Iringa. Hakika maisha ni safari ndefu, ulivyo leo sivyo utakavyokuwa kesho na jambo la muhimu ni kutokata tamaa, huku ukisimamia ndoto zako.
Tangu akiwa na umri wa miaka 20, Daniel Mbwilo aliamini ipo siku atamiliki shule kuanzia chekechea mpaka kidato cha sita na baadaye chuo.
Ndoto hii aliiota wakati akiendelea na kazi yake ya kushona viatu pembezoni mwa kituo cha mabasi cha Mafinga, wilayani Mufindi, Mkoa wa Iringa.
“Kila niliyemwambia jambo hili alicheka, aliona kama natania, lakini moyoni nilinuia hivyo. Niliamini unaweza kufikia ndoto yako usipokubali kukatishwa tamaa na unaweza kuwa yeyote yule haijalishi unaitwa nani sasa, bahati mbaya wengi wanatazama leo, hawaoni kesho,” anasema Mbwilo.
Kwa sasa Mbwilo ni mmiliki wa Shule ya Sekondari ya Adonai iliyopo eneo la Rungemba, Mafinga Mjini.
Kazi yake ya kushona viatu iliyompachika jina la ‘fundi’ ilikuwa njia ya kuelekea kwenye mafanikio yake.
“Kazi ya ufundi wengi wanaichukulia kama kazi ndogo, hata kama unafanya kazi kubwa kama huna malengo huwezi kufika popote. Itafika muda unastaafu huna kitu,” anasema Mbwilo.
Sababu kuwekeza kwenye elimu
Anasema baada ya kumaliza darasa la saba na kufaulu kuanza masomo ya sekondari, hakufanikiwa kuanza masomo baada ya kukosa ada.
Anasema alianza kupambana kutafuta maisha, hivyo akajifunza ufundi viatu.
“Nilijionea huruma kwa kushindwa kusoma sekondari kwa sababu ya kukosa ada na hapo ndio niliapa kuja kuwekeza kwenye elimu. Mimi kuwa darasa la saba hakukufanya nikate tamaa,” anasema Mbwilo.
Miaka ya 1990, Mbwilo alikuwa kijana maarufu katika mji wa Mafinga kutokana na kazi yake ya kushona viatu.
“Uaminifu na bidii kwenye kazi yangu vilisababisha nipate wateja wengi, naweza kusema nilikuwa fundi mzuri wa viatu,” anasema Mbwilo.
Anasema alifanya kazi hiyo kwa miaka minne kabla ya kuanza kuboresha kwa kujifunza kazi nyingine, inayoendana na ufundi wake wa viatu.
“Nilijifunza kushona mikoba ya ngozi na nikaanza kutengeneza viatu vya ngozi. Wateja walikuwa wakija wananunua viatu au mikoba, lakini sikuacha kushona viatu vilivyochanika kwa ajili ya wateja wangu,” anasema Mbwilo.
Anasema baadaye, alijifunza namna ya kushona foronya za ngozi za viti vya magari, baiskeli na pikipiki, kazi ambayo ilimuongezea kipato.
Anasema wakati akiendelea na kazi hiyo, alijifunza kukopa benki na kurejesha fedha kwa wakati, jambo ambalo wapo wanaoogopa.
Mbwilo anasema kiwango chake cha ufundi kiliendelea kuongezeka siku hadi siku, huku akijifunza ufundi mpya kulingana na namna muda ulivyo kuwa ukisogea.
“Fasheni ya sofa ikaingia, nikaamua kujifunza ufundi wa sofa hivyo nikafungua karakana yangu na hapo ndio nilianza kuajiri watu kwa ajili ya kunisaidia,” anasema Mbwilo.
Anasema kadiri alivyokuwa akiboresha ufundi wake, ndivyo kazi yake ya ufundi viatu ilivyoendelea kutoweka.
Anasema kutokana na bidii yake kwenye kazi, alifanikiwa kuwa fundi mahiri wa sofa kwenye mji wa Mafinga kiasi kwamba, alikuwa akipata oda nyingi.
“Biashara ya sofa ilikuwa mtaji wangu, nikaingia kwenye biashara ya vifaaa vya pikipiki.”
Katika kipindi hiki chote Mbwilo alikuwa akiwekeza kwenye ununuzi wa ardhi ambayo aliamini kuna wakati itamsaidia,” anasema.
Anasema kinachowatesa watu wengi ni kushindwa kusimamia malengo yao.
“Nilifanikiwa kununua eka 30 katika eneo la Lungemba ndani ya mji wa Mafinga. Tangu siku ninayonunua niliweka wazi kwamba nitajenga shule yangu nikitimiza ndoto zangu,” anasimulia Mbwilo.
