KAZI imeanza na sasa heshima ya Simba inakwenda kurejea, ndiyo maneno ya mjumbe mpya wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo,Crescentius Magori baada ya kuteuliwa na mwenyekiti wa bodi, Mohammed Dewji ‘Mo’. Hajataka kupoteza muda, ameanza majukumu yake.
Mo Dewji alifanya uteuzi huo juzi Jumapili ambapo aliwachagua wajumbe ambao ni Mohamed Nassor, Salim Abdallah ‘Try Again’, Hussein Kita, Zulfikar Chando, Radhid Shangazi na Magori, watakaoongeza nguvu katika bodi hiyo.
“Siwezi kusema mipango yangu ni mipango ya Bodi ya Simba tukiwa chini ya Mo nafikiri baada ya kutajwa tutakaa pamoja na kuweka mikakati sawa ambayo lengo ni kuirudisha Simba kwenye ubora,” alisema na kuongeza;
“Tumeteuliwa kujenga Simba imara na sio kuendeleza migogoro iliyopo nawaomba wajumbe wenzangu tuungane tujenge umoja ambao utaleta matunda ndani ya timu baada ya kuyumba kwa misimu miwili mfululizo bila kutwaa taji hili ndani ya Simba halijazoeleka,”alisema.
Magori alisema kilichopo sasa ni kukaa pamoja na kuweka mipango yao imara huku akikiri kuwa ni muda sahihi kwao kufanya usajili mzuri ambao utawarudisha kwenye ushindani na kuifanya timu hiyo iendelee kuimbwa kama ilivyokuwa misimu minne nyuma.
Alisema kitu pekee kitakachoirudisha Simba imara na ya ushindani ni kuona viongozi, wanachama na mashabiki wa timu hiyo wanaungana pamoja na kuweka tofauti zao pembeni ili waijenge timu ambayo itawapa furaha na kuwafanya watembee kifua mbele.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba, kimeliambia Mwanaspoti kuwa Magori ni miongoni mwa watu ambao wanasimamia usajili na ameshasaini mastaa wasiopungua watatu kufikia sasa.
“Magori kaanza kazi tayari ndiye aliyetumwa Zambia kumalizana na Joshua Mutale ambaye tayari amesaini mkataba wa kuitumikia Simba msimu ujao akitokea Power Dynamos,” kilisema chanzo hicho.
Magori aliwahi kushika nyadhifa nyeti nchini ikiwemo Mkurugenzi wa uendeshaji wa NSSF, pia amewahi kuiongoza Simba kama Mtendaji Mkuu, Mjumbe wa Kamati ya Usajili, Mjumbe wa Kamati ya Mashindano na ni mmoja wa waanzilishi wa mchakato wa mabadiliko ya mfumo mpya wa uendeshaji ndani ya Simba.
Sambamba na zoezi la kusajili mastaa wapya kuanzia jana jioni Simba ilikuwa ikimalizana na wachezaji inaoachana nao ambapo kuanzia jana mchana ‘Thank You’ zilianza kusambaa kwa fujo wa kwanza akiwa John Bocco.
MO anataka kukamilisha zoezi hilo kwa haraka na kuiweka sawa Simba mpya na ikiwezekana msimu ujao soka lao la Biriani lionekane uwanjani.