Shida ya maji inavyowanufaisha wengi

Dar es Salaam. Wananchi ambao hawajaunganishwa na mtandao wa maji mkoani Dar es Salaam wanapitia maumivu wakilazimika kupata huduma hiyo kwa gharama kubwa.

Wakati uniti moja ya maji (lita 1,000, sawa na ndoo 50 za lita 20) ikiuzwa Sh1, 663 na mamlaka husika, wafanyabiashara wa maji wanayauza kwa Sh15, 000 wanapoyafikisha kwa mteja.

Bei ya Sh1,663 kwa uniti moja inatumiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) kama ilivyopangwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura).

Haijaeleweka bei ya Sh15, 000 imepangwa na nani, lakini inayotajwa kuwa ni njia ya kujitafutia utajiri kupitia kero ya maji.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi hivi karibuni katika maeneo tofauti ya Dar es Salaam, wamesema wanalazimika kuyanunua bei hiyo kwa sababu hawajafikiwa na mtandao wa maji.

“Huku maji hayajafika, tunategemea ya visima ambayo siyo salama kwa kunywa au kupikia, hivyo nikinunua maji ya Sh15, 000 yanaweza kunisukuma hata wiki mbili kwa ajili ya kunywa na kupikia,” anasema Annet Joseph anayeishi Mbezi Msumi.

Maelezo hayo yanafanana na ya Mussa Mapege anayeishi Mbezi Malamba Mawili, anayesema huduma ya maji haipo maeneo yao.

“Huku Mbezi hata uchimbaji wa visima ni mgumu, kwa hiyo inabidi tu ununue maji, vinginevyo tunategemea madimbwi nyakati za mvua,” anasema.

Kwa upande mwingine, wenye viwanda vya vinywaji nao wameelezea adha wanayopata kiasi cha kulazimika kuuagiza maji kwa magari.

Mwakilishi wa kiwanda cha kuzalisha soda cha Pepsi Dar es Salaam, Foti Gwebe anasema kuna shida kubwa ya maji, hali inayoongeza gharama za uzalishaji.

“Shida ni kubwa, hatupati maji ya kutosha, hivyo inatulazimu kuagiza kwa kutumia magari (bowsers).

“Tunapata maji mara tano kwa wiki wakati matumizi yetu ni lita milioni mbili kwa siku, hivyo maji hayatoshi. Tukiagiza maji kwa gari, lita moja ni kati ya Sh7 hadi Sh8, kwa hiyo gharama zinaongezeka.”

Kwa upande wake Chengal Reddy, ofisa katika kiwanda cha A-One kinachosindika maji ya kunywa, anasema maji wanayopata kutoka Dawasa hayatoshi kwa uzalishaji.

“Huwa tunaagiza maji kutoka kwa wauzaji wengine ili kufidia mahitaji. Hii ni shida ya muda mrefu, kwa hiyo hatuoni haja ya kwenda kuwaeleza Dawasa,” amesema.

Fauzia Malik, mmiliki wa kiwanda cha usindikaji maji cha Cool Blue anasema aliamua kuhamisha kiwanda kutoka Mikocheni, Dar es Salaam kwenda Mkuranga mkoani Pwani kutokana na shida ya maji.

“Awali kiwanda chetu kilikuwa Mikocheni, tukawa hatupati maji ya Dawasa, wakati huo mahitaji yalikuwa makubwa, lakini hatukuweza kuzalisha kukidhi soko,” anasema.

“Mwaka 2017 tukahamishia kiwanda chetu wilayani Mkuranga mkoani Pwani ambako tumechimba visima, tunapata maji ya kutosha. Yale maji tunatibu kwa dawa yanakuwa na viwango vya ubora unaotakiwa,” anasema.

Hata hivyo, anasema changamoto anayopata sasa ni umbali na masoko.

Wakati viwanda hivyo vikieleza hayo, Kiwanda cha Coca Cola Kwanza kilichopo Mikocheni nachi, kinapata maji ya kutosha, kama ilivyoelezwa na uongozi wake.

