Huu hapa umuhimu wa kufanya mazoezi

JUMANNE jioni kulikuwa na mjadala wakuvutia kwenye jukwaa la Jamii forum kuhusu umuhimu wa mazoezi ili kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza.

Chini ya mwamvuli wa Wizara ya Afya, mtu ni Afya, mambo lukuki yalizungumzwa na wataalam wa afya. Mwanaspoti Dokta inaungana na wataalamu hao kwa kutoa ufahamu wa umuhimu wa mazoezi.

Mazoezi ni njia rahisi na inayopendwa katika kukabiliana na magonjwa yanayojulikana kama Non-Communicable diseases (NCDs) au life style diseases.

Kwa mujibu wa chapisho la takwimu la Shirika la Afya duniani-WHO 2024, inakadiriwa magonjwa hayo yalisababisha asilimia 71% ya vifo vyote duniani kwa mwaka, sawa na watu milioni 41.

Kufanya mazoezi mara kwa mara ni moja ya hatua muhimu katika kupata afya bora ya mwili, kwani ni moja ya nyenzo rahisi zenye kuboresha afya zetu pasipo kutumia gharama nyingi.

Kijumla mazoezi yana faida kubwa sana katika afya ya mwili na akili. Ndiyo maaana wahenga wanasema “Afya ni mtaji”.

Kadiri unavyofanya mazoezi mara kwa mara kwa kipindi kirefu na ndivyo pia unavyozidi kuimarisha afya ya mwili hatimaye kuepukana na hatari ya kupata magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.

Ukiacha kundi kubwa la wanamichezo ikiwamo wachezaji wa soka ambao kila mara katika kona hii nawazungumzia upande wa majeraha ya michezo, ufahamu wa leo unahusu watu wote.

Mtakumbuka pia wapo wanamichezo ambao tayari wamestaafu na sasa wanakumbana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwamo magonjwa ya moyo, kisukari na kiharusi.

Umuhimu wa mazoezi unawahusu wao pia kwani ukishaachana na michezo ya kulipwa basi mwili unaweza kupata uzito uliokithiri au unene, hivyo kuwa katika hatari ya kupata magonjwa hayo.

Hapo nitalenga zaidi faida za mazoezi dhidi ya magonjwa ya kuambukiza ambayo ndiyo yamekuwa kinara katika kuchangia ulemavu na vifo vingi vya mapema duniani.

Faida kubwa ya jumla ya mazoezi ambayo ina matokeo makubwa ya katika maisha ya mwanadamu ni kupunguza hatari ya kupata magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.

Kwa mujibu wa shirika la Afya duniani WHO, magonjwa hayo ndio yanaongoza duniani kwa kusababisha vifo vingi vya mapema.

Ufanyaji wa mazoezi unasaidia kuporeka na kudumisha afya ya mfumo wa moyo na mishipa ya damu na upumuaji ambayo ndio mihimili kwa afya ya mwili.

Mazoezi huboresha afya ya Moyo, misuli, kudhibiti uzito wa mwili, kuisaidia mishipa ya damu isiharibiwe na mafuta mabaya, kudhibiti kiwango cha sukari katika damu kinachoweza kukusababishia shambulizi la moyo na kiharusi.

Inaeleweka wapo ambao kutokana na umri si mazoezi yote wanaweza kuyafanya. Ingawa mwili ukipata mazoezi mchanganyiko inaongeza faida zaidi katika utimamu wa mwili.

Wanasayansi wa mazoezi ya mwili wanapendekeza mchanganyiko wa mazoezi ya aina tatu ambayo watafiti wa mazoezi na afya wamebaini kuwa na mchango mkubwa kwa afya bora ya moyo.

Inahitajika kufanya asilimia 60% ya mazoezi mepesi, asilimia 20% mazoezi ya viungo na asilimi 20% mazoezi ya kuimarisha misuli.

Niwatoe hofu tu kuwa hata mazoezi pekee ya kukimbia yanajitosheleza kuweza kukusaidia kuwa na mwili imara wenye afya njema.

Kutokana na mazoezi husaidia kudhibiti uzito wa mwili usiangukie katika unene ambao ndio kihatarishi kikubwa cha kujitokeza magonjwa mbalimbali ya kuambukiza ikiwamo magonjwa ya moyo.

Mazoezi yanawezesha mwili kutumia nishati ya ziada iliyohifadhiwa na mwilini. Nishati hiyo inaendelea kukaa bila kutumika ndipo mwili huyabadili na kuwa mafuta ambayo ndio chanzo cha unene.

Faida kubwa ambayo inapatikana na kuwezesha mwili kutumia sukari ya mwili. Hili lina faida kubwa kwa wale ambao tayari wako katika hatari ya kupata au ambao tayari wamepata magonjwa yasiyoambukiza.

Mfano zoezi la kutembea ni moja ya zoezi linalosaidia sana kushusha kiwango cha sukari kwa wale ambao tayari wana tatizo la kisukari. Sukari inaweza kudhibitiwa kwa mazoezi na vyakula tu.

Ugonjwa wa kisukari cha aina ya pili ni moja ya matatizo ya kiafya ambayo kama ufanyaji wa mazoezi utazingatiwa linaweza kusaidia jamii kujikinga nalo.

Kutokana na mazoezi kuwa ni burudani, husaidia sana kuboresha afya ya akili. Vile vile husaidia kuboresha ufanisi wa tendo la ndoa kwa kuwezesha kuwa na misuli imara.

Mazoezi ya mwili yameainishwa katika makundi mawili makuu mawili, mazoezi mepesi yajulikanayo kama Aerobics Exercises ambayo yakifanyika mwili huendelea kupeleka oksijeni katika misuli.

Aina hii hujulikana pia kama Cardio Exercises na yanapofanyika moyo huendelea kusukuma damu yenye hewa ya oksijeni katika misuli inayofanya kazi.

Aina ya pili ni mazoezi magumu yanayojulikana kama Anaerobics ambayo hayahitaji oksijeni ili misuli kufanya kazi na pale yanapofanyika uvutaji hewa husitishwa.

Tafiti za kitabibu zinaonyesha mazoezi yote yana matokeo chanya kiafya lakini yale mazoezi mepesi ya kawaida ni rahisi zaidi kufanyika na kundi kubwa ka jamii ikiwamo kutembea na kukimbia kasi ya wastani.

Mazoezi mengine ni pamoja na kuogelea, kuruka kamba, kucheza muziki, kuendesha baiskeli na mazoezi ya vituo vya michezo.

Ili mazoezi yaweze kuwa na tija hatimaye kuleta matokeo chanya itahitajika kufanyika kwa muda wa dakika 30 kwa siku katika siku tano za wiki.

Au kwa wale ambao ni watu wazima wanaweza kujikita katika zoezi la kutembea angalau kilomita 2 kwa siku katika siku tano za wiki.

Kwa wale ambao wanakuwa na kazi nyingi, wanaweza kujiwekea malengo kuhakikisha anatembea hatua 10,000 kwa siku katika siku 5 za wiki. Inahitajika kutumia simu janja kuweza kuhesabu hatua hizo.

Related Posts