Korea K., Urusi zasaini mkataba wa ushirikiano wa kimkakati – DW – 19.06.2024

Ziara hii ya kwanza ya Putin nchini Korea Kaskazini katika kipindi cha miaka 24 inakuja huku kukiwa na wasiwasi juu ya mpango ambamo nchi hiyo inaipatia Moscow silaha zinazohitajika sana kwa ajili ya vita vyake vya Ukraine, na Urusi kuipa Pyongyang msaada wa kiuchumi na uhamisho wa teknolojia ambao unaweza kuongeza kitisho cha mpango wa silaha za nyuklia na makombora wa Kim.

Haikuwa wazi ni aina gani ya msaada ambao mpango huo, unaoelezewa kama “ushirikiano wa kimkakati wa kina,” utatoa.

Akielezea kuunga mkono kikamilifu hatua za Urusi nchini Ukraine, Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un alisema Moscow inafanya kazi kulinda uhuru, maslahi ya usalama, pamoja na mamlaka ya mipaka yake, na kusisitiza mshikamano na serikali ya Urusi, jeshi na watu wake katika kufanikisha malengo ya operesheni hiyo.

Korea Kaskazini| Pyongyang| Putin akiwa na Kim Jong Un
Rais wa Urusi Vladimir Putin (kushoto) na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un (kulia) wakihudhuria hafla ya makaribisho kwenye Uwanja wa Kim Il Sung mjini Pyongyang Juni 19, 2024.Picha: GAVRIIL GRIGOROV/AFP/Getty Images

“Hivi sasa hali ya ulimwengu inazidi kuwa ngumu na inabadilika haraka. Katika mazingira kama hayo, tutaendelea kuimarisha na kushiriki kwa karibu katika mawasiliano ya kimkakati na Urusi, na tutaendelea kuunga mkono sera zote za Urusi bila masharti,” alisema Kim.

Putin amshukuru Kim kwa uungaji mkono thabiti

“Tunathamini sana uungwaji wako mkono thabiti na wa kudumu kwa sera ya Urusi, likiwemo suala la Ukraine Ninamaanisha katika mapambano yetu dhidi ya sera ya kibeberu, na kibabe iliyowekwa kwa miongo kadhaa na Marekani na satelaiti zake kuhusiana na Shirikisho la Urusi,” alisema Putin akimshukuru Kim.

Soma pia: China na Urusi kuanza “enzi mpya” ya ushirikiano

Viongozi hao wawili pia walibadilishana zawadi wakati wa ziara hiyo, huku Kim akipokea seti ya vikombe vya chai na gari la kifahari aina ya Aurus lililotengenezwa nchini Urusi, kulingana na msaidizi wa Kremlin Yuri Ushakov. Ushakov hakusema ni zawadi gani alizopokea Putin, lakini alidokeza kuwa zilihusiana na picha ya Putin, yakiwemo masanamu.

Kremlin ilisema Jumatatu kuwa mkataba huo utachukua nafasi ya makubaliano ya awali kati ya mataifa hayo na matamko yaliyotiwa saini katika miaka ya 1961, 2000 na 2001.

Korea Kaskazini| Pyongyanga| Ziara ya Putin Korea Kaskazini
Umati wa Wakorea Kaskazini ulijipanga kando mwa barabara kumkaribisha PutinPicha: GAVRIIL GRIGOROV/AFP/Getty Images

Uhusiano wa Moscow na Pyongyang umezusha wasiwasi katika nchi za Magharibi, ambazo zinaamini kuwa Urusi imekuwa ikinunua na kutumia silaha za Korea Kaskazini kufanya mashambulizi yake ya kijeshi nchini Ukraine.

Kim alisema uhusiano wa awali na Urusi umefikia hatua mpya ya juu, na kwamba ziara ya Putin itaimarisha “urafiki wa dhati” wa nchi zao.

Vietnam yamuandalia Putin zulia jekundu

Baada ya Korea Kaskazini, Rais Putin ataelekea nchini Vietnam Jumatano jioni, katika ziara nyingine ambayo imekosolewa vikali na Marekani na washirika wake. Putin anauzuru mji mkuu wa Vietnam kwa mwaliko wa Katibu Mkuu Nguyen Phu Trong.

Soma pia: Ziara ya Xi Vietnam kunatishia usahwishi wa Marekani?

Siku ya Alhamisi, kiongozi huyo wa Urusi atakaribishwa katika Ikulu ya Rais, kabla ya kushiriki mazungumzo ya pande mbili na mkuu wa Chama cha Kikomunisti Trong. Pia atakutana na Waziri Mkuu wa Vietnam Pham Minh Chinh na Wavietnam waliosoma nchini Urusi. Putin pia atahudhuria karamu ya serikali.

Korea Kaskazini yasema Marekani yachochea vita vya Nyuklia

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Urusi na Vietnam zina uhusiano wa karibu wa kihistoria na mizizi ya pamoja ya nadharia za ukomunisti. Maelfu ya makada walisoma katika uliokuwa Umoja wa Kisovieti wakati wa Vita Baridi, akiwemo mkuu wa sasa wa Chama cha Kikomunisti cha Vietnam, Nguyen Phu Trong.

Related Posts