KIPA aliyemaliza mkataba wake na Namungo FC, Deogratius Munishi ‘Dida’ amesema miongoni mwa mabao bora ya msimu ulioisha, limo alilofungwa na kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mudathir Yahya.
Dida alilisimulia bao la Mudathir, namna lilivyomshangaza akiipa Yanga pointi tatu, mechi iliyopigwa Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam (Septemba 20, 2023), ambalo hakulitegemea, kwani akili yake alijua mchezo ungemalizika kwa suluhu.
“Yanga ilikuwa imetoka kuzifunga baadhi ya timu mabao matano, jambo ambalo lilifanya tujipange na kila mmoja kufanya kazi yake kwa asilimia 100, tukaangalia wachezaji hatari kwa wapinzani wetu na tulifanikiwa kuwabana.
Aliongeza “Mechi hiyo tulitumia nguvu, kwani Mudathir alifunga dakika za mwishoni, kitu kilichonishangaza kwake ni moyo wake wa kujitoa kwa timu bila kukata tamaa hadi dakika ya mwisho, bila kupindisha maneno lilikuwa bao bora kwa upande wangu, kwani alifanya kazi kubwa na kuonyesha uzalendo kwa timu yake.” Mudathir alifunga hilo, akipokea krosi ya Yao Kouassi na kisha kuifunga, jambo ambalo Dida alisema alitumia akili kubwa ya kufanya maamuzi ya haraka kumtikisa nyavu zake.
Msimu ujao vipi kwa Dida? “Hadi sasa nina ofa ya timu moja, bado muda upo naamini nitapata timu ya kuichezea.”