Dodoma. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imeitaka Serikali kutekeleza mkakati wa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima baada uchambuzi wake kubaini hautekelezwi ipasavyo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Oran Njeza amesema hayo leo Jumanne Juni 18, 2024 alipotoa maoni ya kamati kuhusu tathimini ya hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka 2023, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2023/24, utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2023/24 na mapendelezo ya mpango wa bajeti 2024/25.
Amesema katika kipindi cha miaka mitatu Serikali imekuwa ikibainisha mikakati ya kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.
Njeza ametaja baadhi ya mikakati hiyo ni Serikali kuendesha vikao kwa njia ya mtandao ili kupunguza safari za ndani na nje ya nchi na kupunguza ukubwa wa uwakilishi kwenye mikutano ya ndani na nje.
“Kudhibiti matumizi ya mafuta kwa magari ya Serikali, kupunguza manunuzi yasiyo ya lazima na kupunguza ununuzi wa magari ya Serikali badala yake kuanzisha utaratibu wa kuwakopesha magari watumishi wenye stahili hiyo,” amesema.
Pia, amesema kamati imefanya uchambuzi na kubaini mikakati hiyo imekuwa haitekelezwi ipasavyo.
Ametoa mfano mwaka 2022/23 Sh500 bilioni zilitengwa kwa ajili ya ununuzi wa magari.
Kamati inaitaka Serikali kutekeleza mikakati hiyo kama ilivyojiwekea.
Njeza amesema usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii hufanywa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu kwa mujibu wa Sheria ya Udhibiti na Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Amesema kamati imebaini uwekezaji usio na tija uliofanywa na mifuko na kuwa kwa kipindi cha miaka miwili na miezi tisa kuanzia mwaka wa fedha 2021/22, 2022/23 na kipindi cha miezi tisa kilichoishia Machi 2024, Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), umelipa mafao ya wastaafu yenye thamani ya Sh4.34 trilioni.
Hata hivyo, amesema katika kipindi kama hicho mfuko umepata faida ya Sh1.8 trilioni kutoka uwekezaji kutokana na uwekezaji wake mkubwa uliofanywa kwenye majengo kutokuwa na tija.
Amesema kiasi kilicholipwa na PSSSF hakilingani na faida ya uwekezaji wake.
Pia, amesema kamati imebaini kiwango cha uhimilivu kinachokubalika ni asilimia 60 na lengo la chini la uhimilivu likiwa ni asilimia 40.
Hata hivyo, amesema kiwango cha sasa cha uhimilivu cha mfuko wa PSSSF ni asilimia 36.4.
“Hali hii ina maanisha mfuko hauna uwezo wa kugharimia mahitaji wa wachangiaji. Kamati inaishauri Serikali kuhakikisha mifuko hii inasimamiwa ipasavyo katika kuhakikisha uwekezaji unaofanywa ni wa tija na unaendana na michango,” amesema Njeza.
Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza vihatarishi na kuwezesha mifuko kulipa mafao ya wastaafu kwa wakati.
Njeza amesema kamati inaishauri Serikali kuondoa ruzuku kwa mashirika yanayojiendesha kibiashara na kuwapa malengo ya ufanisi wa utendaji kazi wake na kupewa uhuru wa kujiendesha kibiashara ili yaweze kupimwa kulingana na malengo.
Amesema kamati inapendekeza Serikali ifanye mabadiliko kwenye Sheria ya Msajili wa Hazina Sura ya 370 ili kumpa uwezo wa kisheria Msajili wa Hazina kuwawajibisha watendaji wakuu wa mashirika watakaoshindwa kusimamia mashirika yao kikamilifu.