Dodoma. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amempeleka Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa kosa la kumdharau yeye na Bunge.
Juni 4, 2024 wakati wa mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2024, Mpina alitoa taarifa bungeni kuwa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alitoa taarifa ya uongo kuhusu suala la uagizaji wa sukari kwa kuwa viwanda vya kuzalisha sukari havijashindwa kuagiza bidhaa hiyo kama alivyosema waziri huyo.
Kutokana na taarifa hiyo, Dk Tulia alimpa siku 10 Mpina kupeleka ushahidi wake wa kuwa Bashe alidanganya Bunge kama Kanuni za Bunge zinavyotaka.
Amesema Juni 14, 2024, Mpina alipeleka ushahidi wake kwa Spika kama alivyotakiwa lakini kabla haujashughulikiwa, aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza aliyoyaeleza kuhusu nyaraka hizo.
Amesema baadhi ya vyombo vya habari vimeendelea kurusha mkutano huo na watu mbalimbali wameendelea kuchambua nyaraka zilizowasilishwa kwake na wengine kutoa kabisa hukumu.
“Kitendo cha nyaraka zilizowasilishwa kwa spika na kuziwasilisha katika vyombo vya habari kuhusu maudhui ni kitendo cha utovu wa nidhamu kwa spika na kwa Bunge, kudharau mamlaka ya spika, kuingilia mwenendo wa Bunge na kushusha hadhi na heshima ya Bunge,”amesema Tulia.
Amesema kifungu cha 26 cha Sheria ya Kinga na Madaraka ya Bunge, kinazuia kitendo cha kumkosea heshima spika kwa maneno ama kwa matendo na kinazua vitendo vya dharau kwa mwenendo wa shughuli za Bunge.
Pia amesema kifungu cha 34 cha sheria hiyo kinazuia kuchapisha kwa umma taarifa zilizoandaliwa mahususi kwa ajili ya kuwasilishwa bungeni pasipo kupata kibali cha Bunge na kabla ya taarifa hizo kuwekwa mezani.
Amesema baada ya kutafakari mazingira ya alichokifanya Mpina Juni 14,2024, ni maoni yake kuwa mbunge huyo amemkosea Spika na amelikosea Bunge kwa kupoka fursa ya spika na Bunge.
Tulia amefafanua Mpina pia amepoka fursa ya Bunge na Spika kutumia mamlaka waliyopewa na kanuni za Bunge katika ushahidi alioutoa bila kuendeshwa na mashinikizo kutoka kwa umma ambao unaendelea kujadili ushahidi huo na kutoa hukumu.
Dk Tulia amesema kanuni za bunge zinatoa mamlaka kwa Spika kutoa adhabu kwa mbunge anayetenda makosa ya kinidhamu na kutoa mfano kwa kanuni ya 83 (2 ) ambayo inampa mamlaka ya kumsimamisha mbunge kuhudhuria vikao vya Bunge visivyozidi 10 mfululizo.
Hata hivyo, amesema kwa kuzingatia misingi ya utawala bora ikiwemo haki ya kusikilizwa, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ikutane mara moja kutafakari jambo hilo lililofanywa na Mpina na kutoa maoni na mapendekezo ya nini kifanywe na Bunge.
“Kwa upande uliowasilishwa na Luhaga Mpina kudhibitisha tuhuma zake kwamba Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema uongo bungeni naikabidhi pia Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili kamati iupitie na kutoa maoni iwapo ushahidi huo unathibitisha tuhuma alizozitoa na nini kifanywe na Bunge,”amesema.
Ameagiza kamati hiyo kuanza kushughulikia masuala hayo leo na kuwasilisha taarifa kwake Juni 24, 2024.