Dodoma. Baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wameitaka Serikali kuondoa ongezeko la Sh382 kwenye bei ya gesi inayotumika kwenye magari badala yake iongeze vituo vya utoaji wa gesi na kuweka ruzuku kwenye vifaa vya matumizi ya gesi.
Wamesema hayo wakichangia makadirio ya bajaeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ambapo Serikali imeliomba Bunge kuidhinisha kiasi cha Sh49.35 trilioni.
Ongezeko hilo lilitangazwa wiki iliyopita na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha bajeti ya Serikali ya mwaka 2024/2025, akisema hatua hiyo imefikiwa ili kuleta usawa kwa kuwa magari yanayotumia mafuta tayari yanachangia mapato kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu ya barabara.
Kutokana na ongezeko kilo moja ya gesi asilia itauzwa Sh1, 932 kutoka Sh1, 550 ya awali.
Akichangia mjadala huo leo Juni 19, 2024, Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku maarufu kwa jina la Musukuma, amesema ongezeko hilo litadumaza lengo la kutaka kuwe na matumizi makubwa ya gesi.
“Tulitembelea viwanda vya kuweka mfumo wa gesi kwenye magari, kwanza gharama za kutengeneza mfumo wa gesi kwenye gari inakaribia Sh2 milioni, vituo vyenyewe kwa kuweka gesi ni viwili pekee.
“Kituo cha Ubungo pale Urafiki, mtu anaenda saa nane usuku anapata huduma saa saba mchana. Tukiwa kwenye kubembeleza watu waingie kwenye matumizi ya gesi, unaongeza tena ushuru.
“Mimi nilidhani Serikali itaweka ruzuku kupunguza bei, lakini inaongeza kodi kukusanya bilioni tisa kwenye magari 3,000, hatuna chanzo kingine?” amehoji.
Tozo hiyo pia imepingwa na Grace Tendega, mbunge wa Viti Maalumu, akiitaka Serikali iweke ruzuku kwenye vifaa vya matumizi ya gesi kwenye magari.
Naye Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage amesema Sh382 iliyowekwa kwa kilo moja ya gesi iondolewe ili watu wengi waingie kwenye matumizi ya gesi na nchi iwe salama pale linapotokea tatizo la mafuta.
“Tumekosea na mheshimiwa Waziri Mwigulu unisikilize kwa nini unaweka ongezeko la pesa kwenye gesi, kwa nini gesi na watu wengi hawataki kuzungumza, sisi gesi kwetu ni kinga, ni usalama kwamba endapo kuna tatizo kwenye ugavi sisi nchi tutabaki salama.
“Dawa ni kuwahimiza Watanzania watumie gesi nyingi tuwape kichocheo, moja tuwe salama kwa vyombo vya usafiri, pili itakapotokea tatizo tutakuwa hatuna tatizo lakini mnatafuta pesa, mbona mnaziacha zinapita?” amesema Mwijage.
Kabla ya suala la gesi asilia, Musukuma ameitaka Serikali kusimama idete kuhakikisha haizui taharuki kwa wananchi katika suala la sukari.
Amesema mwaka 2019 mawaziri wawili wa kilimo na biashara walilazimika kutumia bunduki za SMG kutoa sukari kwenye maghala ya wafanyabishara.
Serikali katika mwaka huu wa fedha ambapo imekusudia kufanya marekebisho ya sheria ili kuwezesha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), kununua na kuhifadhi pengo la sukari kwenye hifadhi ya chakula ya Taifa.
Akizungumzia kusudio la marekebisho hayo, Musukuma ambaye pia ni mfanyabiashara wa sukari, amesema upungufu wa sukari umekuwa ukisumbua nchi na kugeuka hoja ndani ya Bunge kila mwaka.
“Suala la sukari ni kubwa na limekuwa na kelele nyingi sana karibia kila mwaka. Nakumbuka mwaka 2019 wakati Waziri wa Kilimo akiwa Tizeba (Charles Tizeba) na Waziri wa Biashara alikuwa Mwijage, walitoa sukari kwenye maghala kwa kutumia ma-SMG.
“Nishauri sana tunapoona kama suala hili linawakera wananchi ni vizuri tukabadilisha sheria ili haya masuala yakae vizuri, watu wakaacha kuwa kwenye taharuki,” amesema.
Amesema kuhusu suala la njama za kupanga bei, yeye anaishi Mwanza mjini na kwamba kipindi kilichopita cha uhaba wa sukari, Mwanza ilikuwa inauzwa kwa mtu mmoja.
“Ni kweli baadhi ya viwanda wanasema wana mawakala, lakini ni mawakala ‘bosheni’, hawana sukari. Ukienda Kanda ya Ziwa, mimi nakaa Mwanza Mjini, katikati ya mji, watu walianza kwenda kupanga foleni saa 9 usiku na huyo wakala mkubwa alikuwa na sukari imejaa kwenye maghala.
“Tunaona anashusha na meli kutoka Kagera, lakini ili uuziwe sukari hata mifuko 50 inabidi ununue na toilet paper (karatasi ya chooni) au biskuti.
“Sasa nchi ya wastaraabu hatuwezi kuwa na aina hii ya biashara, kwa hiyo ni vizuri zibadilishwe sheria,” amesema.
Amesema Watanzania wamechoka kuona inapofika miezi ya Januari, Februari na Machi wanaanza kupiga kelele za uhaba wa sukari.
“Haiwezekani ukienda Zambia mpakani sukari inauzwa rahisi, ukienda Mtukula inauzwa rahisi. Na mimi nataka kusema kweli, mimi natoka Jimbo la Geita Vijijini, wananchi wangu wa Izibacholi walinunua sukari Sh11, , acha kusema Sh10, 000 na ushahidi ninao, sasa hatuwezi kuwa na nchi ya aina hii,” amesema.
Musukuma amesema mabadiliko hayo ya sheria yatakayoiwezesha NFRA kuziba pengo la upungufu wa sukari itasaidia kuleta nafuu ya maisha ya Watanzania na kwamba si sawa kung’ang’ania sheria ambayo watu wanakandamizwa.
Katika mchango wake, Mbunge Magomeni (Zanzibar), Mwanahamisi Kassim Said, ameeleza kushangazwa na baadhi ya wabunge kupeleka hoja zao kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, badala kuzisema bungeni au ndani ya vyama vyao vya siasa.
“Mimi nashangaa sana kumkuta mbunge anaacha kuzungumza meneno bungeni au kwenye chama chake, anakwenda kuzungumza kwenye mitandao au kwenye vyombo vya habari.
“Tusilichukulie jambo hili kwa urahisi, hawa ndio wanaoturejesha nyuma kimaendeleo, hawa ndio wanaorejesha nyuma Chama cha Mapinduzi,” amesema.
Pia, amezungumzia tatizo la abiria wa mabasi ya mikoani kuzuiwa kupanda mabasi kwenye yadi zao kama zile za Shekilango na kutakiwa waende Mbezi kilipo kituo cha mabasi ya mikoani.
“Toka juzi imekuwa watu wanazuia kuingia na kutoka mjini kwenda Mbezi (Magufuli Terminal) ni Sh30, 000 hadi Sh50, 000 kwa teksi. Wananchi wanapata taabu, tusijitizame sisi tuwatizame na wananchi.
“Leo utasikia DC (Mkuu wa Wilaya) ndio kazuia, DC hana uwezo wa kuzuia mabasi yasipakie Shekilango kwa sababu hana sheria, sasa iseme ile sheria na wamepelekwa kule wakasimamie wananchi na kumsaidia Rais.”