Mbunge alia akielezea mauaji ya albino

Dodoma. Siku moja baada ya mwili wa mtoto mwenye ualbino, Asimwe Novath (2), kupatikana ukiwa umenyofolewa baadhi ya viungo, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Khadija Taya maarufu Keysha amelia bungeni wakati akiomba mwongozo wa Spika wa Bunge akitaka lijadili usalama wa albino wakati huu wa kuelekea uchaguzi.

Hojan ya Keysha imetokana na kile alichodai kuwa kila unapofika wakati wa uchaguzi watu wenye ualbino hukosa amani kutokana na kukithiri kwa matukio ya kuwadhuru.

Akiomba mwongozo huo leo Juni 18,2024, Keysha amesema Mei 4, 2024 mtoto anayeitwa Julius Kazungu (10) alijeruhiwa na kitu chenye ncha kali kichwani na mikononi  Katoro, Wilaya ya Geita, mkoani Geita.

Amesema Mei 30, 2024, watu wasiofahamika walivamia nyumbani kwa mtoto huyo  aliporwa mikononi mwa mama yake katika Kijiji cha Bulamula, kata ya Kamachumu, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera na Serikali imefanya jitihada kubwa za kumtafuta.

“Mtoto huyu amepatikana Juni 17,2024 ambayo ni jana mtoto akiwa amekatwa viungo hana baadhi ya viungo mheshimiwa Naibu Spika, hapa ninapozungumza watu wenye ualbino hawana amani, hawana raha wanaamini kwamba karibia na uchaguzi maisha yao yanakuwa hatarini.”

“Na sisi wabunge tunaenda katika uchaguzi hivyo mheshimiwa spika kwa maumivu waliyonayo watu wenye ualbino, kwa maumivu ya wazazi hawa ambao watoto wao wamejeruhiwa. Ninaomba Bunge liahirishe shughuli zake na kujadili namna nzuri ya kuwalinda watu wenye ualbino pamoja na watoto,”amesema.

“Tuitake Serikali kuleta sheria kali ambazo zitaweza kuonyesha mfano kwa watu wengine kutokufanya vitendo hivi. Naomba sana kiti chako kikubali na kuridhia lakini kuwaomba wabunge wenzangu waniunge mkono hoja hii,”amesema.

Akijibu mwongozo huo, Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu amemtaka mbunge huyo kwenda kumwelezea Waziri wa Mambo ya Ndani ili aweze kumpatia taarifa vizuri.

“Kaa kwanza mheshimiwa mbunge pole na matatizo yote tunasikitika jambo hili. Kanuni ya 54 ina masharti yake naelekeza aonane na Waziri wa Mambo ya Ndani ili umweleze vizuri na akupe taarifa vizuri,”amesema Zungu.

Kwa mujibu wa jarida la Shirika lisilo la kiserikali linalohusika na utetezi na ustawi wa watu wenye ualbino nchini la Under The Same Sun matukio ya ukatili, ukatwaji au unyofolewaji wa viungo vya mwili au ufukuaji wa makaburi na mauaji ya kinyama dhidi ya watu wenye ualbino yalianza kuripotiwa na vyombo vya habari katika kipindi cha miaka 2006 kwa kuhusishwa na imani za kishirikina.

Juhudi mbalimbali zilianza kuchukuliwa kwa kushirikiana na Serikali ambazo ni pamoja na kuanzishwa kwa kambi za watu wenye ualbino ikiwemo kambi ya Kabanga (Kigoma), Buhangija (Shinyanga), Mitindo (Mwanza), Pongwe (Tanga), Kitengule (Tabora) na Mugeza (Kagera).

Hata hivyo, baadhi ya watu wenye ualbino wakiwemo watoto waliokuwa katika kambi hizo wakati wa matukio hayo walianza kurejea makwao baada ya hali ya usalama kuonekana kuwa imeimarishwa.

Hali ya usalama iliboresha zaidi kwa watu wenye ualbino kati ya mwaka 2015 hadi 2019 ambapo hakukuripotiwa tukio lolote la ukatili ama unyama dhidi yao hadi ilipofika Novemba 2,2022 ambapo Mkazi wa Ngula Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, Joseph Mathias (50) aliuawa kwa kukatwa mapanga kisha wakataji kutokomea na mkono wake.

Kwa mujibu wa Under The Same Sun kwa Tanzania na Afrika Mashariki mtu mmoja kati ya  watu 1, 400 ana ualbino.

Related Posts