Anasema mwaka 2011 alianza ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Adonai ambayo wengi waliamini asingefikia popote.
“Wengi walijiuliza maswali na wengine wakajipatia majibu. ‘fundi viatu anawezaje kujenga shule? Lazima kuna mtu nyuma yake sio bure’, lakini sikujali,” anasema.
Anasema wakati wote akipambania ndoto yake ya kuwekeza kwenye sekta ya elimu, kazi ya kushona kava za viti vya magari na biashara nyingine zilikuwa zinaendelea.
Mwaka 2013, ujenzi wa shule yake ulikamilika akapata usajili na kuanza kuchukua wanafunzi.
“Sitasahau mwaka ambao wanafunzi wa kidato cha kwanza walikaa darasani wakifundishwa masomo mbalimbali na walimu wao. Niliona namna ilivyo ngumu kufikia ndoto, lakini uvumilivu na kutokata tamaa vilikuwa silaha yangu,” anasema Mbwilo.
Mbwilo anamiliki shule ya sekondari peke yake, huku ndoto ikiwa kumiliki shule ya msingi, sekondari na chuo.
“Ninayo maeneo makubwa ya ardhi, nimepatanda miti ya matunda, miti ya mbao na ninafuga samaki. Maeneo haya naweza kuwekeza kwenye elimu pia. Natamani kufikia ndoto kubwa zaidi ya sasa,” anasema Mbwilo.
Kwa sasa Mbwilo ameajiri zaidi ya wafanyakazi 30 wasomi, wakiendelea na kazi kwenye biashara zake.
“Shuleni peke yake ninao wafanyakazi zaidi ya 10. Ninao walimu wazuri na watoto wanajifunza elimu ya kujitegemea,” anasema Mbwilo na kuongeza:
“Pamoja na masomo ya darasani, wanafunzi wanapata ujuzi wa kujitegemea. Wanajifunza maadili, nidhamu na kazi kama pacha wanaoweza kuleta mafanikio kwenye maisha,” anaeleza.
Baadhi ya walimu wa Shule ya Sekondari Adonai, wanasema uwekezaji kwenye sekta ya elimu hauhitaji msomi wa kiwango cha juu isipokuwa ni dhamira ya mtu.
“Nilihangaika kutafuta kazi serikalini nikakosa, nimehangaika sana, nilipoomba kazi hapa nimepata. Kama Mbwilo asingewekeza, nisingepata nafasi kufundisha shule hii,” anasema Christian Lukas, mmoja wa walimu shuleni hapo.
Mkuu wa shule hiyo, George Mdege anasema safari ya maisha ya Mbwilo ni darasa kubwa kwa wahitimu wengi wa elimu ya juu ambao, baada ya masomo hukata tamaa.
“Inawezekana, lakini pia eneo alilochagua kuwekeza limempa nafasi ya kuwasaidia wanafunzi wengi zaidi,” anasema Mdege.
Mbwilo anasema hatamani kuona wanafunzi wakiacha masomo kwa sababu ya wazazi au walezi wao kukosa uwezo.
“Nimewasaidia watoto wengi na nitaendelea kuwasaidia, sipendi waishie nilipoishia mimi,” anasema.
Anasema moja ya changamoto anayokabiliana nayo ni wale waliomzoea kutoamini kama bidii ndiyo iliyomfikisha hapo.
“Niseme tu watu wasiogope kujifunza kila siku, napata changamoto wengi hawaamini kama bidii peke yake imenifikisha hapa. Ni bidii na maarifa, kwa hiyo vijana wasiogope kuwekeza na kuishi ndoto zao,” anasistiza.
Mchungaji wa Kanisa la Jerusalem, Ephraim Mgeni amesema Mbwilo amekuwa msaada kwenye jamii, hasa kutokana na mchango wa shule hiyo.
“Amekuwa msaada mkubwa siyo tu kwenye eneo la taaluma peke yake, hata kwenye jamii. Ni mshauri na amekuwa akiwasaidia watu, hasa vijana kufikia ndoto zao,” anasema Mgeni.
Baadhi ya wananchi wanaoishi karibu na shule hiyo wanasema yapo maendeleo ambayo uwepo wa Shule ya Sekondari Adonai umechangia.
“Hapa kijijini Rungemba tuna vitu vingi vinaendelea, Mbwilo na shule yake wanao mchango mkubwa,” anasema Harriet Ngailo, mkazi wa Rungemba.
“Mtoto wangu amesoma hapo, kitu nilichokuwa nafurahia ni namna wanavyofundishwa elimu ya maisha na sio kukaririshwa darasani tu. Nimpongeze Mbwilo, angekata tamaa asingefika alipo,” anasema Ngailo.