Wadau wataja kasoro udhibiti mauaji ya albino

Dar/Kagera. Michakato ya kuelekea uchaguzi imehusishwa kama moja ya sababu za mauaji ya watu wenye ualbino, huku wadau wakitaja kasoro zilizopo katika kuyakabili matukio hayo.

Miongoni mwa kasoro zilizoainishwa na wadau ni uwepo wa shughuli holela za uganga wa jadi na kukosekana mrejesho wa hatua zinazochukuliwa dhidi ya wanaohusika.

Wadau watoa lawama kwa wananchi wakisema baadhi yao wanawajua wanaohusika, lakini wanaendelea kuwaficha kwa hofu ya kusimama mahakamani kutoa ushahidi.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi limesema licha ya hatua kali za kisheria, litaendelea kutoa elimu kwa jamii iondokane na kile lilichokiita kudanganyana kuwa kuna mafanikio katika viungo vya binadamu.

Hayo yanaelezwa kutokana na matukio ya hivi karibuni, likiwemo lililoondoa uhai wa mtoto Asimwe Novath (2) mwenye ualbino, ambaye Mei 30, mwaka huu alinyakuliwa mikononi mwa mama yake.

Tangu aliponyakuliwa alitafutwa bila mafanikio, hadi Juni 17, mwaka huu mwili wake ulipopatikana ukiwa umefungwa kwenye mfuko wa sandarusi, huku baadhi ya viungo vikiwa vimenyofolewa.

Mwili wake umezikwa Juni 18, 2024 nyumbani kwao Muleba mkoani Kagera.

Tukio hilo lilitanguliwa na lililotokea Mei 4, mwaka huu, Katoro mkoani Geita, mtoto Julius Kazungu (10) alinusurika kifo baada ya kujeruhiwa na kitu chenye ncha kali kichwani na mikononi.

Haya si matukio ya kwanza, kumekuwa na historia ya mauaji au kushambuliwa kwa watu wenye ualbino hasa katika kipindi unapokaribia uchaguzi.

Hilo linathibitishwa na ripoti ya mwaka 2013 ya Shirika la Under The Same Sun, iliyoeleza watu 73 wenye ualbino waliuawa kwa kipindi cha miaka sita hasa nyakati za kuelekea uchaguzi.

Akizungumza na Mwananchi Juni 18, 2024, Mratibu wa kitaifa wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF), Anna Kulaya ameainisha maeneo yenye kasoro katika kuvidhibiti vitendo hivyo.

Amesema kwa kuwa waganga wa jadi ndio wanaotajwa kupiga ramli chonganishi, inashindikanaje kuwachunguza kupata undani wa shughuli zao.

Amesema anayetoa vibali vya waganga hao kufanya kazi, anajiridhisha na mambo gani na anafuatilia vipi mwenendo wa kazi za uganga huo.

Kulaya anaeleza kujirudia kwa matukio hayo, kunaashiria mamlaka zinazohusika zimeshindwa kuwalinda watoto na watu wazima wenye ualbino.

Matukio hayo anasema yanahusishwa na michakato ya uchaguzi, akihoji inashindikanaje kujenga utamaduni wa kuchukia mauaji ya wenye ualbino.

“Kwa nini tusitengeneze utamaduni wa kutovumilia vitendo vya mauaji ya albino leo hii pengine visingekuwepo,” amesema.

Kulaya anasema baadhi ya wananchi wana hofu kusimama mahakamani kutoa ushahidi.

“Mtu anajua tukio zima na pengine ameona, lakini anakwambia sitaki ushahidi, siwezi kusimama mahakamani kutoa maelezo, kwa hiyo wahusika wanaachwa,” amesema.

“Mwananchi unakuta anawafahamu wanaohusika, lakini ananyamaza, akiambiwa asimame kutoa ushahidi mahakamani anagoma, hii inatoa nafasi ya wanaohusika kutoa rushwa na matukio yanazimwa,” amesema.

Imani za kishirikina ni sababu inayoaminiwa kuwa chanzo cha mauaji hayo, kama anavyoeleza Mwenyekiti wa Umoja wa Machifu Tanzania, Tonisiza Antonia.

Tonisiza anasema wanaoamini mafanikio katika maisha yao yanatokana na uhai wa aina fulani ya watu, ndio sababu wanajihusisha na vitendo hivyo.

Mitazamo hiyo, anasema inasababisha matukio hayo kujirudia, akieleza pia kuna changamoto ya elimu ya utu.

Licha ya hatua zinazochukuliwa dhidi ya wahusika, amesema zinaonekana za kawaida kwa kuwa wananchi hawapati mrejesho ili kutengeneza funzo kwa wengine.

“Hatua kali zinapaswa zichukuliwe kuwakomesha wanaofanya vitendo hivi. Kuwe na ufuatiliaji na ijulikane anachofanyiwa mkosaji, isiishie kusikia amepelekwa polisi baadaye kimya,” amesema.

Tonisiza amependekeza kufanyika uchunguzi wa kina kubaini wanasiasa wanaojihusisha na imani za kishirikina kama nyenzo ya ushindi katika uchaguzi.

Amesema uchunguzi ufuatiwe na kuwaweka wanasiasa watakaobainika katika kundi lililo karibu kujihusisha na vitendo hivyo, kwa sababu hawaamini katika ushindi halali.

“Mwanasiasa anayeenda kwa mganga kutafuta ushindi maana yake hajiamini yeye na haamini ushindi wake, anatafuta nguvu ya ziada, huyu akiambiwa kafanye kitu fulani ili ushinde hataacha kufanya,” amesema.

