Moshi. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amewasili nyumbani kwa aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, marehemu Tixon Nzunda (56) aliyefariki kwa ajali ya gari pamoja na dereva wake jana mkoani Kilimanjaro.
Nzunda akiwa na dereva wake, Alphonce Edson (54) walifariki jana Juni 18, 2024 kwa ajali ya gari ilitokea saa 8:30 mchana katika eneo la Njia Panda ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) wakati wakienda kumpokea Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango aliyekuwa akielekea mkoani Arusha kikazi.
Makamu huyo wa Rais, amewasili nyumbani hapo eneo la Shanty Town mjini Moshi saa 6:40 mchana akitokea mkoani Arusha
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana usiku na Kamanda wa Polisi Mkoani hapa, Simon Maigwa chanzo ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari aina ya Scania mali ya Orange Gas kushindwa kulimudu gari lake na kwenda kugonga gari la RAS na kusababisha vifo hivyo papo hapo.
Mpaka sasa ratiba ya mazishi ya Tixon hazijatolewa na kwamba inatazamiwa kutolewa muda mfupi ujao na Mkuu wa Mkoa huo, Nurdin Babu.