Simulizi, historia, utukufu na hatari za Mlima Everest

Mlima Everest unaojulikana pia kama Sagarmatha nchini Nepal na Chomolungma nchini Tibet. Ni mlima mrefu zaidi duniani, ukiwa na urefu wa mita 8,848 kutoka ya usawa wa bahari. Mlima huu unavutia watalii kutoka kila pembe ya dunia, na ni alama ya changamoto, ujasiri na maajabu ya asili.

Jina “Sagarmatha” linatokana na lugha ya Kinepali. “Sagar” maana yake ni anga au mbingu, na “Matha” likiwa ni neno linalomaanisha “paji la uso”. Kwa pamoja, maneno haya yanamaanisha “Paji la Uso la Anga.” Jina hili linaashiria urefu na ukubwa wa mlima huu unaogusa mawingu.

Kwa upande wa Tibet, mlima huu unajulikana kama “Chomolungma,” ambalo linamaanisha “Mama wa Dunia.” Hii inaonyesha jinsi mlima huu unavyoheshimiwa na wenyeji wa Tibet kama sehemu takatifu na muhimu sana kiutamaduni.

majina haya mawili—”Sagarmatha” na “Chomolungma”—yanaonyesha jinsi Mlima Everest unavyotazamwa kwa heshima na uzito mkubwa katika tamaduni za Nepal na Tibet. Yanatoa picha ya urefu na ukubwa wa mlima huu, pamoja na umuhimu wake wa kitamaduni na kiroho kwa watu wa maeneo hayo.

Kwa nini jina Everest badala ya Sagarmatha au Chomolungma

Mlima Everest unaitwa hivyo kutokana na historia ya kugunduliwa kwake na ramani zake zilizoandaliwa Waingereza katika karne ya 19.

Ziko sababu kadhaa kadhaa kwanini jina “Everest” lilitumiwa na badala ya “Sagarmatha” au “Chomolungma”.

Kwanza, mlima huu ulipewa jina la “Mlima Everest” na mwanajiografia wa Uingereza Sir Andrew Waugh, ambaye alikuwa Mhakiki Mkuu wa India (Surveyor General of India) wakati huo.

Sir Waugh aliamua kuupa mlima huo jina la mtangulizi wake, Sir George Everest, ambaye alikuwa Mhakiki Mkuu wa India kabla yake. Sir George Everest alitoa mchango mkubwa katika upimaji na uchoraji wa ramani za Himalaya.

Pili, wakati wa upimaji wa mlima huo uliofanywa na Waingereza, jina “Chomolungma” lilikuwa linajulikana katika Tibet, lakini halikuwa linafahamika sana nje ya jamii za wenyeji za Tibet na Nepal. Kwa upande wa Nepal, jina “Sagarmatha” lilikuja kutumika rasmi baadaye. Hivyo, kwa wakati huo, jina la kienyeji halikuwa limetambulika kwa upana wa kimataifa.

Tatu, wakati wa utawala wa kikoloni wa Uingereza katika Asia ya Kusini, Waingereza walikuwa na mamlaka ya kutoa majina ya kijiografia kwa maeneo waliyochunguza na kuyachorea ramani. Hii ilisababisha kuwapo kwa matumizi ya majina ya kizungu kwenye ramani na machapisho rasmi.

Nne, baada ya jina “Everest” kutambulika kwenye ramani za kimataifa na machapisho ya kijiografia, lilianza kutumika sana katika jamii ya wapanda milima na watafiti kote duniani. Jina hili likawa maarufu na likatambuliwa kimataifa, hivyo lilidumu katika matumizi hadi leo.

Kwa hivyo, licha ya kuwa na majina ya kijadi yenye maana kubwa katika lugha na tamaduni za Nepal na Tibet, jina “Everest” limeendelea kutumika kimataifa kutokana na historia ya ugunduzi na urithi wa kikoloni wa Uingereza.

Hata hivyo, majina ya kienyeji “Sagarmatha” na “Chomolungma” bado yanaheshimiwa na kutumiwa na jamii za maeneo hayo, zikionyesha umuhimu wa kijiografia na kitamaduni wa mlima huo.

Kwa kuwa Mlima Everest ni sehemu ya Milima ya Himalaya, inavyojulikana kama “Paa la Dunia,” si tu kwamba kilele chake cha mita 8,848 (futi 29,029), una rekodi ya kuwa mlima wenye kilele kirefu zaidi duniani, pia una matukio mengi ya kihistoria na kijiografia.