Mwenyekiti wa Chama cha Watu wenye Ualbino Tanzania (TAS), Godson Mollel amehoji katika soko lipi viungo vya watu wenye ualbino huuzwa.

“Hivi ulimi wa mwenye ualbino unaenda kuuza wapi au unaupeleka wapi? Mkono wake unaupeleka wapi, soko la viungo vya albino ni lipi,” amehoji.

Maswali hayo amesema ndiyo yanayotengeneza majibu kwamba kuuawa kwa watu wenye ualbino kunasababishwa na imani za kishirikina.

Amesema ni vigumu kutenganisha matukio hayo na uchaguzi.

Amesema inashangaza ni zaidi ya miaka 10 sasa matukio hayo yanaendelea kufanyika, akisisitiza umuhimu wa Serikali kutafuta mbinu ya kuyamaliza.

“Sisi tumechoka, ufike wakati Serikali iseme basi imetosha, inawezekanaje yalipungua leo yanarudi tena,” amehoji.

Kutokana na mauaji ya Asimwe, mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Khadija Taya ‘Keysha’ ameomba mwongozo kwa Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kujadili namna ya kuwalinda wenye ualbino kuelea uchaguzi.

Keysha ametaka Bunge liahirishe shughuli zake nyingine ili lijadili suala hilo.

Mbunge huyo alirejea tukio la Asimwe na lingine lililotokea Mei 4, 2024 Geita la mtoto mwenye ulemavu huo kuchomwa na kitu chenye ncha kali na watu wasiojulikana.

“Tunaitaka Serikali kuleta sheria kali zitakazoonyesha mfano kwa watu wengine kutokufanya vitendo hivi. Naomba sana kiti chako kikubali na kuridhia lakini nawaomba sana wabunge wenzangu, waunge mkono hoja hii,” amesema akibubujikwa machozi.

Rais Samia Suluhu Hassan mwanzo wa hotuba yake katika kongamano la sekta ya habari Juni 18, 2024 amesema kifo cha Asimwe kimemgusa mno.

Kwa taarifa alizonazo, amesema mtoto huyo alikuwa anacheza, akapotea na baadaye mwili wake kupatikana ukiwa umenyofolewa baadhi ya viungo.

Akizungumza na Mwananchi, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime amesema Jeshi hilo kwa kushirikiana na Serikali za Mitaa litaendelea kutambua makundi yanayohitaji ulinzi maalumu, ili kudhibiti matukio hayo kwa wenye ualbino.

Amesema Jeshi litaendelea kutoa elimu kwa kushirikiana na wadau wengine, juu ya jamii kuondokana na mila potofu.

“Tutaendelea kutoa elimu kwa jamii kuondokana na kukumbatia imani potofu kwani huwezi kupata maendeleo kwa kuendekeza na kuabudu ushirikina. Siri ya mafanikio ni kufanya kazi halali,” amesema.

Ameeleza Jeshi litahakikisha wote waliohusika wanakamatwa, akiwasisitiza wananchi kutoa ushirikiano ili kufanikisha hayo.

“Kitendo cha hivi karibuni kilichotokea mkoani Kagera cha kuchukuliwa kwa nguvu kwa mtoto mwenye ualbino na kisha kupatikana akiwa ameuawa ni kitendo cha kulaaniwa na kila Mtanzania anayethamini uhai wake na wa mwingine,” amesema.

“Lakini si kulaani tu bali kuungana na Serikali kuwatafuta wahusika wote waliopanga na kutekeleza uhalifu huo wa aibu na fedheha kwa nchi ambao tulishatoka huko miaka mingi,” amesema.

Misime amesema aina hiyo ya matukio hutokea kwa kuwa baadhi ya wananchi hudanganyana vijiweni kwamba kuna njia za mkato za kupata maendeleo bila kutoka jasho.

“Wanadanganyana kuwa na kiungo cha binadamu mwenzako au kubaka, kulawiti mtoto mdogo utapata mafanikio au utatajirika jambo ambalo siyo kweli,” amesema na kuongeza:

“Kama kungekuwepo na ukweli katika hayo wanayodanganyana basi hao wanaoishi nao wangekuwa matajiri lakini tunachoona wanaishi maisha ya kawaida kama tunayoishi.”

Amesema wote waliofanya mauaji hayo wameishia kukamatwa, kufikishwa mahakamani na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa na wengine kufungwa vifungo vya maisha jela.

Mwili wa Asimwe aliyekutwa amefariki na baadhi ya viungo vya mwili wake kunyofolewa, umezikwa leo Juni 18, 2024 nyumbani kwao Muleba mkoani Kagera.

Judith Richard, mama wa Asimwe amesema kama Serikali imeshindwa kuwalinda watoto wenye ualbino inapaswa iweke wazi.

“Serikali ijitokeze iseme ukweli kama imeshindwa kuwalinda watoto na watu wenye ualbino hapa nchini nimesikitika sana mwanangu aliporwa na leo hii nimeona mabaki ya mwili wake kweli nimezika mabaki tu,” amesema.

Akizungumza wakati wa maziko hayo, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mjini, Erasto Sima amesema taratibu za uchunguzi zinaendelea kuwabaini waliohusika.

“Tayari Rais Samia ameagiza Serikali iendelee kufanya uchunguzi wa tukio hili, naomba kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake,” amesema.

Related Posts