‘Mtoto wa Afrika apewe elimu inayomwandaa kwa maisha ya baadaye’

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Mwenyekiti wa Chama cha Mabuddha cha China kilichopo hapa nchini, Master Xian Hong amesema bado kuna changamoto ya watoto wengi barani Afrika kutopata elimu na kusababisha kushindwa kufikia ndoto zao.

Ameyasema hayo Juni 16,2024 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika katika Shule ya Awali na Msingi LongQuan Bodhi, Dar es Salaam na kushirikisha watoto 200 kutoka vituo 15 vya kulea yatima vilivyopo katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam ambao wamepatiwa msaada wa vyakula na vifaa vya kujifunzia.

Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Abdallah Mtinika, akikabidhi vifaa vya kujifunzia na vyakula kwa mmoja wa watoto anayeishi katika mazingira magumu vilivyotolewa na Chama cha Mabudha cha China kilichopo hapa nchini kuadhimidha Siku ya Mtoto wa Afrika. Kushoto ni Mwenyekiti wa chama hicho, Master Xian Hong na Kulia ni Mwalimu Mkuu wa
Shule ya LongQuan Bodhi, Jane Shao.

“Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inasisitiza juu ya utoaji elimu kwa watoto, ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha haki ya elimu inapewa kipaumbele kwa watoto wote wa Afrika,” amesema Hong.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Jane Shao, amesema inamilikiwa na chama hicho pia ina kituo cha watoto wanaotoka katika mazingira magumu cha Longquan Bodhi Children Care Centre ambapo wanasomeshwa bure shuleni hapo.

Kwa mujibu wa Mwalimu Shao, watoto hao 20 tayari wamefundishwa lugha ya Kichina na kufanikiwa kushiriki katika mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa akiwemo Tausi Julius ambaye anatarajia kwenda China baadaye mwaka huu katika mashindano yajulikanayo kama Chinese Bridge Competition.

Meya wa Manispaa ya Temeke, Abdallah Mtinika, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo amekipongeza chama hicho kwa kulea watoto na kuwasaidia kwa mahitaji mbalimbali na kutaka wadau wengine kuiga mfano huo.

“Tunathamini mahusiano ya kihistoria yaliyopo baina ya China na Tanzania ambayo ni ya miaka mingi, niwapongeze kwa kujitoa kulea watoto, tunawakaribisha watu wa mataifa mengine kuiga mfano huu kwa sababu Serikali haiwezi kufanya kila kitu.,” amesema Mtinika.

Amesema pia wameunda mabaraza katika mitaa 142 ambapo watoto wamekuwa wakikutana na kujadili masuala yanayohusu haki, ulinzi na maendeleo yao.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika mwaka 2024 inasema ‘Elimu jumuishi kwa watoto izingatie maarifa, maadili na stadi za kazi’ ikisisitiza umuhimu wa kutoa elimu inayomuandaa mtoto kwa maisha ya baadaye.

Related Posts