? Sijui alifikaje nchini. Nadhani Simba itaingja hasara kubwa kutokana na ukosefu mzuri wa kukagua wachezaji kabla ya kuwapa mikataba. Huwa tunaita scouting. Kwa Fredy unaweza kusamehe kwamba labda kigezo kikubwa kilikuwa ni kuwa mfungaji bora katika Ligi Kuu ya Zambia. Vipi kwa Jobe. Alionwa kabla? Alikuwa na sifa zipi? Katika Ligi ipi?

Rafiki yangu Crescentius Magori nasikia amerudi katika masuala ya usajili. Inabidi tukubali tu kwamba zamani walikuwa wanafanya vizuri na labda Simba kuboronga katika usajili kulitokana na wao kuwa kando. Hapa katikati Simba imeboronga katika masuala ya usajili. Takribani madirisha sita yaliyopita Simba wamekosea. Labda kina Magori watairudisha Simba katika njia.

Tuna tatizo la kukiri upungufu wetu. Hapa katikati watani wao wamepatia kuliko wao. Sio kwamba kina Hersi Said walikuwa hawakosei, hapana. Walikuwa wanapatia zaidi kuliko kukosea. Unaweza kuzungumza mambo mengi ya kwamba kuna wachezaji wanahujumu timu lakini Yanga wamekuwa bora zaidi kama Simba ya Jose Luis Miquissone ilivyokuwa bora.

Related Posts