Geita. Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita leo Juni 18, 2024 inaanza kusikiliza upya kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Ziwa, Alphonce Mawazo, aliyeuawa Novemba 14, 2015 kwa kupigwa na rungu na kukatwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kesi hiyo imeanza kusikilizwa upya baada ya Mahakama ya Rufani iliyoketi Mwanza mbele ya majaji watatu, Ferdinand Wambali, Issa Maige na Leila Mgonya kutengua hukumu ya kesi hiyo na kuamuru ianze kusikilizwa upya, baada ya kubaini kasoro za kisheria katika mwenendo wa kesi hiyo Mahakama Kuu.
Mahakama ya Rufani katika hukumu imesema imebaini mwenendo wa kesi hiyo ulikiuka masharti ya kifungu cha 246(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA).
Desemba 24, 2020 aliyekuwa Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita, Frank Mahimbali, aliyepewa mamlaka ya ziada kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo iliyopaswa kusikilizwa na Jaji wa Mahakama Kuu, aliwahukumu kunyongwa hadi kufa washtakiwa wanne katika kesi hiyo.
Washtakiwa waliohukumiwa adhabu hiyo ni Alfan Apolnari, Epafra Zakaria, Hashim Sharifu na Kalulinda Bwire.
Aliwahukumu adhabu hiyo baada ya kuwatia hatiani Kwa kosa la kuua kwa kukusudia, kama walivyokuwa wakishtakiwa.
Hata hivyo walikata rufaa Mahakama ya Rufani wakipinga kutiwa hatia na adhabu hiyo.
Mahakama ya Rufani katika hukumu iliyotolewa Agosti 30, 2023, ilibaini kuwa kulikuwa na kasoro za kisheria katika hatua za kumpeleka mtuhumiwa mahakamani (committal proceedings).
Katika mfumo wa kisheria, committal proceedings ni hatua za awali ambazo ushahidi wa kutosha dhidi ya mtuhumiwa unakusanywa na kuwasilishwa ili kuamua kama kuna sababu za kutosha za kumfikisha mahakamani kwa ajili ya kesi kamili. Taratibu hizi hufanyika kabla ya kesi kuu kuanza rasmi, na mara nyingi hufanyika katika mahakama za chini au za mwanzo.
Katika hatua hiyo, kwa mujibu wa kifungu 246(2) cha CPA, sura ya 20 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019 inataka idadi ya mashahidi watakaoitwa na Jamhuri watajwe pamoja na vielelezo vya ushahidi vitakavyotumika, visomwe kwa washtakiwa.
Hata hivyo, Mahakama ya Rufani ilibaini katika kesi hiyo baadhi ya mashahidi hawakuorodheshwa na Jamhuri na maelezo ya baadhi ya washtakiwa waliyoyatoa polisi (ambayo yalikuwa miongoni mwa vielelezo vya upande wa mashitaka) hayakusomwa kwenye hatua hiyo lakini mashahidi hao walitoa ushahidi mahakamani.
Kutokana na kasoro hiyo, Mahakama ya Rufani ilibatilisha mwenendo wa kesi hiyo na hukumu yake, ikaamuru kesi ianze upya kuanzia hatua hiyo.
Kesi hiyo imesikilizwa na Jaji wa Mahakama Kuu, Griffin Mwakapeje.
Upande wa Jamhuri umewakilishwa na mawakili wa Serikali, Godfrey Odupoy na Deodatha Dotto, washtakiwa walitetewa na mawakili wa kujitegemea Rukia Marandu, Siwale Siyambi, Constantine Ramadhan na Beatrice Amos.