Mahakama yakataa nyaraka kuthibitisha malipo ya Continental, Equity Bank

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara imekataa kupokea nyaraka muhimu iliyokusudiwa kuwa kielelezo cha ushahidi katika kesi ya kibiashara iliyofunguliwa na Kampuni ya Continental Reliable Clearing (T) Limited (CRC) dhidi ya Benki za Equity Tanzania (EBT) na Equity Kenya (EBK).

CRC ilifungua kesi hiyo baada ya Benki ya EBK kupitia wakala wake, EBT kuiandikia barua ikiipa siku 21  kurejesha mkopo wake uliotolewa kwake kwa nyakati tofauti kuanzia mwaka 2013, Dola za Marekani Dola 10.13 milioni (sawa na zaidi ya Sh26 bilioni).

Kesi hii ni miongoni mwa kesi kadhaa zilizofunguliwa na kampuni mbalimbali zikipinga kudaiwa na benki hizo na zile zilizofunguliwa na benki hizo dhidi ya kampuni kadhaa zikizidai kampuni mbalimbali fedha ambazo znadai zilizikopesha mabilioni ya fedha, lakini zimeshindwa au zimepuuza kurejesha mikopo hiyo.

Katika kesi hiyo ya kibiashara namba 16 ya mwaka 2023 inayosikilizwa na Jaji Profesa Agatho Ubena, CRC inadai kuwa ilisharejesha mkopo wote na hivyo haina deni kwa benki hizo.

Jana kampuni hiyo kupitia shahidi wake wa pili, Alexander Gombanila akiongozwa na Wakili wa kampuni hiyo, Frank Mwalongo, iliiomba mahakama hiyo ipokee nyaraka hiyo iliyodaiwa kuwa ni jedwali la malipo ya mkopo wote ambao kampuni hiyo ilipewa na benki hizo.

Hata hivyo mawakili wa benki hizo, Emmanuel Sagali anayeiwakilisha EBT (mdaiwa wa kwanza) na Mpaya Kamala, anayeiwakilisha EBK (mdaiwa wa pili) walipinga nyaraka hiyo kupokewa wakidai kuwa haijakidhi matakwa ya kisheria.

Pingamizi hilo lililoibua mvutano mkali wa hoja za kisheria baina ya mawakili wa benki hizo waliobainisha zile walizoziita kasoro za kisheria za zinazoifanya nyaraka hiyo isistahili kupokewa na Wakili wa CRC, Mwalongo, akipinga hoja za mawakili hao na kuiitetea nyaraka hiyo kuwa inastahili kupokewa.

Hata hivyo, jitihada za wakili Mwalongo kupangua hoja za mawakili wa benki hizo kulinusuru nyaraka hiyo ziligonga ukuta kwani, mahakama baada ya kusilikiza hoja za pande zote, katika uamuzi wake leo Juni 19, 2024 imekataa kuipokea nyaraka hiyo.

Katika uamuzi wake, Jaji Ubena amekubaliana na hoja za pingamizi zilizotolewa na mawakili wa wadaiwa, kuwa nyaraka hiyo ilipaswa kuambatanishwa katika hati ya madai kwa kuwa ni nyaraka ya msingi inayokusudia kuthibitisha taarifa zinazobishaniwa.

“Kwa mtazamo wangu iko kinyume na amri ya 7 Kanuni 14(1) (2)”, amesema Jaji Ubena na kufafanua kuwa kusudi la amri na kanuni hiyo ni kulinda wadaawa wasishtukizwe, (bila kuwa na taarifa kuhusu nyaraka zinazowasilishwa bila kufuatia masharti ya kisheria).

Pia, Jaji Ubena amesema kuwa amri hizo hazipaswi kusomwa kwa kupatanisho na amri ya 13 Kanuni ya 1(1) (2), inayohusu nyaraka za ziada, kama Wakili Mwalongo alivyodai, kwa kuwa kila moja Ina jukumu tofauti amri ya 7 Kanuni ya 14 inahusu nyaraka zinazoambatanishwa na hati ya madai.

Pia Jaji Ubena amesema kuwa nyaraka iliyokusudiwa kutolewa inakusudia kujenga msingi wa kesi hivyo, lakini haijatolewa maelezo katika hati ya madai na kwamba hivyo shahidi hawezi kutoa nyaraka hiyo ipokewe na Mahakama.

Jaji Ubena amesisitiza kuwa wadaawa wanapaswa na wanafungwa na mambo yanayodaiwa katika hati ya madai na kwamba hata Mahakama yenyewe zinafungwa na sharti hilo.

Vilevile Jaji Ubena amesema kuwa nyaraka inayokusudiwa kutolewa si sehemu ya vitabu vya benki, kwa kuwa iliandaliwa na shahidi ambaye si afisa wa benki kinyume cha kifungu cha 78 cha Sheria ya Ushahidi

“Kwa hiyo naendelea kuikataa nyaraka hiyo kwa kuwa haikubaliki. Pingamizi limekubaliwa, imeamuriwa hivyo,” amesema Jaji Ubena.

Awali, jana mahakama ilikataa kuzipokea nyaraka nyingine tatu zilizoombwa na shahidi huo kupokewa na mahakama kuwa vielelezo vya ushahidi wake.

