HUU ni ushauri ambao mara nyingi hutolewa kwa wapenzi. Tunaambiwa tusiingilie mahusiano ya watu. Tusiwe washauri sana kwenye ndoa ya Mwekazaji Mohammed Dewji ‘Mo’na Simba. Wanapendana, wamedumu miaka mingi, hivyo wanajuana mapungufu yao. Wapambe tushike jembe tukalime.
Chanzo cha vuta nikuvute Simba hivi karibuni, kwa kiasi kikubwa ni mwenendo mbaya wa timu. Kushindwa kutamba ndani na Afrika. Ni msimu wa tatu sasa mfululizo Simba haijashinda taji lolote kubwa, pia imechezea kichapo cha 5-1 kutoka kwa Mtani wao wa Jadi, Yanga. Hali haiwezi kuwa shwari.
Mo anawajua vizuri sana mashabiki wa Simba na mahali pa kuwashika. Mara kwa mara unapotokea mgongano Simba, Mo huwa sehemu salama. Wanasimba wanajua umuhimu wake na mazuri yake.
Ndani ya Simba kunaonekana kuna mgongano mkubwa wa aina ya mabadiliko ya uendeshaji wa klabu yaliyofanya wanachama kuchachamaa, lakini Mo ndio suluhisho.
Yote haya yanakuja baada ya timu kupoteza ubingwa kwa Yanga msimu wa tatu mfululizo na baada ya kufungwa mabao matano na mtani. Mo anajua vyema kuchanga karata zake, anajua namna bora ya kulinda ndoa yake na Simba.
Hajaanza leo wala jana. Mo amekuwepo tangu na tangu. Hii ndiyo siri ya kuingia kichwa kichwa.
Wanachama na watu wa daraja la kati, wapo wanaoona dosari zilizopo kwenye mfumo wa uendeshaji wa Simba na mapungufu ya Katiba yao waliyoipitisha kuruhusu mabadiliko pamoja na mapungufu kwenye muundo wa Bodi ya Wakurugenzi.
Kundi kubwa na hasa la daraja la kati na chini, shida yao ni matokeo tu. Hawa ndiyo wengi kuliko kundi lingine lolote Simba. Hawa kilio cha ni kuona pira biriani linarejea Msimbazi. Hawana habari na mambo ya uwekezaji wala katiba. Wanataka kuona mtani anafungwa na timu inavuka na kwenda hatua ya Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mo akiweka pesa za usajili na kuifunga Al Ahly kila siku kwa Mkapa, wanasahau mambo ya katiba. Simba ikimpiga Mtani kama Mwanaye, hakuna anayekumbuka kama Mo katoa Bilioni 20 ama laa!
Anachokifanya Mo kwa sasa ni kuwapa furaha walio wengi. Naona dalili za kwenda kutengeneza timu bora zimeanza. Anakwenda kuirejesha tena Simba kwenye ufalme wake. Hakuna atayekayeulizia tena uwekezaji na atakayekumbuka mambo ya katiba. Baada ya usajili hutosikia tena kelele za mabadiliko mpaka pale timu itakapoanza kusuasua.
Kuna bahati mbaya moja tu kwenye soka letu. Mawazo ya kutaka klabu zetu ziendeshwe kisasa na kuruhusu wawekezaji, hayakutoka kwa mashabiki na wanachama, ni mawazo ya watu wachache wa daraja. Wazo lenyewe lilikuja wakati timu inafanya vizuri.
Ni ngumu sana kwa mashabiki na wanachama kuhoji mambo mengi. Mashabiki ni watu wa mihemko na matukio. Matajiri wengi wanaitumia njia hiyo kama mtaji. Mo amerejea na bila shaka yotote anakwenda kuisuka Simba upya.
Ili Simba isirudi tena huku kwenye mivutano ya tangu na tangu, pamoja na kutengeneza timu wanapaswa pia kukamilisha mchakato wa uwekezaji haraka. Tatizo la mashabiki na wanachama wakiona wachezaji wapya wa kigeni, akili zinasahau. Wakishaona wamempata mchezaji kutoka kwa Mtani, roho kwatu.
Simba itakuwa bora baada ya mchakato kukamilika na kuacha kutegemea pesa za mtu mmoja. Ni mfumo huu ndiyo humfanya tajiri kila siku kususa! Ni mfumo huu ndiyo humfanya mwekezaji kujiondoa na kujirudisha. Ni muda wa mwekezaji na wanachama kuboresha mfumo wao ili kuijenga Simba imara.
Ugomvi wa Simba na Mo sio wa kuingilia. Wamefanikiwa mengi pamoja. Mashabiki wa soka letu wote ni wale wale.
Yanga kwa sasa ndiyo usiwaguse kabisa. Hakuna hata anayetaka kujua mchakato wa mabadiliko yao umefikia wapi hadi pale mambo yatakapokorogeka. Ikianza kufanya vibaya, utaona matamko kıla mahali. Utaona lawama nyingi zikielekezwa TFF.
Ni muda wa mashabiki na wanachama wa soka letu kubadilika. Kutengeneza misingi ya kudumu ya ye uendeshaji wa klabu zao. Mambo ya kufurahia Ushindi kutokana na pesa za mtu binafsi ni mzuri lakini sio wa kudumu. Huu sio muda wa Yanga kusaidiwa na GSM. Ni muda wa kufanya naye biashara kwa makubaliano ya kudumu.
Muda wa Simba kusaidiwa kila siku na Mo umekwisha. Ni muda wa wao kutengeneza mfumo wa kudumu wa kufanya naye Biashara. Najua kuna ugumu kwenye ndoa ya Simba na Mo lakini huo ndiyo ukweli. Mchakato gani haukamiliki karibu miaka sita?
Tatizo hata viongozi wa upande wa wanachama baadhi yao ni kama tu chawa wa mwekezaji hadi mambo yakorogeke! Mashabiki na wanachama malizeni mchakato wenu wa mabadiliko Simba iwe imara. Kurudi kwa Mo kutawapa timu bora lakini msisahau kumaliza mchakato wa uwekezaji.