Dodoma. Wakati mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina amepelekwa mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa kudharau mamlaka ya Spika na Bunge, ushahidi wa tuhuma alizotoa dhidi ya Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kwamba amesema uongo nao umepelekwa kwa kamati hiyo ili kufanyiwa kazi.
Uamuzi huo umetolewa leo Juni 18, 2024 na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson akisema kitendo cha Mpina kuupeleka ushahidi kwenye vyombo vya habari ni kudharau mamlaka ya Spika, kuingilia mwenendo wa Bunge na kushusha hadhi na heshima ya Bunge.
Spika amepeleka mbele ya kamati hiyo nyaraka za ushahidi wa Mpina dhidi ya Bashe aliyemtuhumu kwamba amelidanganya Bunge kuhusu utoaji wa vibari vya kuingiza sukari nchini.
Licha ya Spika kuwa na mamlaka ya kutoa adhabu kwa mbunge anayetenda makosa ya kinidhamu, amesema ameamua kumpeleka mbunge huyo kwenye kamati ya maadili kwa kuzingatia utawala bora.
“Mathalani kwa mujibu wa kanuni ya 83, fasili ya pili ya kanuni za kudumu za Bunge, Spika anaweza kumsimamisha mbunge kuhudhuria vikao vya Bunge visivyozidi 10 mfululizo,” amesema Spika.
Amesema kwa kutambua na kuzingatia misingi ya utawala bora, ikiwemo haki ya kusikilizwa amelipekeka suala hilo kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
“Kwa upande wa ushahidi uliowasilishwa na Mpina kuthibitisha tuhuma zake kwamba Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema uongo bungeni, naikabidhi pia Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ushahidi wote ili kamati iupitie na kutoa maoni iwapo ushahidi huo unathibitisha tuhuma kwamba amesema uongo bungeni na nini kifanywe na Bunge,” amesema.
Kamati hiyo iliyo chini ya Mwenyekiti Ally Makoa na Makamu Mwenyekiti, Dk Thea Ntara imeanza kazi hiyo Juni 18, 2024.
“Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ianze kuyashughulikia masuala haya mawili leo Juni 18, 2024 na kuwasilisha taarifa kwangu Jumatatu ya Juni 24, 2024. Bunge litashauriwa juu ya maamuzi aliyoyafanya Mpina,” amesema.
Spika amesema Juni 4, 2024, Mpina alitoa taarifa wakati Bashe akichangia kwenye bajeti ya Wizara ya Fedha kwamba anasema uongo, hivyo alimwelekeza ifikapo Juni 14, 2024 awe amewasilisha ushahidi kwake.
“Hata hivyo, kabla sijachukua hatua yoyote kujiridhisha kuhusu ushahidi huo au kuupeleka kwenye kamati ili kamati ichambue ijiridhishe na kuleta taarifa kwangu.”
“Mpina aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza aliyoyaeleza. Kuanzia Juni 14, 2024 baadhi ya vyombo vya habari na mitandao mbalimbali ya kijamii imeendelea kurusha mkutano huo wa Mpina na watu mbalimbali wameendelea kuchambua nyaraka zilizowasilishwa kwangu na Mpina na wengine kutoa kabisa hukumu,” amesema Spika.
Amesema Mpina amekuwa bungeni kuanzia mwaka 2005, hivyo ni mbunge mzoefu na anazifahamu ipasavyo sheria, kanuni na taratibu zinazoliongoza Bunge.
“Ni dhahiri kitendo cha yeye kuwasilisha nyaraka za ushahidi kwa Spika na wakati huohuo kwenda kuzungumza kwenye vyombo vya habari kuhusu maudhui ya nyaraka hizo ni kitendo cha utovu wa nidhamu kwa Bunge na Spika,” amesema.
“Kifungu cha 26 (d) cha Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge, sura 296 kinazuia kitendo cha kumkosea heshima Spika.”
“Kifungu cha 26 (e) kinazuia vitendo vya dharau kwa mwenendo wa shughuli za Bunge, aidha kifungu cha 34, kifungu kidogo cha kwanza (g) kinazuia kuchapisha kwa umma taarifa zilizoandaliwa mahususi kwa ajili ya kuwasilishwa bungeni pasipo kupata kibali cha Bunge na kabla ya taarifa hizo kuwekwa mezani,” amesema.
“Kitendo cha Mpina kinakwenda kinyume cha kifungu cha 29 (d na e) na kifungu cha 34, kifungu kidogo cha kwanza (g) vya sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge sura 296.”
“Baada ya kuyatafakari mazingira ambayo suala hili lilijitokeza na alichokifanya Mpina Juni 14, 2024 ni maoni yangu kuwa Mpina amemkosea Spika na vilevile amelikose Bunge,” amesema na kuongeza:
“Hii ni kwa sababu amepoka fursa ya Spika na Bunge kutumia mamlaka waliyopewa kikanuni kufanyia kazi ushahidi alioutoa bila kuendeshwa na mashinikizo kutoka kwa umma ambao unaendelea kujadili ushahidi huo na kutoa hukumu.”
Spika akitoa taarifa chini ya kanuni ya 39, fasili ya pili ya Kanuni za Kudumu za Bunge, amesema Juni 4, 2024, katika kikao cha 40 cha Mkutano wa 15 wakati wa mjadala wa hoja ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Waziri Bashe alichangia.