“Kwa sasa tunapata maji ya kutosha, ni mwezi mmoja uliopita ndiyo tulipata changamoto, tukawaita Dawasa wakaja wakasema kulikuwa na shida ya valvu, hivyo walirekebisha,” anasema, Unguu Suley, mkurugenzi mtendaji Coca cola Kwanza, alipozungumza na Mwananchi mwishoni mwa Aprili, 2024

Wakati Dawasa ikisema inauza maji kwa wafanyabiashara kwa Sh1, 663 kwa uniti moja, baadhi yao wameeleza kinyume chake.

Feisal Said, mfanyabiashara ya maji maeneo ya Mbezi, anasema huyanunua kwa Sh5, 500 kwa lita 1,000.

“Tunauza maji maeneo ya Mbezi Msumi na Mpigi Magoe kwa Sh15, 000,” anasema.

Anasema kazi hiyo ni ya msimu, kwani wakati wa mvua mahitaji hupungua.

“Kwa msimu wa jua ndiyo unaweza kwenda hata safari tano, lakini msimu wa mvua tunakwenda mara chache na kazi inakuwa na changamoto nyingi, ikiwemo ubovu wa barabara,” anasema.

“Huwezi ukaenda kuchukua gari la bosi halafu siku nzima ukaenda safari mbili,” anasema.

Said anasema kwa siku anatakiwa apeleke hesabu ya mwenye gari ya Sh60, 000.

“Maji ununue Sh5, 500, ununue mafuta ya gari, pia ununue mafuta ya pampu ya kushushia maji, kwenye gari uko utingo na dereva, bado hujapata posho yenu na ya bosi, kwa hiyo ukifanya safari mbili ni hasara,” anasema.

Hata hivyo, anasema kwa sasa kuna miradi mingi ya maji, hivyo biashara imepungua.

Vincent Peter, dereva wa gari kubwa la maji anasema akipeleka safari moja, huuza Sh100, 000 kwa kuwa gari lake linabeba zaidi ya lita 5,000.

Hata hivyo, anasema licha ya faida wanayopata, biashara hiyo ina changamoto nyingi.

“Ni mpaka upewe oda na mteja ndiyo upeleke. Kwa mfano unaona sasa gari kama hilo hapo limekaa wiki nzima halina kazi. Mwenye gari anaona hali yenyewe, kwa hiyo siku asipopata hesabu anaelewa. Kwa msimu wa mvua hali ndiyo inakuwa mbaya,” anasema.

Mfanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina moja la Mrema, anayeuza maji eneo la Mbezi anasema hununua matanki matatu ambayo ni sawa na uniti tatu kwa Sh6, 000, kisha huyauza kwa Sh45, 000.

“Sasa hapo ukitoa gharama za mafuta lita tano kwa siku (Sh16, 000), hesabu ya mmiliki wa gari ni Sh50,000 na matengenezo ya gari kila linapoharibika. Biashara yenyewe inategemea na hali ya hewa. Kipindi cha mvua hakina biashara, unaweza ukaenda safari moja siku nzima au usipate kabisa mteja, kwa sababu wanakinga maji ya mvua,” anasema.

Kauli hiyo imeungwa mkono na mmiliki wa magari ya kubeba maji, Adam Rashid, anayesema biashara hiyo ina gharama kubwa.

“Magari mengi yanayotumika hapa ni Mitsubishi Canter, bei yake sokoni ni Sh48 millioni. Ukilisajili kwa biashara hii sharti ulipe kodi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Sh500, 000 kwa mwaka, kibali cha Dawasa Sh200, 000 kwa mwaka, kibali cha Wakala wa Vipimo Sh33, 000 kwa mwaka, bima ya gari Sh1.2 milioni. Gharama zote hizi zinafanya biashara iwe ngumu, japo tunapambana vivyo hivyo,” anasema.

Rashid anasema ameanza biashara mwaka 2004 na kadiri miaka inavyozidi kwenda biashara inazidi kupungua kwa kuwa miradi ya maji inaendelea kujengwa.

“Awali, kwenye kikundi chetu tulikuwa na zaidi ya wanachama 600 lakini sasa tumebaki 28 hapa Mbezi. Tulikuwa tunapeleka maji Sinza, Kigogo, Ubungo, Kimara Bonyokwa, Saranga na maeneo ya Mbezi Malamba mawili,” anaeleza.

