Nondo za Cecafa Kagame Cup 2024

Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), limetangaza kwamba mashindano ya Cecafa Kagame Cup mwaka 2024 yatafanyika Tanzania Bara na Zanzibar kuanzia Julai 6 hadi 22 mwaka huu.

Katika taarifa yao ya awali iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa CECAFA, John Auko Gecheo, ilionyesha timu shiriki zitakuwa 16 huku tatu zikiwa ni mwalikwa na 13 zinatokea Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Timu tatu mwalikwa ni TP Mazembe (DR Congo), Nyasa Big Bullets (Malawi) na Red Arrows FC ya Zambia.

Awali, mashindano hayo yalipangwa kufanyika kuanzia Julai 20 hadi Agosti 4 mwaka huu nchini Tanzania, lakini kutokana na ratiba ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuonyesha kuanza Agosti mashindano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho yanaanza, Cecafa limeona mashindano yao yaanze mapema na kumalizika siku chache kabla ya kuanza kwa mtifuano wa michuano ya CAF ngazi ya klabu msimu wa 2024/2025.

Michuano hiyo imerejea baada ya kutofanyika kwa miaka miwili tangu mara ya mwisho iliposhuhudiwa Express ya Uganda ikiwa bingwa mwaka 2021.

Mara ya mwisho michuano hiyo ilifanyika Tanzania mwaka 2021 na Express ya Uganda ilitwaa kombe kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya waalikwa, Nyasa Big Bullets.

Baada ya 2021, michuano hiyo haikufanyika mwaka 2022 na 2023 huku sababu kubwa ikitajwa ni muda uliopangwa kufanyika kutokuwa rafiki kwa timu shiriki.

Mara nyingi michuano hiyo imekuwa ikifanyika Julai na Agosti, muda ambao timu nyingi huwa katika maandalizi ya msimu mpya.

Wakati ambao imeahirishwa, ilitokana na ratiba ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuzibana timu nyingi zilizopaswa kushiriki kutokana na michuano yao hivi sasa kuwahi kuanza ambapo huwa Agosti.

Baadhi ya timu zilisema haziwezi kushiriki mashindano hayo kwa sababu zimewaruhusu wachezaji wake kwenda mapumzikoni kutokana na kalenda ya michuano hiyo kuchelewa kutolewa, lakini klabu nyingine zikidai zimejipanga kuweka kambi ughaibuni kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.

Sababu zote hizi, zilichangia ‘kuua’ au kuondoa ladha ya ushindani ambayo ilizoeleka wakati wote wa mashindano haya yalipokuwa yakifanyika.

Ukiangalia sababu hizo zina mashiko makubwa kwani msimu wa soka Tanzania umemalizika Juni, baada ya hapo timu zimetoa mapumziko ya takribani mwezi mmoja kwa wachezaji wao, wanatarajia kurudi kambini mwanzoni mwa Julai.

Timu nyingi zimekuwa zikisema kutokana na hilo, zinaporudi kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya, haitakiwa kuanza na mashindano kwani wachezaji huwa wametoka kwenye mapumziko, lazima waanze mazoezi mepesi kabla ya kuchanganya.

Wakati michuano hiyo ikirejea, kabla ya kuanza imeibuka sintofahamu ambayo inaweza kuifanya kutokuwa na mvuto na pengine kutofanyika.

Hiyo inatokana na timu zilizotajwa kushiriki, baadhi kutangaza kujitoa kutokana na ratiba kuwabana.

Azam FC kupitia Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano, Zakaria Thabit ‘Zaka Zakazi’ amethibitisha kwamba timu yao haitashiriki.

Mabingwa hao wa Kagame Cup mwaka 2015 na 2018, wametoa sababu ya kutoshiriki ni kutokana na muda uliopangwa kutokuwa rafiki kwani tayari wamewapa mapumziko wachezaji wao na wanatarajiwa kurudia kambini Julai 4 kuanza maandalizi ya msimu mpya, yaani siku mbili kabla ya kuanza kwa michuano hiyo.

“Ili timu iweze kukuonyesha kitu inahitaji kufanya mazoezi ya ‘pre season’ kwa muda wa wiki sita, sasa sisi tutaanza kambi siku mbili kabla ya kuanza mashindano,” alisema Zaka Zakazi.

Kwa upande wa uongozi wa Yanga, bado haujatoa majibu ya moja kwa moja kama timu yao itashiriki mashindano hayo ambayo wana rekodi ya kubeba ubingwa mara tano.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, alisema: “Uongozi utatoa tamko, wanachama na mashabiki watulie, tutatoa tamko letu rasmi kuhusiana na mashindano haya.”

Yanga nao ni kama wapo njiapanda kushiriki mashindano hayo kutokana na ratiba pia kuwabana kwani hivi sasa wametoa mapumziko ya mwezi mmoja kwa nyota wao amabao watarudi mwanzoni mwa mwezi ujao.

Baada ya kurejea kambini, timu hiyo imepanga kwenda kufanya maandalizi ya msimu ujao nje ya nchi ambapo hadi sasa kuna mwaliko kutoka Kenya, Afrika Kusini na Urusi.

