Kamati ya Uongozi IPU kujadili idadi ya nchi washiriki

Unguja. Kamati ya Uongozi ya Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) imekutana Zanzibar kujadili namna ya kuongeza idadi ya washiriki katika mkutano wa umoja huo upande wa Afrika.

Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuanza kikao cha kamati hiyo Juni 19, 2024 Kizimkazi Zanzibar, Rais wa IPU, Dk Tulia Ackson amesema moja ya mambo inayosumbua Afrika, wanapokutana maspika wa dunia nzima kunapokuwa na maeneo ambayo yana nguvu zaidi kuliko mengine.

“Kwa hiyo tukikutana IPU kuna maeneo ambayo yana nguvu zaidi kwa maana ya idadi ya watu wanaohudhuria, wakati wa kupiga kura kwenye maamuzi fulani inatuletea athari, tunajikuta hoja zetu haziwezi kujadiliwa kwenye mkutano,” amesema.

Dk Tulia ambaye pia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema kikao hicho kinafanyika ikiwa ni maandalizi ya mkutano mkuu wa maspika unaotarajiwa kufanyika Oktoba, 2024.

“Haya ni baadhi ya maeneo ambayo tunakutana kuyajadili na kufanya maamuzi, hivyo tutakubalina na kuyapeleka kwenye mkutano mkuu ili yachukuliwe yafanyiwe marekebisho ndani ya chombo hiki,” amesema.

Jambo lingine litakalojadiliwa katika kikao hicho cha siku mbili, amesema ni sera kuhusu changamoto wanazokumbana nazo wasaidizi wa wabunge hao.

Amesema mkutano wa umoja wa mabunge unakutanisha wabunge zaidi ya 2,000 kwa hiyo wanapokuwa na kundi kubwa kuna mambo mengi yanatokea.

“Wakati mwingine watumishi wanaokuja kuwahudumia wanapata changamoto kutoka kwa wabunge na kupata athari, kwa hiyo tutaangazia sera inayohusu usumbufu wa kijinsia. Sisi kama viongozi tumeona ni jambo la kutilia mkazo ili mtu asije kuona na kupata hofu kufanyiwa jambo ambalo halipendezi,” amesema.

Amesema watajadili maandalizi ya mkutano mkubwa wa maspika wote duniani ambao hufanyika mara moja kwa miaka mitano. Mwaka huu unafanyika Oktoba, Geneva nchini Uswisi.

Dk Tulia ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi watoe mapendekezo ni mambo gani wangetamani kusikia maspika wakijadili.

Kwa mujibu wa Dk Tulia, kuna hoja ya umasikini, bado kuna nchi zipo vizuri lakini zingine zinaendelea na wimbi la umasikini unaosababishwa na vita katika nchi zinazoendelea.

Amesema Bara la Afrika lina changamoto mbalimbali ikiwamo vita katika nchi za Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), Sudani, Afrika Magharibi na kwingineko hivyo wapate nafasi ya kujadiliwa na maspika wa dunia nzima.

Amesema umoja wa mabunge pia wanatamani uwe na nchi zote tofauti na ilivyo sasa zipo 180 kwa hiyo zile za Umoja wa Mataifa wanataka nazo ziingie huko na zile nchi ambazo ni ndogo.

Related Posts