“Lakini kote huko sasa kuna miradi ya maji, mahitaji yamepungua. Kwa sasa soko letu limebaki Mbezi Msumi, Msakuzi na maeneo mengine,” anasema.

Kwa mujibu wa Dawasa, biashara ya maji inafanyika kwa kufuata Kanuni za Maji na Usafi wa Mazingira, huduma ya magari ya majisafi za mwaka 2023, sura namba 272, kifungu cha 29 (1) (m) ambazo zinaelezea masharti, taratibu za kusajili na kufuta usajili, bei, majukumu kwa pande zote mbili.

“Dawasa imesajili magari 55 ya majisafi ikisimamiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) kwa kuyatambua na kuyasajili magari hayo, kusimamia usalama wa walaji kwa maana ya kuyasafisha kwa kutumia dawa za kuua vijidudu,” inaeleza taarifa ya Dawasa.

Akizungumza na Mwananchi, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Kiula Kingu anaema wafanyabiashara ya maji wanauziwa bei ya kawaida ya Sh1,663 kwa kila mita moja ya ujazo (uniti moja).

Hata hivyo, amesema hakuna mwongozo wa kwenda kuuza kwa mnunuzi wa mwisho, akisema hilo ni jukumu la Ewura.

“Hakuna mwongozo ambao Ewura wameutoa wa kudhibiti uuzaji kwa sababu kila mmoja anauza kwa umbali tofauti na kulingana na gharama wanazotumia, kwa hiyo ni maelewano kati yao na wateja wanaonunua maji,” amesema.

“Sisi siyo watoa mwongozo wa tozo, Ewura ndio wanaofanyia kazi,” anasema.

Hata hivyo, Meneja mawasiliano wa Ewura, Titus Kaguo anasema Dawasa ndio wanapaswa kusimamia biashara hiyo.

“Dawasa ndio anayetakiwa kuwadhibiti hao wenye magari. Sisi bei tunayompa ni ya eneo la kuchukulia maji, kwamba wewe ukiwa na gari ukienda Dawasa bei yako itakuwa ni hii,” anasema.

“Kwa hiyo, katika maeneo ambayo kuna maboza atakayesimamia hayo magari ni Dawasa, hata unapoomba leseni unapeleka kwake.”

“Yeye (Dawasa) kimsingi anatakiwa kutoa maji, ndiyo maana tunasema wewe hujafikisha maji Kimara, unatakiwa usimamie operesheni ya magari,” amesema.

Kwa mujibu wa Kingu, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya maji na usafi wa mazingira.

Hata hivyo, anasema inakuwa vigumu kwa kuwa huduma hiyo ni gharama kubwa.

“Sidhani kwamba Serikali ina hela ya kuhakikisha kila mmoja anapata maji nyumbani kwake, kwa hiyo miradi inayotekelezwa ni kutokana na fedha zilizopo na bajeti ambayo imepitishwa.

“Kila mradi unahitaji fedha, kwa hiyo hata wale wenye maboza wanavyofanya maana yake wanahudumia walio mbali, lakini Serikali ni kuhakikisha watu wanapata maji, ndiyo maana kila siku miradi inakuja,” amesema.

Pamoja na dhamira ya Serikali kupeleka maji kwa wananchi, amesema hawatarajii huduma hiyo itawafikia kwa asilimia 100.

“Kwa sababu leo unafikisha maji hapa, kesho watu wanajenga sehemu nyingine na wanapojenga hakuna maelekezo kwamba kabla hujajenga hakikisha kuna maji,” anasema.

Anasema kuna miradi inayoendelea kufanyiwa kazi ukiwemo wa Kusini ya Dar es Salaam utakaogharimu Sh39.6 bilioni, mradi wa Pugu Majohe na mradi wa Goba, ambayo amesema ikikamilika itapunguza kero ya maji.

“Tunafanya lakini watu wanaongezeka, lakini siyo kwamba ili wauza maji wafanye biashara sana, bali kwa sababu Serikali inapambana usiku na mchana watu wapate maji, ndiyo maana tumeambiwa tufikishe asilimia 95,” amesema.

Itaendelea kesho tukiangazia jinsi Kigamboni wanavyotamani kupata maji ‘baridi’.

Related Posts