Moshi. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amewataka wanachama wa chama hicho Mkoa wa Kilimanjaro kumuenzi mwanasiasa mkongwe mkoani humo, Philemon Ndesamburo kwa kuyaenzi mema aliyoyafanya ndani ya chama hicho.
Amesema Ndesamburo alifanya kazi kubwa ya kimageuzi mkoani humo na maeneo mengine “na kwa heshima ya Mzee Ndesamburo lazima chama hiki tukilinde kwa wivu mkubwa kama kumuenzi baba yetu ambaye alijitoa sana kwa muda mrefu.”
Mbowe amesema hayo leo Jumatano, Juni 19, 2024 katika kikao cha mashauriano kilichofanyikia Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro. Ni mwendelezo wa vikoa hivyo anavyovifanya mikoa ya kaskazini.
Ndesamburo, alikuwa Mbunge wa Moshi Mjini (Chadema) kwa miaka 15 kuanzia (2000-2015) na alichochea mageuzi ya upinzania ndani na nje ya mkoa huo. Alifariki dunia Machi 31, 2027 katika Hospitali ya KCMC, alipokuwa akipatiwa matibabu.
Katia kikao hicho, Mbowe amewataka viongozi na wanachama wa chama hicho, kuendeleza umoja na mshikamano ulioasisiwa na Mzee Ndesamburo enzi za uhai wake.
Amemtaja Ndesamburo kama mwanamageuzi kwa Mkoa wa Kilimanjaro na kwamba alijitoa kwa muda mrefu hivyo katika kumuenzi lazima wakilinde chama hicho kwa wivu mkubwa.
“Pamoja na mapungufu yote ambayo tutaelezana hapa, inawezekana tusiwe wepesi sana kutekeleza mipango ya mikakati mingi, lakini ukweli ni kwamba mageuzi ni nia ya watu wa Mkoa wa Kilimanjaro na tukizungumza nia ya mageuzi tunamzungumzia mzee Ndesamburo,” amesema.
“Hatutazungumza mageuzi Mkoa wa Kilimanjaro bila kumtaja Ndesamburo, kama Mzee Ndesamburo angefufuka leo auone Mkoa wa Kilimanjaro kwamba chama hiki kimelegealegea lakini bado hakijafa, angefurahi sana,” amesema Mbowe.
Chadema malengo yetu ni kukamata dola ya nchi hii tukabadilishe mifumo ya utawala wa nchi, tutengeneze na tutumie vizuri rasilimali za Taifa hili, tukarejeshe furaha kwa Watanzania, tukalete maendeleo kwa watu wote, tutengeneze Taifa la watu wenye haki, tusiendelee kuwa kama Taifa la watu misukule.”
Awali, akizungumzia kuhusu uchaguzi ujao ndani ya chama hicho, Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa amesema chama hicho hakitawafumbia macho wale wote ambao watajihusisha na masuala ya rushwa kwa kuwa chama hicho kimekuwa ni kinara wa kukemea matendo hayo.
“Na mimi kama mtendaji mkuu wa chama Kanda ya Kaskazini tunakemea rushwa na matendo hayo, hatuwezi kuyakubali ama kwa fununu au kitendo chenyewe cha rushwa kufanyika, kwa hiyo tumekemea na pale ambapo tendo la rushwa tukilidhibitisha hatupaswi kulifumbia macho,” amesema.
Amani amesema:”Hivyo tunakemea rushwa katika chama chetu na tunakataza kabisa na adhabu kubwa kabisa ni kufungiwa kugombea nafasi yoyote ndani ya chama, iwe ubunge, urais, udiwani mpaka serikali za mitaa unafungiwa.
“Kwa sababu rushwa ni adui wa haki, na sisi kama chama kinachohubiri haki hatuwezi kuruhusu, tunakemea matendo ya rushwa ndani ya chama hiki, tunakemea rushwa kwenye chaguzi zetu za Kanda ya Kaskazini,” amesema Golugwa.
Pamoja na mambo mengine amesema chama hicho kitafanya operesheni kubwa ambayo itaongozwa na Mbowe pamoja na mwenyekiti wa kanda anayemaliza muda wake, Godbless Lema kwa kutumia helikopita na kufanya mikutano 105 kwenye mikoa ya Arusha, Manyara, Tanga na Kilimanjaro kuanzia Juni 22, mwaka huu.
“Ni operesheni kubwa sana ambayo tunataka kuwaonyesha Watanzania na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwamba tuna watu, alafu tuna Mungu na nguvu, kwa hiyo operesheni hii itafanyika kwa njia ya chopa, tutafanya mikutano minne hadi sita kwenye jimbo moja.”
Kwa upande wake, Lema amesema hajarudi kuwa mbunge na kwamba kuitwa mbunge wa Arusha Mjini kwake ni sehemu ya utumishi ambao ni wito.
“Ndugu zangu mimi kwa zaidi ya miaka 22 iliyopita, kazi ninayofanya ni biashara, harakati, siasa na sifanyi kazi hii kwa sababu natafuta kazi nyingine, sijarudi kuja kuwa mbunge, kwangu ubunge ni jukwaa la utumishi wa umma, utumishi wa wito ambao ninao,” amesema Lema.