Geita. Kesi ya mauaji ya aliyekuwa mfanyakazi wa kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu ya Geita (GGML), Milembe Seleman inatarajiwa kuanza tena kusikilizwa kwa wiki mbili mfululizo kuanzia kesho Juni 18 hadi Juni 28, 2024.
Milembe (43), aliuawa Aprili 26, 2023 kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali mwilini, ikiwemo kichwani, usoni na mikononi.
Tayari mashahidi 11 kati ya 32 wa upande wa Jamhuri wameshatoa ushahidi wao wakiongozwa na mawakili wa Serikali, Merito Ukongoji, Grace Kabu wakisaidiana na Scolastica Teffe.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Dayfath Maunga (30), Safari Labingo (54), Genja Deus Pastoy, Musa Lubingo (33) na Ceslia Macheni (55) ambao wote wanakabiliwa na shtaka moja la mauaji.
Kesi hiyo namba 39 ya mwaka 2023, inasikilizwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Kelvin Mhina.
Aprili 12, 2024, shahidi wa 11 wa upande wa Jamhuri, G.4026, Ditektivu Koplo Darius ambaye ni askari polisi, Idara ya Upelelezi Wilaya ya Geita, aliieleza Mahakama kuwa mshtalkiwa wa kwanza, Maunga ndiye aliyewakodi wauaji kwa malipo ya Sh2.6 milioni.
Katika ushahidi wake akiongozwa na mwendesha mashtaka wakili wa Serikali, Merito Ukongoji, shahidi huyo aliieleza Mahakama kuwa ndiye aliyemhoji mshtakiwa huyo baada ya kukamatwa na kwamba katika mahojiano hayo alikiri kutenda kosa hilo, huku akieleza sababu na namna alivyofanikiwa kuwapata wauaji.
Sambamba na maaelezo hao, pia shahidi huyo aliwasilisha mahakamani hapo maelezo ya onyo aliyodai kuwa ya mshtakiwa huyo aliyoyarekodi wakati akimhoji kuhusiana na tuhuma hizo.
Aidha, maelezo hayo pia yalipokelewa mahakamani hapo na kuwa kielelezo cha tisa cha ushahidi wa upande wa mashtaka.
Washtakiwa hao wanatetewa na mawakili; Liberatus John (mshtakiwa wa kwanza), Laurent Bugoti anayemtetea mshtakiwa wa pili, Elizabeth Msechu anayemtetea mshtakiwa wa tatu, Erick Lutehanga na Yesse Lubanda anayemtetea mshtakiwa wa tano.