FOUNTAIN GATE imeanza mazungumzo ya kumuongezea mkataba mpya nyota wa timu hiyo, Deus Kaseke aliye huru kwa sasa.
Kaseke ameitumikia Fountain kwa miaka miwili tangu alipojiunga mwaka 2022 akitokea Yanga aliyodumau nayo kwa miaka saba tangu 2015 alipotokea Mbeya City, huku viongozi wakiamini bado ana uwezo mkubwa wa kuwasaidia msimu ujao.
YANGA Princess imedaiwa kurudi tena kwa kiungo wa JKT Queens, Amina Bilal kuulizia ofa waliyotuma kumtaka mchezaji huyo kwa msimu ujao.
Yanga ilikuwa na machaguo mawili kumpata Diana Msewa ambaye ilisitisha mazungumzo na kiungo huyo hadi sasa inadaiwa amekataa ofa ya Yanga hivyo wameamua kurudi kwa Amina aliyewahi kuitumikia kabla.
KENGOLD iliyopanda Ligi Kuu, imeanza mazungumzo ya kumnasa straika Mcameroon, Daniel Fotso aliye huru baada ya kuachana na Acireale Calcio ya Italia.
Nyota huyo aliyeitumikia timu ya vijana ya Cameroon na klabu za AS Roma ya Italia na Dynamo Zagreb ya Croatia U17 na U19 anawinda na KenGold kuziba nafasi ya Edgar William anayetakiwa Pamba Jiji, Singida Black Stars. Daudi Elibahati
UONGOZI wa Ceasiaa Queens umeanza mazungumzo na beki wa kulia wa Geita Gold Queens, Patrisia Salum kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL).
Beki huyo mwenye uwezo wa kucheza kama winga, mkataba wake unaisha na timu hiyo ambayo imeshuka daraja msimu huu.
BAADA ya Yanga Princess kumalizana na Kaeda Wilson kwa sasa ipo mbioni kukamilisha dili la kiungo wa Fountain Gate Princess, Protasia Mbunda anayemaliza mkataba na timu hiyo.
Inadaiwa, Yanga inamuona Protasia ndiye mbadala Mzungu Kaeda anayerudi kwao Marekani kuendelea na masomo akiifungia timu hiyo mabao matatu katika Ligi ya WPL msimu huu. Nevumba Abubakar
MABOSI wa Geita Gold wapo katika harakati za kumrejesha aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Fredy Felix ‘Minziro’.
Minziro kwa sasa yupo Kagera Sugar, ikielezwa huenda akaachana na timu hiyo, jambo lililowafanya mabosi wa Geita kumvizia wakiamini uzeofu alionao utawarejesha Ligi Kuu Bara baada ya kushuka hivi karibuni.
KLABU za KMC na Kagera Sugar zinadaiwa kumnyemelea beki wa zamani wa Yanga na Singida FG, aliyemaliza mkataba Ihefu, Paul Godfrey ‘Boxer’, ili kumsajili. Rafiki wa karibu na beki huyo anayemudu winga, alisema mbali na timu hizo mbili, lakini Boxer pia ana ofa kutoka kwa timu nyingine za Ligi Kuu Bara.