KUNDI la vijana wanaojishughulisha na uchimbaji wa chokaa katika kijiji cha Nanyala wilayani Mbozi mkoani Songwe wameiomba serikali na wadau wengine kuwapatia mikopo ili waongeze tija katika shughuli zao za uzalishaji. Anaripoti Ibrahim Yassin, Songwe…(endelea).
Kundi hilo la vijana zaidi ya 300 wametoa maombi hayo ili waweze kuchimba na kuchoma chokaa kisasa kwa kutumia makaa ya mawe kwa sababu sasa huchoma kwa kutumia kuni.
Wakizungumza leo Jumatatu wamesema njia wanazotumia zimetafsiriwa kuwa ni uharibifu wa mazingira kutokana na kutumia kuni nyingi zinazokatwa kwenye mapori.
Fransis Siame ambaye ni mchimba chokaa, amesema wamekuwa wakitumia magogo ya kuni wanazozinunua mikoa ya jirani na wanapochoma kwenye mashimo ya kienyeji wanaipua na kuyasaga mawe hayo kwenye mashine ndipo wanapopata chokaa.
Naye Daud Mwanyerere mchimbaji wa chokaa kutoka Nanyara amesema licha ya kupata manufaa mengi hasa kipindi hiki cha utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan, wanaomba uwezeshaji wa mikopo ili waachane na kutumia kuni waweze kuagiza makaa ya mawe.
Kalantin Paul naye amsema pamoja na mafanikio waliyonayo changamoto nyingine kwao ni soko la uhakika kwani kwa sasa wanauza kiroba cha kilo 25 kwa ghrama ya Sh 20,650 bei ambayo haiwapi faida ya kutosha.
Japhet Kasewa ambaye ni mmiliki kiwanda cha kusaga chokaa naye ameongeza ili wafanikiwe zaidi, wanaomba mfumo wa ruzuku iliyositishwa 2016 urejeshwe.
Amesema kwa sasa bado wanatumia miundombinu ya zamani kwa kubeba mawe kutoka kwenye machimbo kwa Sh. 95,000 kwa awamu moja ambayo hugharimu magogo ya Sh. 550,000 kutoka mkoani Iringa.
Akizungumzia changamoto hizo, Afisa Madini anayesimamia eneo hilo, Fransis Gewe ameahidi kuyafikisha mahitaji ya wachimbaji hao kwa afisa madini mkaazi mkoa wa kimadini ili afikishe sehemu husika kufanyiwa kazi.