Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema watumishi wa Umma wanapaswa kumuenzi aliyekuwa Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro marehemu Tixon Nzunda kwa kuwa waadilifu, wazalendo na kumtanguliza Mungu katika majukumu yao.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizungumza na waombolezaji alipowasili nyumbani kwa aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro Marehemu Tixon Nzunda, Moshi mkoani Kilimanjaro. Amesema marehemu Nzunda alikuwa kiongozi na mtumishi wa umma muadilifu na makini katika nafasi mbalimbali alizowahi kuzitumikia serikalini.
Amesema serikali imeguswa na msiba huo na inaungana na waombolezaji wote katika kipindi hiki kigumu. Aidha amewashukuru wananchi kwa kujitoa na kuwa pamoja na familia tangu ilipofikwa na msiba huo.
Vilevile Makamu wa Rais amewasihi watanzania kuendelea kuishi vema kazini, kuishi vema na marafiki pamoja na majirani. Amewaasa waombolezaji kupokea msiba huo kama ni mipango ya Mungu na kumuombea marehemu apumzike kwa amani.
Halikadhalika Makamu wa Rais ametoa salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu Alphonce Edson aliyekuwa dereva wa Marehemu Tixon Nzunda waliofariki pamoja katika ajali ya gari Wilaya ya Hai mkoani Kilimanajro tarehe 18 Juni 2024.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akimfariji
Bi. Grace Mgombela ambaye ni Mjane wa aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa
Kilimanjaro Marehemu Tixon Nzunda mara baada ya kuwasili nyumbani kwa familia
hiyo Moshi mkoani Kilimanjaro tarehe 19 Juni 2024.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza
na waombolezaji mbalimbali mara baada ya kuwasili nyumbani kwa aliyekuwa Katibu
Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro Marehemu Tixon Nzunda Moshi mkoani Kilimanjaro
tarehe 19 Juni 2024.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisali
pamoja na familia ya aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro Marehemu
Tixon Nzunda mara baada ya kuwasili nyumbani kwa familia hiyo Moshi mkoani
Kilimanjaro tarehe 19 Juni 2024.