Wanamichezo mbalimbali nchini watashiriki mbio za kilomita 2.5 na kilomita 5 zitakazoanzia kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro kuadhimisha miaka 130 ya Olimpiki.
Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) ilianzishwa mwaka 1894 na mwaka huu nchi mwanachama zinaadhimisha miaka 130, ambapo Tanzania katika siku hiyoya Olimpiki Jumapili ijayo itaadhimishwa kwa mbio hizo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya siku tano ya uongozi na utawala katika michezo iliyoanza Juzi mjini Morogoro, Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi amesema wanatarajia mbio hiyo kushirikisha wanamichezo 800.
Amesema, itakuwa ni ‘fun run’ ambayo itashirikisha watu wa umri tofauti, wakilenga kuitumia kuadhimisha miaka 130 ya Olimpiki.
Akizungumzia semia ya uongozi na utawala katika michezo, Bayi amesema imekuwa ikifanyika kila mkoa, lengo likiwa kuwajengea uwezo walimu wa michezo na viongozi wa vyama vya michezo nchini.
“Tumefanya kwenye mikoa karibu yote, mjini Morogoro hii ni mara ya pili yanafanyika na yamekuwa na tija kwa vyama vya michezo ambavyo viko chini ya TOC,” amesema.
Awali, mmoja wa wakufunzi Irene Mwasanga alisema semina hiyo imeshirikisha watu 30 ikiwamo walimu kutoka Manispaa ya Morogoro, Gairo, Mvomero na viongozi wa vyama vya michezo vya soka, soka la wanawake, riadha, kikapu na netiboli wa mkoa huo.
Mgeni rasmi katika semina hiyo na Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Pascal Kihanga aliwataka washiriki kutumia ujuzi watakaoupata kupanua wigo kwa wengine ili mkoa huo uzidi kufanikiwa kimichezo.
“Vipaji vipo vinasubiri kuongozwa na wa kuviongoza ni ninyi, mkitumia semina hii ipasavyo, hakuna shaka mkoa wetu utapanua wigo na kuendelea kufanya vizuri kimichezo,” amesema Kihanga.