Geita. Mahakama Kuu Kanda ya Geita imekataa kupokea maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili, Safari Lubingo anayeshtakiwa kwa mauaji ya aliyekuwa mfanyakazi wa Mgodi wa Dhahabu Geita (GGML), Milembe Suleman, ikieleza yalitolewa bila ridhaa ya mshtakiwa.
Mahakama imefikia uamuzi huo baada ya kuendesha kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi kutokana na pingamizi lenye hoja tatu zililowasilishwa na upande wa utetezi.
Upande wa utetezi jana Juni 18, 2024 uliwasilisha pingamizi mahakamani ukidai mshtakiwa alitoa maelezo bila ridhaa yake kwa kuwa alipigwa, maelezo ya onyo yalichukuliwa nje ya muda wa kisheria wa saa nne; na kuwa mshtakiwa hakusaini baadhi ya maelezo ikidaiwa saini inayoonekana ni ya askari aliyeandika maelezo hayo.
Awali, upande wa mashtaka kupitia shahidi wa 12 Sajenti Said, aliieleza Mahakama kuwa yeye ndiye aliyechukua maelezo ya onyo ya mshtakiwa huyo akiwa kwenye hali nzuri kiafya.
Upande wa utetezi ulipinga na kuiomba Mahakama kuwasilisha mashahidi wawili watakaothibitisha hoja hizo.
Upande wa mashtaka ulikuwa na shahidi mmoja aliyedai mshtakiwa alisaini maelezo hayo na kuhusu kupigwa, alidai kumhoji mshtakiwa akiwa kwenye hali nzuri.
Shahidi wa utetezi ambaye ni mshtakiwa wa pili, Safari Lubingo akiongozwa na wakili Laurent Bugoti katika ushahidi jana Juni 18, 2024 alidai alikamatwa Mei 3, 2023 na kufikishwa Kituo cha Polisi Geita alikohusishwa na mauaji ya Milembe (43) ambaye hakuwa akimfahamu.
Amedai akiwa chini ya polisi aliamriwa kuvua nguo zote na kulala chali kisha kupigwa na askari ili akubali tuhuma alizokuwa akipewa.
Baada ya kipigo amedai alipelekwa Kituo cha Polisi Nyarugusu.
Amedai alipigwa kwa siku tatu na Mei 5, 2023 ndipo alipoandika maelezo akidai kutokana na kipigo Mei 9, 2023 alipelekwa Hospitali ya Mkoa wa Geita.
Akitoa ushahidi Juni 19, 2024 shahidi wa pili wa utetezi, Dk Christopher Matola amedai Mei 9, 2023 saa 10.30 jioni mshatakiwa wa pili (Safari Lubingo) akiwa na mgonjwa mwingine ambaye hamkumbuki jina walipelekwa na polisi kwa ajili ya matibabu Hospitali ya Mkoa wa Geita.
Amedai mshtakiwa alilalamika kuwa na maumivu ya mwili na sehemu za nyayo, magoti na kwenye viwiko.
Baada ya kusikiliza maelezo amedai alimpatia dawa za maumivu na kujaza fomu namba tatu ya polisi (PF3).
Dk Matola amedai majeraha ya mgonjwa hayakuwa na damu lakini alikuwa na uvimbe mdogo kwenye nyayo na goti na alidai kupigwa akiwa polisi.
Akitoa hukumu ya kesi hiyo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Kelvin Mhina amesema kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa na mashahidi wawili wa upande wa utetezi, umethibitisha mshtakiwa alipigwa akiwa polisi.
Jaji Mhina ametupilia mbali hoja mbili ambazo ni mshtakiwa kuhojiwa nje ya muda na kusema hakuna mahali shahidi alipoeleza muda mshtakiwa aliokamatwa na kukosa ushahidi unaoonyesha saini iliyotumika si ya mshtakiwa.
Ameeleza pingamizi la mtuhumiwa kupigwa linathibitishwa na PF3 ambayo ina muhuri wa polisi, nembo ya polisi na ushahidi uliotolewa na daktari, saini yake na muhuri wa hospitali unaoonyesha wazi kuwa mshtakiwa alitibiwa.
“Maeneo aliyoeleza mshtakiwa kupigwa ndiyo hayohayo ambayo daktari ameeleza kuwa na majeraha madogo, hivyo ushahidi unaonyesha mshtakiwa alipigwa akiwa polisi,” amesema Jaji Mhina.
Katika hatua nyingine Mahakama imepokea vielelezo viwili vilivyotolewa kwenye kesi ya msingi ambavyo ni ramani ya eneo lilikofichwa jambia lililotumika kwenye mauaji na ramani ya eneo zilikokutwa simu za marehemu.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Dayfath Maunga (30), Safari Lubingo (54), Genja Pastoy, Musa Lubingo (33) na Ceslia Macheni (55), ambao wanakabiliwa na shtaka la mauaji ya Milembe Seleman.
Upande wa Jamhuri unasimamiwa na Wakili wa Serikali, Merito Ukongoji akishirikiana na Scolastica Teffe, huku upande wa utetezi washtakiwa wanatetewa na mawakili Liberatus John (mshtakiwa wa kwanza), Laurent Bugoti (mshtakiwa wa pili), Elizabeth Msechu (mshtakiwa wa tatu), Erick Lutehanga na Yesse Lubanda (mshtakiwa wa tano).