Arusha. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe anatarajiwa kuongoza operesheni ya siku 21 ya kukijenga chama kuanzia ngazi ya chini maarufu “Grassroot Fortification (GF) itakayoanza Juni 22, 2024.
Operesheni hiyo inatarajiwa kufanyika katika majimbo 35 yaliyopo mikoa ya Kanda ya Kaskazini ambayo ni Arusha, Manyara, Tanga na Kilimanjaro.
Akizungumza na Mwananchi Digital kwa njia ya simu leo Juni 18, 2024, Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa amesema katika kikao cha mashauriano ya Mkoa wa Manyara kilichofanyika mjini Babati leo, wamejadiliana kuhusu operesheni hiyo.
Amesema operesheni hiyo inayotarajiwa kuanza Juni 22, 2024 katika Jimbo la Karatu, itaongozwa na Mbowe pamoja na Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema.
“Kiukweli kikao chetu cha mashauriano cha leo tulisema ni mazungumzo ya ndani, tulijihifadhi lakini miongoni mwa mambo tuliyojadiliana ni pamoja na kuwa na mkakati wa utekelezaji wa operesheni hiyo itakayoanzia Arusha, kisha Manyara,” amesema Golugwa.
Amesema wataanzia Karatu na watakuwa na mikutano mitano, kisha kuelekea Monduli, Longido (Arusha), majimbo yote ya Mkoa wa Manyara wakianzia Mbulu Vijijini, kisha Mkoa wa Tanga na kumalizia mkoani Kilimanjaro Julai 12, 2024.
“Huu ni mwendelezo wa vikao vya kimkakati kama tulivyofanya Arusha na leo ulikuwa wa ndani pia na tumewaweka viongozi pamoja, kuonyana, kumaliza tofauti zetu na kuweka mikakati ya kutekeleza GF. Kikao cha kesho tutatoa taarifa zaidi kuhusu operesheni hii,” amesema Golugwa.
Juzi, mkoani Arusha, katika hali iliyoonekana kuzima moto unaotajwa kuwaka ndani ya chama hicho, Mbowe alitoka hadharani akisema: “Katika muda huu kidogo tuliobaki nao, silaha ya kwanza ni nguvu na umoja wetu, tukienda vitani tumetawanyika hivi hatuwezi kushinda vita hii.”
Mbowe ametoa kauli hiyo kipindi ambacho kuna fukuto la chini kwa chini linaloendelea ndani ya chama hicho kilichochagizwa na uchaguzi wa ndani unaoendelea na wapo wanaodai mwenyekiti huyo “hapikiki chungu kimoja” na makamu wake, Tundu Lissu.
Awali, akizungumza katika kikao cha mashauriano Mkoa wa Arusha, Lema amesema cheo hicho siyo mbingu bali ni sehemu ya kutumikia wito, hivyo hatakitafuta kwa kufungia watu kwenye magodauni, ndiyo maana amesema hagombei tena nafasi hiyo.
Mbunge huyo wa zamani wa Arusha Mjini amewaonya wanaopanga makundi akisema wawe na amani, wasije wakaharibu chama kwa madai kuwa wanatoa hela kwa ajili ya kumpiga yeye vita.
Amesema kuwa imefika mahali licha ya kuwa mtu ana uwezo wa kuwa kiongozi lakini kwa kuwa hawamtaki au wamegombana naye, hawataki awe kiongozi.
Ametolea mfano miaka mingine ya uchaguzi, akisema kipindi kama hiki, wanakuwa na asilimia kati ya 70 au 80 ya nani anagombea mtaa gani na wajumbe ni kina nani, lakini kwa mwaka huu wamechelewa kwa sababu wako kwenye vita vya uchaguzi.
“Nawaomba sana viongozi mimi ni Mwenyekiti wa Kanda, hiki cheo siyo mbingu, mimi ni platform (jukwaa) ya kutumikia wito, sitakitafuta kwa kufungia watu kwenye magodauni ndiyo maana nilisema sitagombea kanda,” amesema.
Amesema chama hicho kinapoelekea kwenye uchaguzi wa ndani ni uchaguzi makini na muhimu kuliko uchaguzi wa kumtafuta mbunge, diwani au mwenyekiti wa mtaa kwa sababu ndiyo unaamua uchaguzi wa nje wa Serikali.
“Tumefika mahali huyu ana uwezo kabisa kwa sababu hatumtaki kwa sababu huyu alikuwa amekaa na Mungure jana na sisi Mungure hatumtaki au huyu ana uwezo kabisa lakini huwa anakunywa kahawa na Lema na Lema tumeshagombana naye lakini ana uwezo ndiyo hatumtaki,” amebainisha.
Amesema ataomba wapeleke mapendekezo Baraza Kuu la chama hicho ya kuwa uongozi wa kanda au mkoa uweze kufanya uamuzi kwenye kata ya kubadilisha viongozi wanaokuwa wametekeleza majukumu yao chini ya kiwango.
Lema amesisitiza kuwa, Chadema haiwezi kujengwa kuwa taasisi ambayo haina nidhamu na malengo, hivyo ameomba kufanyika kwa mkutano wa maadili kuelekea uchaguzi huo wa ndani.