Mahakama yabatilisha kifungo cha miaka 20 jela kwa aliyedaiwa kusafirisha mirungi

Arusha. Mahakama ya Rufani nchini imebatilisha mwenendo wa kesi na kufuta hukumu ya kifungo cha miaka 20 jela aliyohukumiwa Mussa Bakari, aliyetiwa hatiani kwa kosa la kusafirisha kilo 109.17 za mirungi.

Aidha, mahakama hiyo imeamuru kesi hiyo isikilizwe upya na mahakama yenye uwezo baada ya kupata kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) na wakati huohuo mrufani atasalia kizuizini akisubiri kusikilizwa upya.

Uamuzi huo umetolewa baada ya Mahakama ya Rufani kubaini dosari za kisheria katika mwenendo wa kesi hiyo.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kukubaliana na hoja ya Wakili wa Serikali, Fidesta Uisso ambaye kabla ya kusikilizwa kwa rufaa hiyo, liibua suala muhimu kuhusu uhalali wa idhini DPP, iliyotolewa chini ya kifungu cha 26 (1) cha EOCCA.

Wakili huyo aliieleza mahakama kuwa aligundua kibali cha DPP kilichopatikana katika ukurasa wa nne ya rufaa, kina dosari kubwa kwa kutokunukuu kifungu cha 15 (1) (a) cha DCEA ambacho mrufani alishtakiwa kwacho.

Rufaa hiyo inapinga uamuzi wa kesi ya uhujumu uchumi namna 19/2021 iliyotolewa na Jaji Elinaza Luvanda Oktoba 26, 2022 kwenye Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam.

Rufaa hiyo ya jinai namba 532/2022 ilisikilizwa na jopo la majaji watatu – Dk Mary Levira, Abdul-Hakim Amer Issa na Ismail Ijelu.

Mrufani alishtaakiwa kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya kinyume na kifungu cha 15 (1) (a) cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.

Kifungu hicho kilisomwa pamoja na aya ya 23 ya jedwali la kwanza la sheria na vifungu vya 57 (1) na 60 (2) vya Sheria ya Kudhibiti Uhalifu wa Kiuchumi na Kuratibu, Sura ya 200 (EOCCA).

Ilidaiwa kuwa Desemba 13, 2018 katika eneo la Kiromo Magengeni barabara ya Bagamoyo – Dar es Salaam wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani, mrufani alisafirisha dawa hizo, kosa ambalo alilikana.

Hata hivyo, kaada ya kesi kusikilizwa pande zote, Mahakama ilimtia hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miaka 20 jela na baada ya kutokuridhishwa na uamuzi huo alikata rufaa.

Katika hati ya rufaa aliyowasilisha Juni 8, 2023, alikuwa na sababu 11 na katika hati ya nyongeza aliyowasilisha Juni 27, 2023 aliongeza sababu nne za rufaa.

Katika rufaa hiyo mrufani huyo alijitetea mwenyewe huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Fidesta.

Kabla ya kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo, Wakili Uisso aliibua suala la uhalali wa idhini ya DPP iliyotolewa chini ya kifungu cha 26 (1) cha EOCCA haikunukuu kifungu cha 15 (1) (a) cha DCEA ambacho mlalamikaji alishtakiwa kwacho.

Kufuatia dosari hiyo Wakili Uisso aliwasihi majaji wabatilishe mwenendo wa kesi wa mahakama ya mwanzo, kufuta hukumu na kutengua hukumu na kuamuru kusikilizwa upya kwa kesi hiyo.

Katika uamuzi huo wa Juni 13, 2024, majaji hao walieleza kuwa wamepitia kwa kina rekodi ya rufaa na kuzingatia uwasilishaji wa Wakili Uisso, suala ambalo linahitaji uamuzi ni hilo la kibali cha DPP.

“Kwa kuzingatia masharti ya kifungu hiki, hakuna kesi inayohusiana na kosa la kiuchumi inayoweza kuanzishwa chini ya sheria hii isipokuwa kwa idhini ya Mkurugenzi wa Mashtaka.”

Wameeleza kuwa kifungu tajwa kipo wazi kwamba kibali cha DPP kinahitajika kabla ya kuanza kusikilizwa kwa kesi ya mtuhumiwa ambaye anashtakiwa kwa kosa la kiuchumi.

“Mrufani humu alishtakiwa kwa kosa la kiuchumi la kusafirisha dawa za kulevya kinyume na kifungu cha 15 (1) (a) cha DCEA, kama ilivyoonyeshwa hapo juu. Kifungu hiki kinatoa masharti ya kosa ambalo linadaiwa kutendwa na mrufani na hukumu yake.

“Ili ridhaa ya DPP iwe halali, lazima iwe na, miongoni mwa mambo mengine, kifungu kilichokiukwa lazima kionekane kwani mtuhumiwa anashtakiwa na kufunguliwa mashtaka kwa kukiuka kifungu maalumu cha sheria,” ilieleza.

Majaji hao walieleza kwa sababu hiyo hapakuwa na kibali cha kusikilizwa kwa kesi ya mrufani, hivyo mahakama haijasukumwa ipasavyo kutumia mamlaka yake ya kumsikiliza mrufani.

“Ndivyo ilivyokuwa, mwenendo mzima wa mahakama ya awali na hukumu havikuwa chochote bali ni ubatili. Katika hali hii, hatuwezi kubainisha sababu za kukata rufaa kwa kuwa suala lililotolewa na Wakili wa Serikali, limeondoa rufaa hiyo,” wamesema.

“Kwa hiyo, kwa kutumia mamlaka yetu ya marekebisho kwa mujibu wa kifungu cha 4 (2) cha Sheria ya Mamlaka ya Rufani, Sura ya 141, tunabatilisha mwenendo wa mahakama ya awali, kufuta hukumu na kutengua hukumu ya mrufani.

Majaji hao baada ya kuzingatia sababu hiyo waliamuru kesi hiyo kusikilizwa upya kwa mahakama yenye uwezo, baada ya kupata kibali halali kutoka kwa DPP na wakati huohuo mrufani atasalia kizuizini akisubiri kusikilizwa tena.

Related Posts