Kwa karne nyingi, Mlima Everest umekuwa lengo la safari zenye changamoto kwa wapanda milima, kila mmoja akitafuta kushinda mapambano ya asili katika kupanda mlima huo.

Lakini zaidi ya kuwa kivutio kwa wapanda mlima, mlima huu wa kifahari pia ni maabara kubwa ya watafiti wa kijiografia, ambao huchunguza mifumo ya hewa, jiolojia na sayansi ya hali ya hewa.

Kupitia juhudi zao, wamegundua mafumbo mengi ya asili na kuongeza uelewa wa binadamu wa sayari yetu. Kwa maana hii, si tu kwamba Mlima Everest ni kivutio cha wapanda milima, bali pia ni kito cha thamani kwa utafiti wa kisayansi na kijiografia.

Kivutio kwa wapanda milima

Kutafuta kilele cha Mlima Everest ni safari ya kipekee, iliyofunikwa na changamoto na utukufu wa asili. Edmund Hillary, mmoja wa watu wa kwanza kufika kilele cha mlima huo, anakaririwa na kitabu ‘Sir Edmund Hillary Explores Mount Everest’ cha Heather Moore Niver, akisema:

“Mlima Everest … unaweza kuushinda ikiwa tu unaamini kwamba unaweza kufanya hivyo.” Maneno haya yanasisitiza kwamba kufikia kilele cha Everest ni safari inayohitaji si tu ujasiri na azimio, bali pia imani katika uwezo wa binadamu kushinda vikwazo vya asili.

Edmund Hillary, raia wa New Zealand, na Tenzing Norgay, mzaliwa wa Khumbu, Nepal, walikuwa watu wa kwanza kufika kilele cha Mlima Everest Ijumaa ya Mei 29, 1953.

Hata hivyo, mafanikio katika kupanda Everest hayaji bila gharama. Kama ilivyosemwa na Jon Krakauer, mwandishi wa riwaya maarufu ‘Into Thin Air’: “Hakuna uhuru wa kwenda Everest; kila mtu anahitaji kupewa ruhusa.”

Hii inaonesha jinsi kupanda mlima huo kunavyohitaji maandalizi makini, pamoja na kibali cha Serikali na ushirikiano na wapagazi na waongoza wakufunzi wenye uzoefu.

Lakini, licha ya hatari na changamoto, watu wanaendelea kuvutiwa na uzuri na umuhimu wa mlima huo. Kama alivyoandika George Mallory, mwandishi wa kwanza ambaye alijaribu kupanda Everest, katika kitabu chake, ‘Climbing Everest: The Complete Writings of George Mallory’ cha mwaka 2022 akishirikiana na ‎Peter Gillman: “Kwa nini tunapanda? Kwa sababu mlima upo.”

Maneno haya yanaonesha kiu ya binadamu ya kuchunguza na kushinda mazingira magumu, na hamu ya kufikia maeneo ambayo yanaonekana kuwa nje ya uwezo wa binadamu.

Hivyo, ingawa safari ya kuelekea kilele cha Everest inaweza kuwa ngumu, imejaa hatari na inahitaji maandalizi makini, ni nafasi ya kipekee ya kutafakari juu ya uwezo wa binadamu na kutafuta utukufu wa asili.

Kupanda Mlima Everest si tu suala la kufikia kilele cha juu zaidi, bali pia ni mtihani wa uvumilivu, ujasiri na uwezo wa kukabiliana na changamoto. Mipango na maandalizi ya kupanda Everest yanaweza kuchukua miezi au hata miaka, na wapandaji wanakabiliwa na hali ngumu kama vile baridi kali, upepo mkali, ukosefu wa oksijeni na hatari za kijiografia kama maporomoko ya theluji.

Hata hivyo, sio wapandaji wote wa mlima huo hufanikiwa. Wengine huporomoka kwenye mlima na kupotea. Je, ni mambo gani mahususi yanayosababisha kupotea na kufa? Je, kunakuwa na hali mbaya ya hewa, matatizo ya vifaa au makosa ya kibinadamu yanayochangia hali hiyo? Je, miili ya wapandaji hao hupatikana? Ikiwa ndivyo, imepatikana vipi?

Kupata majibu ya maswali haya na mengine, tukutane toleo lijalo.

Related Posts