Dar es Salaam. Wakati deni la Serikali likiendelea kuongezeka, wasomi na mchambuzi wa uchumi wamehoji matumizi ya mikopo inayochukuliwa na Serikali, huku pia wakihoji tozo zinazoanzishwa na Seriakali zikidaiwa kuwaumiza maisha ya wananchi.
Akiwasilisha bajeti ya Serikali ya mwaka 2024/25, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alisema hadi Machi 2024, deni la Serikali lilikuwa zaidi ya Sh91.7 trilioni. Kati ya kiasi hicho, deni la nje ni Sh60.9 trilioni na deni la ndani ni Sh30.7 trilioni.
Wakizungumza katika mjadala wa X-space iliyoandaliwa na Mwananchi Communications Ltd wenye mada isemayo ‘Upi mtazamo wako kuhusu mwenendo wa deni la Serikali?” leo Juni 19, 2024, wachambuzi hao wametaka pia kuwepo na uwazi katika matumizi ya mikopo hiyo ili kuondoa maswali kwa wananchi.
Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Ahobokile Mwaitenda amesema kumekuwa na ongezeko la ghafla la deni la Serikali, huku matumizi yake yakikosa uhalisia.
“Waziri (wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba) alisema deni limekuwa likiongezeka kwa sababu limekuwa likitumika kujenga miundombinu, huduma za jamii, elimu, afya na maji. Sikubaliani na maelezo hayo kwa sababu, wakati wanaposoma hii bajeti huwa wanasema miundimbinu yote kama SGR (reli ya kisasa), miradi ya umeme, wanasema ni fedha za kodi na tozo, kwa sababu kumekuwa na tozo kila mahali. Sasa tunajiuliza hizi fedha zinakwenda wapi?” amehoji.
Kuhusu uhimilivu, amesema kuna vigezo vimewekwa kuangalia ukubwa wa deni na pato la Taifa na Wizara ya Fedha inasema hatujavuka asilimia 40.
“Swali linakuja, unakokotoa vipi pato la Taifa na deni la Taifa? Deni tunalijua, lakini tuangalie Watanzania wote wamechangia nini kwenye pato la Taifa?” amehoji.
Akifafanua zaidi, Mwaitenda amesema madeni ya nchi zinazoendelea hayalipiki, kwa sababu fedha haziendi kwenye shughuli za uzalishaji.
“Kwa mfano fedha za Uviko-19, zaidi ya Sh1.3 trilioni badala ya kupeleka kwenye uzalishaji tukapeleka kujenga vyoo.
“Kama deni linahudumia huduma za jamii, kwa nini elimu yetu iko chini ukilinganisha na nchi za Afrika Mashariki? Maji tu Dar es Salaam ni shida, kuna huduma mbovu za afya,” amsema.
Maoni hayo yameungwa mkono na mchangiaji, Peter Kahindi akisema licha ya Serikali kusema deni hilo linahudumia miradi ya maendeleo na huduma za jamii, bado haoni unafuu wa maisha.
“Sioni kama kukopa ni tatizo, tatizo ni matumizi. Kwa sababu kama ni kujenga madarasa tunalipa tozo, kwenye barabara kuna tozo. Kwa hiyo tunapoambiwa tunakopa, Watanzania wanataka ujua hizo fedha zinakwenda wapi?
“Ukishika salary slip (hati) za mishahara ya wafanyakazi ni kodi tupu, ukilipa umeme wanakata kodi,” amesema.
Akijibu hoja hizo, Kamishina wa Usimamizi wa Deni la Serikali wa Wizara ya Fedha, Japhet Justin, amesema ukubwa wa deni unakua kwa kuongozwa na shabaha za uchumi.
Kwenye bajeti kuna sehemu inazungumzia nakisi ya bajeti, isiyozidi asilimia 2.9. Tumeona Uganda wametuzidi. Lakini ukitaka kuongeza bajeti maana yake itabidi ukope zaidi.
Amesema kwa bajeti ya mwaka 2024/25, Serikali imedhamiria kukopa Sh14.7 trilioni.
Akitaja miradi inayokopewa, Justin amesema ipo miundombinu likiwemo daraja la Tanzanite la Dar es Salaam lililojengwa kwa mkopo kutoka Korea.
“Tanzania inaongelea mradi wa umeme wa megawati 1,600, zaidi ya asilimia 60 ya umeme kwa miaka mitano iliyopoita, lile bomba la gesi lilikuwa ni mkopo kutoka benki ya Exim ya China.
“Kwa hiyo huu umeme tulionao kwa miaka mitano iliyopita ni kwa mkopo huo ambao tunaulipa kwa miaka 25,” amesema.
Awali akieleza umuhimu wa Serikali kukopa, mchambuzi wa uchumi, Oscar Mkude amesema Serikali imekuwa ikilazimika kukopa kwa sababu makadirio yake yanakosa fedha za kutosha.
Hata hivyo, ametahadharisha kuwepo kwa mikopo ya kibiashara akisema inaweza inaongeza ugumu wa kulipa na kuwapa mzigo wa wananchi.
“Mikopo ya biashara sio mizuri na kwa muda mrefu inaweza kuleta athari kubwa. Hivi karibuni nchi za Afrika zimetajwa kuwa na madeni makubwa kwa sababu imekopwa katika masharti ambayo si rahisi,” amesema.