Dar es Salaam. Wapangaji wanunuzi 20 wa nyumba za mradi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mtoni Kijichi wilayani Temeke wamejikuta wakitolewa kwenye makazi hayo kwa nguvu, wakidaiwa kushindwa kulipia nyumba hizo.
Operesheni hiyo iliyoanza leo Juni 18, 2024 itakuwa endelevu katika kudhibiti wadaiwa sugu imeanza maeneo mbalimbali nchini kwenye miradi ya nyumba hizo lengo likiwa kubaki na wapangaji wanaozingatia matakwa ya mikataba yao.
Akizungumza wakati operesheni hiyo ikiendelea, Dar es Salaam jana Juni 18, 2024, Meneja Miliki wa NSSF, Geoffrey Timothy amesema wateja hao wamekuwa na malimbikizo ya madeni ya muda mrefu na matokeo yake wamekuwa wakirudisha nyuma azma ya mfuko huo kuboresha mafao ya wafanyakazi.
“Ili kudhibiti mfumo huu wateja sugu tumekuwa tukiwatoa na operesheni hii inahusisha nyumba zote zilizojengwa nchi nzima na kuna maeneo mengi hatuuzi nyumba ila tunapangisha,” amesema.
Timothy amesema njia sahihi ya kusalia kwenye nyumba hizo na kuishi kwa amani ni kuzingatia matakwa ya mikataba waliyoingia kwa kulipa kwa wakati na siyo vinginevyo.
“Lengo la mfuko ni kuwa na mteja anayetii na kufuata taratibu za mfuko. Utaratibu wa ulipaji mpangaji anatakiwa kulipa mwezi mmoja kabla na anayekiuka tunatoa notisi ya siku 30 usipolipa tunatoa tena notisi ya siku 14 ukishindwa tunakuja kukutoa,” amesema.
Amesema wadaiwa hao licha ya kuondolewa katika nyumba hizo lakini wataendelea kudaiwa kupitia wakala wao wa kufuatilia madeni kuhakikisha wanalipa kwa kuwa fedha hizo ni mali ya Serikali.
“Nyumba hizi tutaziweka sokoni kwa anayetaka kuja kupanga kwa kukubaliana na masharti ambayo yanatolewa na meneja wetu kwa kila mradi kwa kuanza kulipa asilimia 10 ya kwanza na baada ya hapo kunaandaliwa mpango wa malipo kila mwezi,” amesema.
Amesema baada ya kutoa asilimia 10 mteja anakabidhiwa funguo na baada ya hapo huwa wanatoa utaratibu wa kufanya malipo kila mwezi kwa kipindi cha miaka 15.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Changanyike, Donisia Kamugisha amesema ni muhimu kwa wapangaji kuzingatia makubaliano wanayoingia ili kuepuka kufukuzwa kwenye nyumba hizo.
“Unajua hili ni jambo la aibu. Ni busara kama mmekubalina kuingia makubaliana ya kupanga basi wazingatie masharti sasa hapa wengine hadi miaka mitano hawajalipa unadhani hiyo haki,” amesema Donisia.