VIGOGO wapya waliopewa jukumu la kuisuka Simba mpya wameanza kishindo cha anga kwa anga. Zambia na Ivory Coast zimekuwa nchi za kwanza kukumbana na mziki huo.
Mwanaspoti linajua hivi karibuni kwamba Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Mohammed Dewji aliwateua kimyakimya, Cresentius Magori, Mulamu Ng’ambi na Kassim Dewji kushika jukumu la kusimamia usajili wa Mnyama na wameshaanza cheche zao.
Huko Ivory Coastam Beki wa kati ASEC Mimosas, Anthony Tra Bi Tra amekiri kwamba Simba iliongea na meneja wake lakini yeye anamalizia msimu kwa mechi ya FA, ndipo atakapofahamu hatima yake kuhusu msimu ujao.
Alieleza kuwa mpaka sasa mjadala mkubwa ni dau la usajili ambalo anataka lakini Simba bado haijaafiki moja kwa moja. “Mambo mawili pekee ndio yanakwamisha dili hili la kwanza; bado nina mechi za FA hivyo nimeamua kufikiria kwanza kibarua kilichopo mbele yangu na timu kwa ujumla,”
“Jambo la pili ni dau ambalo Simba bado halijalifikia mpaka sasa ndio maana nimemuachia meneja wangu aendelee na maongezi hayo, kwani wao wakikubaliana mimi sina shida,” alisema Tra bi.
“Simba ni timu kubwa na ningependa kujiunga nayo lakini sitalazimisha sana kwa kuwa wapo wote kwenye Shirikisho msimu ujao, ingawa ninatamani kupata changamoto mpya,” alisema Tra bi.
Iko hivi mlinzi huyo kitasa wa Asec Mimosas, Anthony Tra Bi Tra Raia wa Ivory Coast mwenye umri wa miaka (25), kama dili hilo litakamilika basi atakuwa mrithi wa Mkongo Henock Inonga anaedaiwa kuondoka msimu huu.
Kule Zambia, bosi wa Simba Magori ameshaimsainisha winga kiberenge Joshua Mutale kutoka Power Dynamos ya huko lakini akawaita chemba mabeki wawili wa kati akianza na Kelvin Kapumbu kisha baadaye Tandi Mwape.
Zesco ya Zambia, ilikuwa inamtaka Mwape mali ya TP Mazembe ili akaungane na Kapumbu, kutengeneza ukuta imara kwa ajili ya msimu ujao itakaposhiriki mashindano sawa na Simba ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Zesco inacholia ni kwamba mabeki hao wawili wamekuwa wasumbufu ghafla kuendelea na mazungumzo wote wakitajwa kutiwa kiburi na Simba kupitia mazungumzo na Magori.
“Kapumbu amekuwa hataki kupokea simu, tunataka kumuongezea mkataba, huku pia Tandi (Mwape) naye tulikuwa tunakwenda naye vizuri lakini amekuwa hajibu tena simu zetu na wote wawili walionekana na kiongozi wa Simba alipokuja hapa,” alisema bosi wa juu wa Zesco ambao ni Mabingwa wa zamani wa Soka nchini humo.