Mahakama ilizikataa nyaraka hizo ambazo zilielezwa kuwa ni taarifa za akaunti tatu tofauti za benki, zilizoandaliwa na shahidi huyo, baada ya kuwekewa pingamizi na mawakili wa benki hizo, kwa sababu zinazofanana na zile zilizotolewa katika jedwali la malipo, ambazo mahakama ilikubaliana nazo.

Jinsi mawakili walivyochuana

Kabla ya mahakama kutoa uamuzi wa kuzikataa nyaraka hizo ikiwemo jedwali hilo, mawakili wa pande zote walichuana vikali kwa hoja za kisheria kuhusiana na pingamizi hilo.

Wakili Sagali alidai kuwa nyaraka hiyo ilipaswa iambatanishwe kwenye hati ya madai wakati hati hiyo ilipowasilishwa mahakamani, lakini haikuambatanishwa katika hati hiyo na kinyume cha masharti ya Amri ya 7, Kanuni ya 14(1) ya Kanuni za Mashauri ya Madai (CPC).

Pia alidai kuwa nyaraka hiyo haikuwa imetajwa katika orodha ya viambatanisho vya hati ya madai kinyume cha amri ya 13 (1), (2) ya CPC, wala haikuelezwa katika hati ya madai.

Vilevile Wakili Sagali amedai kuwa taarifa zozote zinazoingizwa katika vitabu vya benki zinapaswa kuthibitishwa na afisa wa benki au mbia kama Sheria ya Ushahidi inavyoelekeza.

Amedai kwamba shahidi aliyeomba nyaraka hiyo ipokewe hana mamlaka kwa kuwa hana sifa hizo na kwamba pia uhalisia wake unatia mashaka, kwani haina saini, mhuri wala hakuna kiapo cha mdaiwa yeyote kuthibitisha kuwa imetolewa naye.

“Hivyo haiwezi kuaminika katika kuthibitisha marejesho ya mkopo,” amedai wakili Sagali.

Naye wakili Kamala aliunga mkono hoja za wakili Kagali na kuongeza kuwa nyaraka hiyo ilipaswa kuambatanishwa na hati ya madai iliyofanyiwa marekebisho, iliyowasilishwa mahakamani Juni 26, 2023; lakini iliandaliwa Septemba 8, 2023 baada ya kukamilisha ubadilishanaji wa nyaraka za kesi.

Alidai kuwa ni jambo la hatari kutengeneza ushahidi mpya baada ya kukamilika kwa hatua ya ubadilishanaji nyaraka za kesi.

Akijibu hoja hizo, wakili wa CRC, Mwalongo amekiri kuwa kweli nyaraka hiyo haikuambatanishwa katika hati ya madai, lakini akadai kuwa inawasilishwa kama nyaraka za nyongeza chini ya amri ya 13 kanuni ya 1 (1) na (2) ya CPC.

Amedai kuwa amri na kanuni hiyo inaruhusu nyaraka ambazo hazikuwasilishwa mahakamani sambamba na hati ya madai kutolewa siku ya kwanza ya usikilizwaji wa kesi.

“Amri hii inawahusu wadaawa wote (pande zote husika katika kesi) yaani mdai na mdaiwa. Mdai ametumia haki hiyo kuwasilisha nyaraka za nyongeza,” amedai wakili Mwalongo.

Wakili Mwalongo alidai kuwa amri ya 13 kanuni ya 1 (1), (2) inapaswa kusomwa pamoja na kwa upatanisho na amri ya 7 kanuni ya 14 (1).

Vilevile amedai kuwa hati ya madai imeelezea wazi marejesho ya mkopo huo na kwamba jedwali hilo ni orodha ya malipo yote yaliyofanywa na mdai (CRC).

Amedai kuwa nyaraka hiyo ni halisi kwa kuwa mwandaaji amebainishwa, na kwamba nakala halisi imesainiwa, imegongwa mhuri na inaonesha tarehe na kiwango cha malipo.

Hata hivyo mawakili Sagali na Kamala walizipinga baadhi ya hoja za Mwalongo, wakidai kuwa amri ya 13 kanuni ya 1 (1), (2) hazipaswi kusomwa kwa pamoja kwani kila moja ina jukumu tofauti.

Wakili Sagali amebainisha kuwa amri ya 13 inazungumzia nyaraka za nyongeza ambazo zinaweza kusaidia hati ya madai katika ulali wa uwezekano na si nyaraka muhimu kama hiyo.

Amesisitiza kuwa nyaraka hiyo ni nyaraka muhimu kwa kuwa ndio msingi wa kesi ya mdai ilipaswa kuambatanishwa na hati ya madai.

Amehitimisha kuwa taarifa za kuthibitisha kutolewa na kurejeshwa kwa mkopo huo kunapaswa zitolewe kwenye taarifa za kibenki na si kwingineko kokote.

Kwa upande wake wakili Kamala naye alisisitiza kuwa amri ya 13, kanuni 1 (1), (2) na amri ya 7 kila moja ina jukumu tofauti na nyingine na kwamba hakuna inayopuuza nyingine.

Related Posts