JIWE LA SIKU: Simba mpya, mitihani iko hapa!

SIMBA haijashinda mataji makubwa katika misimu mitatu iliyopita ambayo yote yamekwenda kwa watani wao, Yanga. Jambo hili halikai vizuri kwa mashabiki ambao walizoea kuiona timu yao ikishinda mataji manne mfululizo ya Ligi Kuu Bara kuanzia msimu wa 2017-18, 2018-19, 2019-20 hadi 2020-21.

Wekundu wa Msimbazi walikuwa wanatwaa mataji kibabe sana kwa sababu walikuwa sio tu wanakufunga bali pia walikuwa wanakupigia mpira mwingi sana. Hii ndio Simba ambayo mashabiki wameizoea.

Lakini mtingishiko huu uliopita Msimbazi wa kwenda misimu mitatu bila ya taji la maana, unaifanya Simba kupitia kipindi kigumu ikikabiliwa na vitu vingi huku mashabiki wanatamani kujua nini kitatokea kwa ajili ya msimu ujao.

Baada ya mpasuko wa kiuongozi, ambao umeshuhudiwa wajumbe wa bodi ya klabu upande wa mwekezaji wakijiuzulu, huku wale wa upande wa wanachama wakikomaa kwamba hawatajiuzulu na baadhi wakijitokeza kutema nyongo — Simba inajipanga upya baada ya mwekezaji, Mohammed ‘Mo’ Dewji, kutangaza wajume wapya wa bodi kwa upande wake akiwarejesha ‘watu wa mpira’ waje kuikomboa timu.   

Ujio wa wajumbe hao walioteuliwa na Mo, yaani kina Salum Abdallah Muhene ‘Try Again’, Salum Kitta, Crescentius John Magori, Mohamed Nassor, Zulfikar Chandu na Rashid Shangazi (Mbunge), una kazi kubwa ya kuifanya kuirejesha Simba katika makali yake, huku wakitambua kwamba wapinzani wao Yanga na Azam FC wanaonyesha kila dalili kwamba wanazidi kuimarika.

Hii ni mitihani mitano inayoikabili bodi mpya ambayo inapaswa kufanyiwa kazi haraka ili kuirejesha Simba ile tunayoijua:

KANSA YA UCHAGUZI
Licha ya uchaguzi kufanyika mwaka jana wa kuchagua mwenyekiti na wajumbe wa bodi ya Simba kwa upande wa wanachama, bado Simba ina mpasuko mkubwa unaotokana na matokeo ya uchaguzi huo.

Presha inayoendelea ya baadhi ya wanachama na mashabiki kutomtaka mwenyekiti wa klabu Murtaza Mangungu ni kufukua makaburi juu ya kumkataa kiongozi wao ambaye wengine bado hawakubaliani na ushindi wake.

KUIUNGANISHA BODI
Baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Salim Abdallah Mhene ‘Try Again’, kuna vita ya maneno ilianza kwa baadhi ya wajumbe wa bodi hiyo dhidi ya mwekezaji, hapa hili halitapita kirahisi kwani upande wa mwekezaji naye anaweza kuishi nao kwa kinyongo na hapo lazima kutaanzisha safari mpya ya kutokukubaliana.

Hili lisipomalizwa kwa vikao vya ndani linaweza kuleta presha mpya ya mgawanyiko.

KATIBA, MCHAKATO WA MABADILIKO
Simba bado mchakato wa mabadiliko haujakamilika na hali inavyoonekana kuna shida kubwa zaidi ambazo wengi hawataki kuzisema kwa kuhofia kuondoka kwa MO. Ukimsikiliza mwekezaji anajitambulisha kama Simba ni mali yake aliyoinunua miaka kadhaa iliyopita, lakini ukiwasikiliza wajumbe wanadai hata zile Sh20 bilioni ambazo alionyesha mfano wa hundi kuwa aliziweka benki tayari na kwamba klabu inaendelea kuvuna gawio kutokana katika akaunti iliyowekwa pesa hizo — kwamba kumbe hazijawekwa!

Na pia wengine wanakwenda mbali wakisema kwamba Simba haina thamani ndogo kama hiyo, ambayo ni chini ya bajeti yao wa mwaka mmoja tu (kwa msimu uliopita bajeti ya Simba ilikuwa ni Sh23 bilioni). Hivyo wanahoji inawezekana vipi mtu apewe klabu aimiliki milele kwa kiwango cha pesa ambacho ni chini ya bajeti yao mwaka mmoja tu?

Hao ndio wanaodai Simba bado haijathaminishwa sawasawa. Maswali yanakuja hapa, ni nani aliyesema hisa za Simba asilimia 49 anazotaka kupewa Mo ni sawa na Sh20 bilioni?

Eneo jingine ni nani anatakiwa kuwa na nguvu — mwekezeja mwenye asilimia 49 au wenye mali ambao ni wanachama chini ya kiongozi wao Mangungu wanaomiliki asilimia 51 za hisa.

Hapa ndio wanachama wanaona kuna shida ya kikatiba kwa sababu kwa hali ya sasa, mwenyekiti wao Mangungu anaonekana kana kwamba hana nguvu ya uamuzi na amekuwa akitoa kauli za kuuma na kupuliza juu ya mwekezaji na jinsi ya kuongoza mambo.