Amesema Bashe alichangia kwamba kampuni na viwanda vya sukari nchini vilivyopewa dhamana na Serikali ya kuhakikisha kunakuwa na sukari ya kutosha nchini vimeshindwa kutekeleza wajibu huo na kushindwa kuagiza na kusambaza sukari kutoka nje ya nchi kama inavyotakiwa.
Hali hiyo alisema imesababisha kuendelea kuwepo kwa tatizo la uhaba wa sukari nchini.
Spika amesema Bashe alieleza jambo hilo lilisababisha bei ya sukari kuendelea kupanda hadi kufikia Sh10,000 kwa kilo moja.
Amesema wakati Bashe akiendelea kuzungumza Mpina alipata nafasi ya kutoa taarifa kuhusu mchango huo.
“Taarifa ya Luhaga Mpina ililenga kuonyesha Waziri alikuwa analidanganya Bunge kwa sababu kampuni na viwanda vilivyopewa dhamana ya kuagiza sukari havijashindwa kutimiza wajibu wao, bali upande wa Serikali umekuwa ndiyo kikwazao cha kufanikisha lengo hilo.”
“Serikali imeshindwa kushirikiana vyema na wenye viwanda na kampuni zilizopewa dhamana ya kuagiza sukari, hivyo kusababisha kuadimika kwa sukari, kupanda bei, hivyo kuleta kadhia kwa wananchi,” amesema.
“Mpina aliendelea kusisitiza Waziri amelidanganya Bunge na anao ushahidi unaothibitisha jinsi wizara ilivyochangia kuendelea kwa tatizo la uhaba wa sukari nchini,” amesema.
Amesema baada ya taarifa ya Mpina alitoa ufafanuzi kuhusu masharti ya kanuni ya 70 fasili ya kwanza, ya pili na ya tatu ya Kanuni za Kudumu za Bunge.
“Kanuni inafafaua kuhusu kutosema uongo bungeni, mbunge yeyote anayetoa tuhuma kwamba mbunge mwingine anasema uongo bungeni anatakiwa kuwasilisha ushahidi ili kuthinitisha uongo huo.”
“Hivyo, kwa kutumia kanuni hiyo niliekeza Mpina awasilishe ushahidi ifikapo Juni 14, 2024 ili kuthibitisha tuhuma kwamba Waziri wa Kilimo amelidanganya Bunge,” amesema.
Spika amesema Juni 14, 2024 Ofisi ya Bunge ilipokea barua kutoka kwa Mpina iliyowasilisha nyaraka za ushahidi kama alivyoelekeza.
Juni 30, 2016 mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ alisimamishwa kuhudhuria vikao 10 vya Bunge la 11 kuanzia Juni 30, 2016 kwa kosa la kunyoosha kidole cha kati juu bungeni hatua inayoashiria matusi.
Mbilinyi alitenda kosa hilo alipotoka nje ya ukumbi wa Bunge baada ya kile alichodai kuna mbunge wa CCM aliyemtusi mama yake.
Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea alisimamishwa kushiriki vikao vitano vya Bunge kwa kushindwa kuthibitisha kauli aliyoitoa kuhusu Waziri wa Ujenzi kujengewa nyumba na nyumba za wanajeshi.
Mbunge James Ole Miliya alifungiwa kushiriki vikao vitano kutokana na kushindwa kuthibitisha tuhuma za kumhusisha Jenista Mhagama na kampuni moja ya madini.
Pia, wabunge wawili wa Chadema walisimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa kosa la kusema uongo bungeni. Suzan Lyimo vikao vitano na Anatropia Theonest vikao vitatu.
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee alisimamishwa kuhudhuria mikutano miwili ya Bunge kwa kosa la kulidharirisha Bunge.
Juni 2018 wabunge Halima Mdee wa Kawe, Ester Bulaya wa Bunda Mjini na Conchesta Rwamlaza wa Viti Maalumu walisimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge.
Conchesta Rwamlaza alisimamishwa kutohudhuria vikao vitatu kwa kosa la kusema uongo mbele ya Bunge akimtuhumu mbunge wa Muleba Kusini Profesa Anna Tibaijuka kujimilikisha ardhi yenye ukubwa wa ekari 400 kinyume cha sheria taarifa ambazo hazikuwa kweli.
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ilitoa msamaha kwa mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari kwa kosa alilolifanya Mei 30, 2017 kudharau mamlaka ya Spika ikiwemo kupiga kelele bungeni na kutupa karatasi hovyo.
Nassari alipata msamaha kwa kuwa ilikuwa mara yake ya kwanza kutenda kosa kama hilo kisha kupelekwa mbele ya Kamati.
Mbunge Jesca Kishoa alisimamishwa kuhudhuria vikao viwili vya bunge baada ya kuleta bungeni habari kuhusu mabehewa feki na kushindwa kulithibitishia Bunge.
Wabunge wa CCM waliowahi kupelekwa
Agosti 2021 wabunge Josephat Gwajima (Kawe) na Jerry Silaa (Ukonga) walifikishwa mbele ya Kamati ya Maadili na Madaraka ya Bunge kwa tuhuma kadhaa ikiwemo kusema uongo na kushusha hadhi na heshima ya Bunge.
Pia, Silaa, Gwajima na Humphrey Polepole waliwahi kufikishwa mbele ya Kamati ya Maadili ya wabunge ya CCM na kuhojiwa ikiwa ni kuitikia agizo la Bunge.