MASHINDANO ya soka ya Kombe la Zuberi Cup yameanza kuchanganya mjini hapa na kuwa gumzo katika vijiweni na mitaani mbalimbali.
Sio watoto,vijana wala wazee wa mitaa ya mji wa Moshi na viunga vyake ikiwemo Bomambuzi,Kaloleni,karanga, kiboriloni,Longuo,Majengo,Njoro,Pasua mpaka Soweto kote huko gumzo ni moja tu,uhondo wa Zuberi Cup msimu wa 2024.
Mashindano hayo yanayoendelea mjini hapa kwa msimu wa nne tangu kuanzishwa kwake mwaka 2021 yakiratibiwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi ambaye pia ni diwani wa Kata ya Njoro,Zuberi Abdallah Kidumo yamekuwa na msisimko mkubwa mjini hapa.
Zuberi ameufanya mchezo wa soka kupendwa kwani kauli mbiu yake ya Soka ya Maisha ‘Another Level’ inasadifu maisha halisi kama ilivyo kwenye soka Kuna kushinda na kushindwa.Hali kadhalika maisha yanajumuisha mafanikio na changamoto.
Hivyo kupitia mashindano hayo mashabiki huja wakifurika kwa umati mkubwa kusapoti timu zao na kuburudika haijalishi wamepata ama wamekosa riziki katika shughuli zao za kilasiku jambo ambalo limekuwa gumzo zaidi.
Diwani huyo ambaye amehamasisha Moshi iwe na msisimko hasa kila baada ya ligi kuu kutamatika mashabiki wamekuwa wakimiminika nyakati za jioni mamia Kwa mamia kuelekea katika viwanja vinne yanapopigwa mashindano hayo ambavyo ni Njoro, Mandela, Magereza na Majengo kwani huko kote Meya amewekeza kwenye timu shiriki na miundo mbinu mbalimbali.
Klabu 44 zinashiriki msimu huu zikitoka ndani na nje ya Manispaa ya Moshi ambapo Katika mechi ya ufunguzi iliyochezwa juzi jumapili katika uwanja wa Reli uliopo Kata ya Njoro,bingwa mtetezi wa mashindano hayo timu ya Pasua Big Star waliichapa timu ya Wazalendo mabao 4-1.
Mwenyekiti wa mashindano hayo,Japhet Mpande alisema mashindano yatachezwa kwa hatua ya makundi saba yenye timu sita na saba ambapo kila kundi litatoa timu mbili zitakazoenda hatua ya 16 bora isipokuwa kwa makundi yenye timu saba ambayo yatahitaji timu itakayoshika nafasi ya tatu yaani ‘Best Loser’.
Akizungumzia mashindano hayo, Zuberi Kidumo alisema ameanzisha mashindano hayo kukukuza vipaji vya vijana pia kutoa burudani Kwa wanakilimanjaro ndio maana ameweza kumualika Mtangazaji na mchambuzi,Shaffih Dauda kuja kutazama na kuchukua vijana wenye vipaji na vigezo kuwaendeleza zaidi.
“Umeona leo amekuja kiongozi mkubwa wa mashindano ya Ndondo Cup,Shaffih Dauda kutusapoti sisi na kuyaona mashindano yetu ya Zuberi Cup Tournament kwamba namna gani yanaweza kuifikia jamii,lakini pia tumemwomba awe ni daraja la kuchukua vipaji vya vijana wetu na kuwasogeza mbele”
Vilevile alimshukuru mbunge wa jimbo la Moshi Mjini, Priscus Tarimo Kwa kusapoti mashindano hayo Kwa kuahidi kutoa zawadi Kwa mshindi wa kwanza wa michuano hiyo atakayekabidhiwa kitita cha Sh 3 milioni, mshindi wa pili atapata Sh2 milioni na wa tatu atapata Sh1 milioni pamoja na zawadi nyingine nyingi kwa mchezaji mmoja mmoja.
“Tumetengenezewa daraja hili kwaajili ya kuonesha vipaji vyetu mbalimbali kwa wachezaji lakini pia kwa mashabiki na wenyeji pia kupata burudani kama hii jambo hili lisingekuwepo mashabiki wengi wangekuwa mtaani huko wengine wangekuwa hawana shughuli ya kufanya,”alisema Zuber.
Kupitia mashindano hayo Dauda alitoa ombi Kwa serikali na vyama vya mpira nchini kuyatambua rasmi mashindano hayo maarufu kwa jina la ‘Ndondo Cup’ wasiishie tu kuwapa vibali pekee bali waungwe mkono Kwa kutambua jitihada zao kwani shirikisho na vyama vinavyoongoza mpira nchini haviwezi kufika kila mahali.
“Sisi kama wadau wa mpira wa mtaani tunaomba mtutambue rasmi,sio tu tuje kuchukua vibali na kutuacha,mtuunge mkono mtambue jitihada zetu na sisi tupo hapa kuwasapoti nyie,hatupo hapa kuwatengenezea ushindani tupo hapa kusapoti mambo mazuri mnayoyafanya lakini hamuwezi kufika kila sehemu,”
“Kwaupande wa serikali sisi hatujazaliwa kucheza kwenye viwanja vibovu ni kwa sababu ya ukata, kwasababu ya ukosefu wa miundombinu mimi naamini kwa jitihada zinazofanywa na serikali yetu ya awamu ya sita kwa kutoa msamaha wa kodi za majani bandia na baadhi ya vifaa vya michezo kutolipiwa Kodi iwe fursa kwa taasisi za serikali zinazosimamia wananchi”
“Tunacheza huku kwasababu ya ukata lakini tukipata wawezeshaji wa kuja kutuwekea majani bandia kwenye viwanja vyetu vya mtaani watakuwa wametuaaidia sana kuwapa nafasi vijana uwezo wakuonesha uwezo wao.”
Kocha wa timu ya Kilimanjaro Wonders,Ally Juma alisema kuwa mashindano hayo yanawapa nafasi ya kujifua na kukuza vipaji vya vijana wa timu yake ambao mwaka jana kwenye mashindano hayo walishika nafasi ya tatu.
“Mashindano haya ya Zuberi Cup sisi kama kituo cha kukuza vipaji tumeyapokea vizuri na mwaka jana tuliingiza timu moja ya wakubwa pekee na tukakosa nafasi lakini mwaka huu tumeingiza timu mbili wakubwa na vijana na tumejipanga kupambania kituo chetu kwani fursa tumeipata Zuberi Cup”.
Kocha msaidizi wa timu ya Kilimanjaro Plantation FC,Goodluck Barakaeli alisema; “Tulipata msukumo baada ya kupata taarifa kuwa Kuna mashindano mazuri sana kwenye Halmashauri ya mji wa Moshi tukashawishika kushiriki kwasababu timu yetu ni changa na ina vipaji,tunataka vijana wenye vipaji waje wajionyeshe na kama itatokea wakasonga mbele inshallah.”
Kwa upande wa baadhi ya mashabiki wa soka Mkoani hapa,wao walisema kuwa mashindano hayo yana mchango mkubwa katika jamii kwani yamekuwa yakiwezesha vijana kujenga umoja na ushirikiano pia kuonesha vipaji vyao na kupunguza matukio ya uharifu mtaani.
“Mashindano ni mazuri mno,vijana tunafurahia soka hapa Njoro yaani hata uharifu unapungua kwani badala ya kijana kushinda mtaani bila kazi huja hapa kickeki boli linavyotembea na alitoka hapo msongo WA mawazo imeisha” alisema shabiki huyo Frank Mtipe.