Kwa maana hiyo haya yanatakiwa kutibiwa wakati huu na bodi hii ili kuirejesha Simba katika makali yake.

KUIRUDISHA SIMBA KIWANJANI
Kujenga kikosi bora na imara ni mojawapo ya mambo muhimu ya kufanya na bodi hii, ambayo kwanza kabla ya yote inapaswa kutafuta kocha bora wa viwango, ambaye atakabidhiwa jukumu la kuliendesha jahazi la Simba.

Kumekuwa na sajili nyingi ambazo zimekosewa Simba na hivyo kuchangia kuwatoa Wekundu wa Msimbazi katika ushindani.
 
Kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu Bara msimu uliopita, imekuwa ni pigo kubwa kwa Simba kwa sababu msimu ujao haitashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kupitia kwa rais wake Patrice Motsepe likitangaza kwamba linatarajia kuyafuta mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika. Hii haiwezi kuwa habari njema kwa wanasimba.

Bodi hii mpya ina kibarua cha kuirudisha Simba kwenye ubora wake kwa mataji ya ndani.

PATO LA SIMBA
Ukiondoa udhamini wa M-Bet, Pilsner, mkataba wa vifaa kama jezi na ile mikataba midogo midogo kutoka kampuni za mwekezaji, klabu hiyo haina vyanzo vingine zaidi ukiachana na mapato ya uwanjani.

Simba kitu ambacho itakabaliana nacho sasa ni namna gani itashusha bajeti yake kwa mwezi ambayo ilikuwa inazidi kukimbia kwenda mbali, inawezekana Mo anaweza kuja kuweka pesa zake lakini bado sio afya sana endapo itakuja kuendeshwa na mtu mwingine wakati mwekezaji huyo akiwa nje na akiwa na hali kama iliyotokea wakati wa utawala wa Try Again kwamba atoe pesa au asitoe.

Simba inatakiwa kujitanua kwa mfuko wake wa mapato kwa kuwa na wadhamini wengi zaidi kama ambavyo wenzao Yanga wamefanikiwa na sasa wanakimbia wakiwa na kipato ambacho kinaweza kuwaongezea kitu kabla ya fedha za mfadhili.

Hilo linatakiwa kufanywa na bodi ya Simba kwa kuunda mkakati mzuri wa kuingiza kipato zaidi kwa kuweka msingi mizuri ya idara ya masoko na hapa Simba inaweza kumpa jukumu hili Ofisa Mtendaji Mkuu wao wa sasa Imani Kajula ambaye hili ni eneo lake bora kuliko kumweka kwenye utendaji wa juu ambao haonekani kukumudu sana hususan mambo ya kimpira.

Simba lazima pia itengeneze akili ya wanachama wake kupata kadi za wanachama. Wenzao Yanga wanavuna pesa wakati wao hakuna kitu kikubwa kinaingia kwenye mfuko wao kutokana na ada za wanachama.

WASIKIE WADAU
Kocha Sunday Kayuni, ambaye mwaka 1998 aliacha rekodi ya kuipa ubingwa AFC Leopards ya Kenya, ameishauri klabu ya Simba kutengeneza falsafa yake, ili inaposajili wachezaji na makocha wasitoke katika misingi yao.

Kayuni ambaye ni mkufunzi wa kimataifa wa makocha, amesema falsafa ya klabu, inasaidia kutoiyumbisha timu, kwani maskauti wanapokuwa wanasajili wanakuwa wanasimamia kuangalia wachezaji ama makocha wanaoendana na mifumo yao.

“Barani Ulaya, timu nyingi zina falsafa, hivyo zinapotafuta kocha, ama wachezaji hawatoki katika falsafa za klabu, ndio maana naishauri Simba na klabu nyingine za Ligi Kuu Bara kufanya hivyo, hilo litazisaidia kuwa imara wakati wote.

“Pamoja na Simba kukosa ubingwa sioni kama ina wachezaji wabaya, huenda hawakuendana na mifumo ya makocha, mfano wangekuwa na falsafa ya timu, ingekuwa rahisi kwao kuwa imara.”

Kwa upande wa mdau wa soka nchini, Heri Chibakasa ‘Heri Mzozo’ amesema: “Simba inahitaji utulivu katika usajili, pia isiwaweke mbali wadau wanaolijua soka, kubwa zaidi wawe na maskauti wenye jicho la kuona vipaji vikubwa vya soka.”

Mchezaji wa zamani Simba, Dua Said alisema kinachohitajika kwa sasa ni kuangalia wapi pana makosa ili warekebishe kwani kinachohitajika ni uwezo mkubwa wa wachezaji watakaoifanya timu kuendelea kuwa juu.

Anasema: “Hakuna Simba bila kikosi imara, kwa hiyo jambo la msingi sana ni kuangalia ni kwa namna gani wanaweza kuijenga timu na mapato yake bila kusahau viongozi wasimame na kutuliza amani ya mashabiki.

“Wakati tulipokuwa tunacheza kulikuwa na changamoto na haziishagi, lakini hazitakiwi kuzidi hilo ndio jambo ambalo viongozi wanatakiwa kulitendea kazi kwa sasa.”

Related Posts