Donesia Minja: Mkongwe anayekimbiza WPL

UKITAJA wakongwe 10 wanaokiwasha katika Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) basi huwezi kuacha kutaja jina la kiungo mkabaji Donisia Minja ambaye amekuwa bora tangu ligi hiyo ianzishwe mwaka 2017.

Kiungo huyo tangu ajiunge na JKT Queens msimu wa 2017/18 amekuwa chaguo la kwanza la makocha wanaofundisha timu hiyo na kuweka ufalme kwenye eneo hilo.

Mwanaspoti wiki hii lilifanya mahojiano na mchezaji huyo na hapa anajibu siri ya ubora wake unaomfanya awe tishio kwa JKT na timu ya taifa, Twiga Stars.

“Nafikiri sababu kubwa ya kuwa na muendelezo wa kufanya vizuri ni kujitunza na kufuata ushauri wa madaktari lakini kubwa zaidi juhudi zako binafsi.” anasema.

KUKABA HADI KUFUNGA
Kiasili mchezaji huyo anacheza sehemu ya ulinzi lakini mbali na kukaba ni mzuri wa kufumani nyavu.

Msimu uliopita alikuwa moja ya wachezaji walio kwenye vita ya ufungaji bora na alimaliza msimu na mabao 17 akiwa nafasi ya pili nyuma ya straika wa Simba, Jentrix Shikangwa aliyeweka nyavuni mabao 19.

Msimu huu ni kama amemwachia mwenzake Stumai Abdallah kwenye vita ya ufungaji kwani ametoa asisti 10 kwenye mechi 11 na kufunga mabao matano.  

GOLIKIPA TU
Anasema eneo la golikipa ndio nafasi ambayo hawezi kucheza kwa kuwa inahitaji umakini na kujitoa kwa asilimia kubwa tofauti na eneo.

Minja anasema mbali na kiungo mkabaji na mshambuliaji ana uwezo wa kucheza nafasi karibu zote uwanjani kasoro nafasi ya kipa.

“Mimi kocha akiniweka nafasi ya winga, beki wa kati au beki wa pembeni kokote nacheza kutokana na kazi yetu inabidi tu upambane ili angalau siku mmoja wenu akiumia basi nafasi yake uzibe,” alisema Minja.

MSIMU ULIOPITA
Kiungo huyo anasema msimu uliopita ulikuwa na ushindani kwa upande wake kwa kuwa timu tatu za juu zilipishana pointi chache.

“Kwangu msimu uliopita ulikuwa wa aina yake ya ushindani kwanza kila timu ilikuwa inapambana hata ukiangalia bingwa alikuwa anatazamwa kwenye mechi za mwisho, ukipoteza ilikuwa ndio basi tena.” 

PENALTI NA FRII-KIKI
Kwa Simba na Yanga inapotokea wamepata penalti ama frii-kiki chaguo la kwanza ni Aziz KI na Clatous Chama ambao kwa asilimia kubwa wanaaminiwa na timu kwenye kupiga mipira hiyo.

Inapotokea JKT Queens au kwenye kikosi cha timu ya taifa Twiga Stars imepatikana mipira ya kutengwa, wachezaji wote wanamuachia kiungo huyo mpira na hapa anajibu kwanini.

“Kwanza mipira ya penalti au kona na frii-kiki huwa mara nyingi nazifanyia mazoezi na kocha muda mwingi ananielekeza, mbali na hilo nafikiri ni uhodari wa mtu kufanya hivyo ndio maana  naweza hata kufunga mwenyewe au ikamfikia mmoja akafunga.”

KIMATAIFA
Msimu uliopita JKT Queens ilishiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutolewa hatua ya makundi na AS Casablanca ya Morocco kwa mabao 4-1 katika mchezo wa mwisho wa makundi.

Msimu huu ili timu hiyo ishiriki klabu bingwa lazima ichukue ubingwa wa ligi kisha Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

Donisia anasema: “Tunaamini msimu huu utakuwa mzuri kwetu na kwa uwezo wa Mungu tutachukua ubingwa wa ligi na kushiriki mashindano ya CAF ambayo msimu uliopita hatukufanya vizuri sana.” 

Related Posts