Ukiachana na sintofahamu hizo mbili kutoka kwa Azam na Yanga, upande wa wawakilishi kutoka Zanzibar ambao ni JKU, nao wamewekwa kando na mamlaka za soka visiwani humo.

Taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Mohamed Kabwanga, ilibainisha kwamba, hawaitambui JKU kama mwakilishi wao katika mashindano hayo kwani bado hawajathibitishwa kuwa mabingwa wa msimu huu.

“Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) linapenda kutoa ufafanuzi kuhusu timu itakayoshiriki mashindano ya CECAFA Kagame Cup 2024 kufuatia taarifa iliyotolewa na CECAFA ikionyesha timu ya JKU SC kutoka Zanzibar ndiyo itakayoshiriki mashindano hayo.

“Hatua hiyo iliyofanywa na CECAFA kuichukua timu inayoongoza katika msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar kwa sasa bila ya ligi kumalizika rasmi na kabla ya bingwa kupatikana haikuwa sawa kwa mujibu wa kanuni za ZFF.

“Hivyo basi ZFF itaitambua timu yoyote ambayo itakuwa bingwa katika Ligi Kuu Zanzibar ndiyo itakayoshiriki mashindano hayo na mashindano Klabu Bingwa ya CAF na sio vinginevyo.

“Kwa taarifa hiyo, ZFF linawatoa hofu timu zote za Ligi Kuu Zanzibar, mashabiki na wadau wa mchezo wa mpira wa miguu kuwa ZFF haikuhusika kuichagua JKU kuwa ndiyo timu pekee itakayoshiriki mashindano ya CECAFA Kagame Cup,” ilisema taarifa hiyo iliyotolewa Juni 11, 2024.

Kutokana na sintofahamu hiyo, timu za Tanzania Bara ambazo ushiriki wao unaweza kusema hauna shaka kutokana na orodha iliyotolewa na CECAFA ni Coastal Union pekee kwani hata Simba hadi sasa wamekuwa mguu mmoja ndani mwingine nje.

Ahmed Ally, Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba, amesema: “Kama klabu tumepata taarifa za kuwepo kwa mashindano ya Kagame Cup, tutakaa na kuangalia uwezekano wa kushiriki.”

Ukiachana na timu tatu zilizoalikwa ambazo zimeainishwa hapo juu huku Simba, Yanga, Azam na JKU zikibaki kwenye sintofahamu, zingine kutoka Ukanda wa Cecafa zitakazoshiriki kwa mujibu wa CECAFA ni Vital’O (Burundi), APR (Rwanda), El Merreikh, Al Hilal, Hai El Wadi (Sudan), Gor Mahia (Kenya), SC Villa (Uganda), El Merreikh FC-Bentiu (Sudan Kusini), Nyasa Big Bullets (Malawi), TP Mazembe (DR Congo), Red Arrows (Zambia) na Coastal Union (Tanzania).

Mpaka sasa mashindano hayo bado yamebeba jina la Rais wa Rwanda, Paul Kagame, kutokana na ufadhili wake mbalimbali anaotoa ikiwemo fedha za zawadi kwa washindi (Dola za Marekani 60,000) ambapo mshindi anapata Dola za Marekani 30,000, atakayeshika nafasi ya pili anazawadiwa Dola za Marekani 20,000 na yule wa tatu Dola za Marekani 10,000.

Mbali na zawadi hizo, Rais Kagame pia anatoa Dola za Marekani 15,000 kila mwaka kwa maandalizi ya michuano hiyo na kufanya mchango wake jumla kuwa dola 75,000.

Simba SC ndio mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo baada ya kushinda mara sita katika miaka ya 1974, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002, ikifuatiwa na Gor Mahia ya Kenya iliyoshinda mara tano katika miaka ya 1979, 1982, 1983, 1984 na 1997.

Yanga ya Tanzania nayo imeshinda taji hilo mara tano katika miaka ya 1975, 1993, 1999, 2011 na 2012 sawa na Tusker, zamani Breweries ya Kenya katika miaka ya 1988, 1989, 2000, 2001 na 2008.

Michuano hii hushirikisha mabingwa wa nchi kutoka Ukanda wa CECAFA huku mwenyeji akiwa na faida ya kuingiza timu nyingi kuzidi wenzake.

Mwaka huu, Tanzania ni mwenyeji, amepata nafasi ya kuingiza timu nne ambazo zote zinakwenda kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao.

Kutokana na timu hizo kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao, Uongozi wa CECAFA umesema utakuwa wakati mzuri kwa kufanya maandalizi ya kwenda kufanya kweli huko kimataifa kwani timu zinazoshiriki Kagame Cup, wanaamini zitatoa ushindani wa kweli.

“Mashindano haya yatasaidia timu zetu katika ukanda huu kujiandaa vizuri kabla ya msimu wa CAF Champions League na CAF Confederation Cup 2024/2025 ambao unaanza mwezi Agosti. Kuwa na timu kubwa kutoka DR Congo, Malawi na Zambia pia kutatoa pa msisimko kwenye mashindano yetu na kutoa changamoto halisi kwa timu zetu,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa CECAFA, John Auko Gecheo.

Faida nyingine ya mashindano haya ni kutoa nafasi kwa wachezaji kujiweka sokoni kwani hiki ni kipindi cha usajili.

Related Posts