MABOSI wa Simba wameshtuka baada ya kubaini ukuta wa Yeriko unataka kubomolewa na Waarabu kwa kugoma Fondoh Che Malone kuondoka klabu baada ya Future Fc ya Misri kumtaka beki huyo wa kati kutoka Cameroon.
Inaelezwa kuwa Malone aliyekuwa akiunda ukuta wa Simba sambamba Henock Inonga, hana furaha Msimbazi na anatakiwa na Wamisri, lakini mabosi wa Simba wameamua kuchomoa ofa zote ikiwamo ya Waarabu hao.
Malone aliyejiunga na Simba Julai 9, 2023 akitokea Cotonsport ya Cameroon, inaelezwa hana furaha ndani ya timu hiyo, japo viongozi hawataki kumpoteza baada ya kuwa na hatihati ya kumbakisha Henock Inonga anayeripoti-wa kujiandaa kutua FAR Rabat ya Morocco.
SIMBA Queens imeweka mzigo mzito kuwapata viungo wawili wa Yanga Princess, Precious Christopher na Saiki Atinuke ambao mikataba yao iko ukingoni. Inaelezwa Simba imeweka kiasi cha Sh 10 milioni kama pesa ya usajili kwa wote wawili na mshahara wa Sh 700,000 kwa mwezi.
TIMU iliyopanda Ligi Kuu kwa msimu ujao, Pamba Jiji imeanza mazungumzo na Kipa wa Alliance inayoshiriki Ligi daraja la kwanza, Amos Tibaskana. Kipa huyo anamaliza mkataba na Alliance na mazungumzo yamefikia pazuri kama mambo yatakwenda vizuri anaweza kujiunga nao kwa ajili ya msimu ujao.