Jaji Mkuu: Mapendekezo Tume ya Haki Jinai yafanyiwe kazi

Dar es Salaam. Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amewataka viongozi wa taasisi za haki jinai kuwahimiza watendaji wao kuisoma taarifa ya Tume ya Haki Jinai ili kuboresha utendaji kazi wao wa kila siku.

Julai mwaka 2023, Tume ya Haki Jinai iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan iliwasilisha ripoti yake yenye mapendekezo mbalimbali yanayolenga kuhuisha mfumo wa haki jinai nchini.

Miongoni mwa mapendekezo hayo ni matumizi ya amri ya kamatakamata bila kuzingatia matakwa ya sheria, ambapo tume ilitaka sheria kufuatwa.

Pia ilisema kuna taasisi nyingi zenye sura ya kijeshi, ikipendekeza zile zinazotekeleza jukumu la kipolisi kuzingatia misingi ya kazi ya Polisi.

Profesa Juma ameeleza hayo leo Jumatano Juni 19, 2024, akifungua mafunzo ya uhifadhi wa wanyamapori yaliyohusisha maofisa wa Ofisi ya Taifa ya Mwendesha Mashtaka (OTM), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Ofisi ya Upelelezi na Makosa ya Jinai na Kikosi cha Kupambana na Ujangili.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na shirika la Pams Foundation linalojihusisha na ulinzi wa mazingira na usalama wa wanyamapori.

Katika maelezo yake, Jaji Juma amesema, “taarifa ya tume ya haki jinai umegusa maeneo mengi, tuwahimize watumishi tunaowasimamia kusoma taarifa ya Tume ya Haki jinai.

“Tuimiliki taarifa ya tume isibaki kwa viongozi, bali ishuke kwa wananchi ili kuboresha utendaji kazi wa haki jinai na ulinzi wa wanyamapori,” amesema Profesa Juma.

Profesa Juma amsema ni wakati mwafaka kwa taasisi zilizoshiriki mafunzo kujifunza kutoka kwenye taarifa hiyo.

Profesa Juma amesema mafunzo hayo yana faida kubwa kwa ajili ya kuwajengea uwezo watumishi wa sekta ya mahakama na maliasili katika kulinda misitu, wanyama pori na haki za wananchi.

Kaimu mkurugenzi wa idara ya wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Fortunata Msofe amesema mkutano huo unawakutanisha wadau wa uhifadhi na wanufaika wa mafunzo yanayotolewa kwa nyakati tofauti na IJA.

“Mafunzo haya yana manufaa makubwa, tunavyoshirikiana na Jeshi la Polisi, wapelelezi na vyombo vya mahakama, tunaamini haki jinai itatenda haki kwa wananchi na wahalifu wanaohusika na ujangili wa rasilimali za wanyama pori na misitu,” amesema Msofe.

Related Posts