Wajerumani walivumbua magari – na wakati Carl Benz alipopata hati miliki ya “gari linaloendeshwa na injini ya gesi” mnamo 1886, tayari alijua kuwa kuyauza kungekuwa biashara ya kimataifa.
Mteja wa kwanza wa kampuni yake alikuwa sultani wa Morocco, Hassan I. Na gari lake la kwanza lilifika China miaka michache baadaye, mnamo 1901, kama zawadi ya siku ya kuzaliwa kwa mama wa mfalme alietawala wakati huo.
Hata hivyo, Carl Benz hakuwa na njia ya kujua kwamba miaka 120 baadaye sekta ya magari ya ndani ya China ingekua na kuwa mpinzani mkubwa wa watengenezaji wa magari wa Ujerumani.
Nchi hizo mbili zilishirikiana kwa karibu kwa miongo kadhaa, ambapo Volkswagen iliingia ubia wa kuunda magari mjini Shanghai mwaka 1983 na magari ya Ujerumani kuitawala mitaa ya miji ya China kwa miongo kadhaa iliyofuta.
Soma pia: China yahadharisha juu ya kuporomoka biashara ulimwenguni
Hata leo, chapa za Ujerumani zinapata faida kubwa katika soko la China. Na wengi wanakubaliana na Rais wa zamani wa Ujerumani na Mwenyekiti wa IMF Horst Köhler, ambaye hivi karibuni alivuma nchini China kwa mahojiano ambamo alisema, “sisi sote tungekuwa wajinga – China itakuwa wajinga na Ujerumani itakuwa wajinga – ikiwa hatungekuwa na uhusiano mzuri.”
“Tunahitaji kufanya kazi pamoja na kuhakikisha uchumi wa dunia unakua,” Köhler alimwambia mwanablogu wa video wa China.
Watengenezaji magari wa Ujerumani wakasirishwa na ushuru wa EU
Lakini Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya inaonekana kuwa na mtazamo tofauti. Siku chache tu baada ya uchaguzi wa Bunge la Ulaya, mhimili huo wa utendaji wa umoja huo ulilitangaza ushuru wa adhabu wa hadi asilimia 38.1 kwa magari ya umeme ya China (EVs), licha ya ukosoaji kutoka kwa watengenezaji magari wa Ulaya na serikali ya Ujerumani.
Maafisa wa Umoja wa Ulaya wanasema hatua hiyo ilichochewa na China kutoa ruzuku kwa kampuni zake. Na licha ya shuru wa EU kuwa mkubwa, bado uko chini sana kuliko ushuru wa asilimia 100 uliotangazwa hivi karibuni na Marekani.
Kwa Hidlegard Müller, mkuu wa chama cha watengeneza magari cha Ujerumani, VDA, ushuru wa EU ni “hatua moja mbali ya ushirikiano wa kimataifa.” Mkurugenzi Mtendaji wa BMW, Oliver Zipse, alisema Halmashauri Kuu ya Ulaya “inadhuru makampuni ya Ulaya na maslahi ya Ulaya.”
Soma pia: Viongozi wa Ulaya wakutana na Xi Jinping
Ola Källenius, Mkurugenzi Mtendaji wa Merzedes-Benz, ambayo ukoo wake unakwenda nyuma zaidi ya karne moja kwa Carl Benz, alionya kwamba Ujerumani ilikuwa taifa linalotegemea mauazo ya nje lisilo na haja ya “kuongezeka kwa vikwazo vya biashara.”
Waziri wa Uchumi wa Ujerumani Robert Habeck pia alihimiza mazungumzo na kuonya dhidi ya “mashindano ya ushuru.”
Wakati huo huo, Beijing imeonyesha kutofurahishwa kwake. Siku ya Jumatano jioni, Wizara ya Biashara ya China iliahidi kuchukua hatua zote muhimu ili kulinda maslahi ya watengenezaji magari wa China. Maafisa walipuuza uamuzi wa EU kama usio na msingi na hatua ya kujilinda dhidi ya ushindani, wakidai shutuma za ruzuku “zilibuniwa na kukuzwa kwa njia isiyo halali.”
Wizara hiyo pia ilisema magari ya bei nafuu ya umeme yalikuwa muhimu kwa kuruhusu EU kufikia malengo yake ya kupunguza uzalishaji wa kaboni.
Mabadiliko ya kijani ‘katika hatari’
Mkuu wa VDA Hidlegard Müller aliunga mkono maoni hayo. “Tunahitaji China kutatua masuala ya kimataifa,” alisema. “China ina jukumu muhimu katika mageuzi yenye mafanikio kuelekea EVs na mfumo wa kidijitali. Mgogoro wa kibiashara unaweza kuweka mageuzi haya hatarini.”
