Nairobi. Serikali imezindua ujenzi wa majengo pacha ya ghorofa 22 kila moja jijini Nairobi, Kenya, yatakayotumika kama Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini humo na kitega uchumi kwa ajili ya kuongeza fedha za kigeni.
Kwa sasa, Tanzania inatumia Sh29 bilioni kwa mwaka kulipia kodi kwa ajili ya balozi na makazi ya watumishi wake wanaofanya kazi nje ya nchi, na ujenzi huu unaelezwa kuwa ni sehemu ya mkakati mpya wa Serikali kutumia viwanja na majengo yake kujiongezea mapato.
Kwenye uzinduzi huo uliofanyika katika eneo la kibiashara la Upper Hill jijini Nairobi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesema majengo hayo ambayo ujenzi wake utagharamiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF, yataipa Tanzania fursa ya kutumia eneo ililonalo Kenya kujenga ubalozi na kupangisha kwa makazi na ofisi ili kupata fedha.
“Kwa mwaka tunatumia wastani wa Sh29 bilioni kulipa gharama za kupangisha ofisi zetu za kibalozi na nyumba za mabalozi wetu duniani kote. Kupitia mkakati huu mpya ambao unaanzia Kenya, tumepanga kuanza kuingiza zaidi ya Sh36 bilioni kwa mwaka kupitia uwekezaji tutakaofanya kwenye majengo na viwanja vyetu vilivyopo ughaibuni.
Tanzania itajenga majengo hayo kwenye eneo ililopewa bure na serikali ya Kenya kwa ajili ya kujenga ubalozi wake, ikijibu ukarimu wa namna hiyo uliofanywa na Tanzania kwa kuipa Kenya bure eneo ambako imejenga ofisi za ubalozi wake, Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Eneo hilo ambalo Tanzania imepewa kujenga ubalozi wake, ni mojawapo ya maeneo ya kimkakati jijini Nairobi, kukiwa na ofisi nyingi za serikali huku ikiwa inatazamana na ulipo ubalozi wa Uingereza katika taifa hilo.
Akizungumza kwenye tukio hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu), Deo Ndejembi amesema uamuzi wa kujenga majengo hayo ulizingatia upembuzi yakinifu uliofanywa na wataalamu na kuona namna mradi utakavyoingiza mapato kwa serikali.
“NSSF ina Kamati ya Uwekezaji ambayo kwa kushirikiana na Bodi ya Wakurugenzi na wataalamu wetu wa masuala ya uwekezaji waliutazama mradi huu na kuona utakuwa na faida kwa nchi yetu. Kwa sasa, mwelekeo wetu ni kutazama miradi yenye faida na masilahi kwa Taifa,” amesema Ndejembi.
Kwa sasa, ubalozi wa Tanzania nchini Kenya unafanya shughuli zake katika ghorofa ya tisa ya jengo la Re Insurance jijini Nairobi ambapo Serikali inalipa kodi ya pango kwa ubalozi na inalipia pia kodi za pango kwa watumishi wake wanaoishi nchini humo.
Mgeni rasmi katika tukio hilo, Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi amepongeza hatua ya Tanzania kujenga jengo hilo akisema litakuwa mojawapo ya alama za kudumu za uhusiano wa kirafiki baina ya nchi hizo mbili.
“Eneo hili zuri tulilitoa kwa Tanzania kwa kuzingatia uhusiano mzuri na wa kipekee uliopo baina ya nchi zetu hizi mbili. Tulikuwa tu tunajiuliza mbona wenzetu tumewapa eneo na hawataki kuja kujenga. Nimeona ramani na naona litakuwa mojawapo ya majengo mazuri hapa Kenya,” amesema.
Tanzania ina jumla ya viwanja na majengo 101 duniani kote na kwa mujibu wa mkakati mpya uliopitishwa na Wizara ya Mambo ya Nje hivi karibuni, lengo la serikali ni kutaka kuona inatumia mali zake hizo kuiingizia nchi mapato.