Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)- Bara, Tundu Lissu ametaja changamoto kubwa tatu zilizojitokeza kwenye mikutano yake 17 ya hadhara aliyoifanya mkoani Singida ikiwemo unyang’anyi wa ardhi wa kutisha.
Nyingine zilizojitokeza katika ziara hiyo iliyoanza tangu Juni Mosi, 2024 ni unyonyaji unaofanya na baadhi ya watumishi wa umma kwa kuanzisha michango kila kona na jambo lingine kodi na ushuru, huku akieleza yote hayo yanaongeza ugumu wa maisha.
Hayo ameyaeleza leo Jumatatu Juni 17, 2024 akiwa Itigi mkoani Singida, wakati akifanya tathimini ya mikutano yake 17 ya hadhara aliyoifanya mkoani humo ya kusikiliza kero na kutoa elimu kwa wananchi wajipange kufanya mageuzi ya kisiasa nchini kupitia chaguzi zijazo.
“Sasa nizungumze na nyie mtaendelea na haya hadi lini? Tutaendelea kunyonywa, kunyang’anywa ardhi na kuwa wajinga na kutiwa umaskini hadi lini.”
“Niwafundishe, mwaka huu tunaingia kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, sasa tujiulize tunataka kuendelea na ujinga au tunataka na sisi tupate unafuu,” amesema.
Lissu amesema wanatumia nguvu ya kura zao kufanya mageuzi ya kisiasa kwa kuchagua viongozi wa haki wanaotoka upinzani ili kuondoa manyanyaso yanayoendelea kutamalaki.
Akizungumzia kuhusu unyang’anyi wa ardhi aliodai umekithiri hasa eneo la Kiminyanga, Nkarama na Itigi, Lissu amesema mapori mengi yamechukuliwa na watu wanaoitwa wawekezaji na baadhi ya viongozi.
“Ardhi hiyo ni mali ya wananchi tangu enzi za ukoloni, misitu hii ni mali zetu kwa mujibu wa mila ni sehemu tunakopata kuni, matunda, miti ya dawa na tumefanya hivyo enzi na enzi na umiliki huo unalindwa na sheria ya Tanzania,” amesema Lissu ambaye ni mzaliwa wa Ikungi, mkoani humo.
Amesema misitu hiyo inafyekwa wanalima zao la mikorosho na watu ambao hawajali maisha na wananchi
“Gharama za uendeshaji wa shule zote zimehamia kwa wazazi. Wanasema elimu bure lakini wametuletea mzigo wa michango ambao haubebeki wazazi wanauza kila kitu kulipa michango,”amesema.
Amesema mtoto akianza shule ya msingi, sekondari hadi chuo hali imekuwa ngumu huku akieleza serikali imeshaacha utamaduni wa kushughulika na watoto wa maskini.
Amesema suala la kodi au ushuru unatozwa kila mwananchi hata akiwa mkulima kazi zote anazofanya akimaliza kuvuna ni mali zao hawezi kwenda mita tano bila kutozwa ushuru.
“Ukiwa mfugaji hivyo ukichinja lazima utozwe ushuru na ng’ombe wakiwa bado zizini lazima wavalishwe heleni ambazo zinatakiwa kulipiwa,”amesema.
Awali, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), John Pambalu amedai Serikali imeshapoteza uelekeo wa kuongoza nchi huku akieleza imefikia watu wameanza kujiuza.
Amesema ili kupata suluhu ya tatizo hilo la kiuchumi dawa yake ni kuwaondoa watawala madarakani kuweka safu nyingine itakayokuja kuleta mageuzi na kuwaneemesha wananchi wake.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa zamani wa Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa amesema wananchi wanapitia maisha magumu baada ya Serikali kuingia kwenye utekelezaji miradi mikubwa ikiwemo kuhamia Dodoma.
“Matokeo yake tumewekeza nguvu kukopa fedha nje ya nchi na mwisho wa siku mzigo anabeba mwananchi wa kawaida anayeendelea kudumaa, afya na elimu,” amesema.
Mchungaji Msigwa amesema vijana wengi wa Kitanzani wana umri mdogo lakini wakitazamwa wanaonekana wazee kutokana na ugumu wa maisha wanaopitia.
“Wananchi lazima mfanye mabadiliko ya kisiasa kwa kukiweka pembeni chama tawala kilichotawala miaka 60 na matokeo ni yaleyale hivyo lazima tubadilike,”amesema.
Kwa upande wake, Askofu Maximilian Machumu maarufu ‘Mwanamapinduzi’ amesema, “Msikubali rasilimali za nchi zitapotea na mwisho wa siku kizazi kinachokuja kitapata shida kimaisha kwa kukosa sehemu ya kuishi na kushindwa kufaidi urithi,” amesema.