Paroko msaidizi, baba mzazi washikiliwa tuhuma za mauaji ya Asimwe

Dar es Salaam. Watu tisa akiwemo Paroko Msaidizi wa Parokia ya Bugandika wilayani Misenyi Mkoa wa Kagera, wamekamatwa kwa tuhuma za mauaji ya mtoto mwenye ualbino, Asimwe Novath (2).

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa leo Juni 19, 2024, pamoja na paroko huyo msaidizi, kati ya watu waliokamatwa yumo, baba mzazi wa Asimwe, Novart Venant aliyekamatwa tangu Mei 31, 2024.

Asimwe alinyakuliwa mikononi mwa mama yake mzazi nyumbani kwao Kitongoji cha Mbale, Kijiji cha Bulamula wilayani Muleba Mei 30, 2024 na baadaye Juni 17, mwaka huu mwili wake ulipatikana huku baadhi ya viungo vikiwa vimenyofolewa.

Mwili wa Asimwe ulizikwa nyumbani kwao jana Juni 18.

Saa chache baada ya maziko hayo, Mwananchi Digital iliripoti kuhusu kukamatwa kwa wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo wakiwa na vidhibiti, ikimnukuu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni.

Taarifa ya kukamatwa kwa watu hao, imetolewa leo, Jumatano Juni 19, 2024 na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime.

Kupitia taarifa hiyo, Misime amesema watuhumiwa hao wamekamatwa wakiwa na viungo vinavyodhaniwa ni vya Asimwe, walivyovihifadhi katika vifungashio vya plastiki wakitafuta mteja.

Ameeleza watuhumiwa hao wamekamatwa katika kipindi cha kuanzia Mei 31 msako ulipoanza hadi usiku wa kuamkia Juni 19, mwaka huu.

Amewataja wengine waliokamatwa kuwa ni Desideli Evarist ambaye ni mganga wa jadi mkazi wa Nyakahama, Dastan Kaiza mkazi wa Bushagara, Faswiru Athuman mkazi wa Nyakahama na Gozibert Alkadi mkazi wa Nyakahama, Kamachumu.

Kadhalika, wamo Rwenyagira Burkadi mkazi wa Nyakahama, Ramadhani Selestine mkazi wa Kamachumu na Nurduni Hamada mkazi wa Kamachumu na Elipidius Rwegoshora Paroko Msaidizi wa Parokia ya Bugandika.

“Elipidius Rwegoshora Paroko Msaidizi wa Parokia ya Bugandika ndiye anayedaiwa kumfuata na kumshawishi baba mzazi wa mtoto ili wafanye biashara ya viungo vya binadamu.

“Pia anatuhumiwa kuwa ndiye aliyemtafuta mganga wa jadi na kulipia gharama zote za uganga,” inaeleza taarifa hiyo.

Kupitia taarifa hiyo, Misime amesema watuhumiwa waliokamatwa walieleza jinsi walivyoshiriki katika tukio hilo kwa kushirikiana na baba mzazi wa mtoto.

“Jeshi la Polisi linatoa onyo kali kwa watu wanaoendekeza imani za kishirikina ikiwemo kupiga ramli chonganishi, wakiaminishana kwamba wanaweza kupata utajiri kwa njia za kishirikina, waache tabia hizo,” amesema.

Pia limewataka wananchi waache kudanganyana kwamba kuna utajiri unaopatikana kwa kumiliki viungo vya binadamu mwenye ualbino kwa kuwa si kweli.

“Kama ingekuwa hivyo, familia zenye watoto au ndugu wenye ualbino wangekuwa na utajiri mkubwa lakini badala yake tunaona wakiishi maisha ya kawaida kama sisi wengine,” amesema.

Imeeleza vitendo hivyo ni uhalifu uliopitiliza na ni ushamba katika karne ya maendeleo ya sayansi na teknolojia.

“Yeyote anayefanya na anayeshiriki katika uhalifu wa aina hiyo lazima atakamatwa kwa sababu vitendo hivyo havina baraka za mwenyezi Mungu wala sheria za nchi,” amesema.

Amesema vitendo hivyo ni aibu kwa anayefanya, kwa familia yake, pia vinalifedhehesha Taifa.

Misime amesema watu wenye mawazo hayo wanapaswa kuachana nayo badala yake wafanye kazi halali, watoke jasho na ndiyo siri ya kufanikiwa katika maisha.

Related Posts