Waislamu watakiwa kulinda amani, maadili na kufichua wahamiaji haramu

Mbeya/Manyara. Waislamu nchini Tanzania wametakiwa kutumia sikukuu ya Eid Al Adha kumpiga vita shetani katika kupotosha maadili, kudumisha amani kama dini hiyo inavyoelekeza na kufichua wahamiaji haramu.

Akitoa hotuba ya sikukuu ya Eid Al Adha, Kadhi wa Mkoa wa Mbeya, Sheikh Hassan Mbarazi amesema siku ya leo (Jumatatu, Juni 17, 2024) hutumika kumpiga vita shetani katika kupotosha maadili, huku akiwataka wenye uwezo kuwajali maskini na wenye uhitaji.

Amesema katika kusherekea sikukuu hiyo, shetani huwa karibu kupumbaza wanawake na watu wengine, hivyo kuomba kutumia ibada kukabiliana na changamoto hizo.

“Pia tutumie ibada kulinda amani kama inavyoelekeza dini yetu na kuondoa mgongano baina ya mtu na mtu isitutoe katika kufanya yale Mungu anayopenda na ili kufanya hivyo, tusiishie kuswali siku za sikukuu na Ijumaa, badala yake iwe swala tano” amesema kadhi huyo.

Akitoa salamu za Sheikh wa Mkoa wa Mbeya, Ayasi Njalambaha, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), mkoani humo, Sheikh Mussa Ismail amewataka Waislamu kutowakumbatia wahamiaji haramu.

Amesema ili kuhakikisha amani ya mkoa na nchi kwa ujumla inaendelea kuwapo, kila mmoja awe balozi wa kufichua wahamiaji haramu na kuwaomba kutumia fursa ya uchaguzi kujitokeza kujiandikisha na kushiriki uchaguzi.

“Sheikh wa Mkoa (Njalambaha) ameelekeza mambo yafuatayo tusiwapokee wala kuwatunza wahamiaji haramu, bali tuwe mabalozi kuwafichua ili kulinda amani, tutimize wajibu na kupata haki yetu kushiriki uchaguzi,” amesema Sheikh Ismail.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera,  katibu tawala wa wilaya hiyo, Mohamed Aziz ameelekeza watu kufanya kazi, kuwa waadilifu na kuwalea watoto katika maadili, upendo na uaminifu na kwamba kila kitu kina mipaka yake.

Amesema kwa sasa uadilifu na maadili ni changamoto kubwa katika jamii, akilaani baadhi ya viongozi wa dini kufanya vitendo visivyo vya kimaadili kwa watoto.

“Serikali inaelekeza kufanya kazi kwa maendeleo binafsi na Taifa, uislamu unafundisha amani, upendo na uadilifu, lakini inasikitisha huko mikoa ya kusini wiki iliyopita sheikh mmoja ametuhumiwa kulawiti watoto 15, hii si sawa na haipendezi, kwani inabomoa uislamu wetu.

“Hakuna dini inafundisha mambo ya hovyo, tuwalee watoto katika utaratibu ulio sahihi, kuwafundisha maisha yaliyo bora, Serikali inahitaji haki, uadilifu na amani ndio maana unaona mkoa wetu wa Mbeya umetulia kutokana na ushirikiano,” amesema Aziz.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amewaomba wazazi na walezi kuwalea watoto katika misingi ya imani, ili kupata Taifa lililo bora na kuondokana na mmomonyoko wa maadili.

“Vitabu vyote tukufu vimeelekeza kuishi kwenye imani, sasa niwaombe wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao katika kuwalea kwenye misingi ya imani, ili kuwa na Taifa bora,” amesema Kuzaga.

Katika viunga vya Masjid Noor Mji Mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara, Imamu wa msikiti huo, Sheikh Ramia Mohamed amesema sikukuu hiyo inapaswa kusherehekewa kwa amani.

Sheikh Ramia amesema si vyema kusherehekea sikukuu kwa ulevi na kufanya vurugu kinyume na mafundisho ya dini yao.

Hata hivyo, amewaasa wenye uwezo kuwasaidia wenye uhitaji na uwezo wa kuchinja au kununua kitoweo cha sikukuu.

“Sikukuu hii inaendana na kuchinja, hivyo waliojaaliwa uwezo mkubwa wawasaidie waliokosa, ili nao washerehekee kwa furaha na amani sikukuu hii,” amesema sheikh Ramia.

Imamu msaidizi wa msikiti huo, sheikh Mohammed Shauri amesema kisa cha kuchinja kwenye sherehe hiyo ni kutokana na agizo la Mungu kwa Ibrahim alipomtaka amchinje mtoto wake, Ismail ambapo aliridhia.

“Nasi tunapaswa kuchinja ngamia, ng’ombe, mbuzi, kondoo na wanyama wengine halali kwa ajili ya kusherehekewa sikukuu hii,” amesema Shauri.

Related Posts