Moto waua wagonjwa tisa waliokuwa ICU Iran

Tehran. Wagonjwa tisa wamethibitishwa kufariki dunia leo Jumanne Juni 18,2024 kufuatia moto kuzuka Hospitali ya Ghaem iliyopo mji wa Rasht Kaskazini mwa Iran. Vyombo vya habari vya Serikali vimeripoti.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AFP, moto huo ulizuka kuanzia saa nne usiku wa kuamkia leo na kusababisha maafa hayo. 
Taarifa zinasema moto huo ulifanikiwa kuzimwa huku wachunguzi wakiwa wanafanya kazi kubaini chanzo kilichosababisha kama alivyosema Jaji Mkuu wa jimbo la Gilan, Esmaeil Sadeghi Niarki.

“Kwa bahati mbaya watu tisa walipoteza maisha katika ajali hii ya moto,” amesema Mohammad Ashobi, Rais wa Chuo Kikuu cha Gilan cha Sayansi ya Tiba huko Rasht.

Ameongeza kwamba wagonjwa wengi waliofariki walikuwa wamelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU). Kwa mujibu wa taarifa hizo, hospitali ina vitanda 250 na 142 kati ya hivyo vilishika moto.

Hata hivyo tovuti ya News.AZ International imesema kulingana na moto huo, idadi ya waliokufa huenda ikaongezeka.
Hata hivyo inaelezwa takribani wagonjwa zaidi ya 140 wameokolewa. 

Vilevile Shirika la Habari la Iran International limesema watu 118 wamelazwa hospitalini kufuatia tukio hilo.

Mnamo Novemba mwaka 2023, moto mkubwa uliwahi kutokea na kuteketeza kituo cha kurekebisha tabia ya watu wanaotumia dawa za kulevya katika mji wa Langarud, pia katika mkoa wa Gilan na kuua watu 32.

Aidha, Juni 2020, watu 19 walikufa katika mlipuko mkubwa uliosababishwa na mitungi ya gesi ambayo ilishika moto kwenye zahanati kaskazini mwa Tehran.

Related Posts