Soma pia: Von der Leyen: Siku zijazo Ulaya huenda zikawa ngumu
Wanauchumi kwa muda mrefu wamekuwa wakifahamu juu ya mkakati wa China kuimarisha kwa makusudi baadhi ya sekta za viwanda ili kujaa soko na kupunguza bei ya kimataifa. Hakuna shaka kwamba Beijing inatoa ruzuku kubwa kwa makampuni yake, alisema mtaalamu wa uchumi wa DW Lars Halter.
“Hata hivyo, haiwezekani kutoa maelezo maalum kuhusu kiwango ch ruzuku,” aliongeza. “Sio tu suala la serikali kuhamisha fedha kwa makampuni. Pia wanahakikisha makampuni yanapata betri za bei nafuu au malighafi, au mikopo nafuu.”
Makabiliano ya wasafirishaji wakuu wa nje
Mwanasiasa wa Ujerumani Walter Döring aliwahi kuwa waziri wa uchumi na naivu waziri mkuu katika jimbo la Ujerumani la Baden-Württemberg. Sasa anaongoza Chuo cha Viongozi wa Soko la Dunia cha Ujerumani katika jiji la Schwäbisch Hall. Baden-Württemberg ni nyumbani kwa makampuni mawili makuu ya magari – Porsche na Mercedes – pamoja na kampuni nyingi ndogo zinazohusiana na magari.
“Kwa miaka mingi, Ujerumani ilikuwa bingwa wa mauzo ya nje duniani,” Döring alisema katika mkutano wa Stuttgart zaidi ya wiki moja iliyopita. “Siku zote tulijivunia kutoa bidhaa na huduma zetu kwa ulimwengu mzima. Hakuna mtu aliyewahi kutushtaki kwa uzalishaji kupita kiasi.”
“Leo tuna mashindano ya ubingwa wa kimataifa wa mauzo ya nje,” Döring aliongeza.
Soma pia: Marekani, China zakamilisha mazungumzo ya biashara
Linapokuja suala la magari, China ndio bingwa wa mauzo ya nje wa 2023, mbele ya Japan na Ujerumani. Lakini mauzo ya China kwenye uwanja wa nyumbani Ujerumani sio ya kuvutia kabisa. Mwaka jana, kampuni mbili kuu za utengenezaji magari ya umeme za China, BYD na NIO, kwa pamoja ziliuza chini ya magari 5,400 ya umeme katika nchi hiyo ya Umoja wa Ulaya.
Nani mwenye uwezekano mkubwa wa kuathiriwa na majibu ya China?
Wakati huo huo, mzuka juu ya magari ya umeme unaonekana kushuka barani Ulaya. Kwa mwanauchumi wa Ujerumani Ferdinand Dudenhöffer, ukosefu huu wa shauku umetengenezwa na wanasiasa.
“Gari la umeme ndiyo mustakabali,” alisema. “Wanasiasa wetu kwa ujinga wamepoteza hamu katika mustakabali.”
Shauku hii inayofifia yumkini inadhihirika katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kupunguza motisha zao kwa ununuzi wa EVs na “mtazamo wa jumla miongoni mwa wanasiasa kwamba magari ya mafuta kwa mara nyingine tena yana mustakabali.”
Mwishowe, hata kama vita vya kibiashara vitazuka, “Beijing haitaweka ushuru kwa bidhaa za Umoja wa Ulaya ambazo bado inazihitaji,” alisema Jakob Gunter kutoka Taasisi ya Mafunzo ya China ya Mercator, MERICS, yenye makao yake makuu mjini Berlin.
Soma pia: Trump kuzungumza na Xi kuhusu vita vya kibiashara
“Hii ni pamoja na mashine, bidhaa za thamani za viwandani, kemikali, teknolojia ya matibabu na bidhaa nyinginezo. Pia hakuna uwezekano wa kulenga viwanda vikubwa vya Ulaya vinavyowekeza kwa kiasi kikubwa nchini China, kutengeneza ajira, kulipa kodi na kuchangia ukuaji wa uchumi,” aliongeza.
Badala yake, kampuni zinazoathirika zinaweza kuwa zile zinazouza “bidhaa za kilimo, chakula na vinywaji ambavyo wateja nchini China wanaweza wakamudu bila kuwa nazo” au ambazo China tayari inazalisha kwa kiwango cha kutosha.