Zulfa Macho:Ngumi zilivyomgombanisha kiungo wa Yanga na mwanawe

UKIONDOA Mkoa wa Morogoro katika soka kuwa na wachezaji wengi wenye majina makubwa hapa nchini basi itakuwa ngumu kama utashindwa kuutaja Mkoa wa Kigoma ambao umetoa wachezaji wa kutosha kwenye mchezo huo.

Achana na Juma Kaseja ambaye alitajwa hadi katika ile nyimbo ya Bongo Fleva iliyowakutanisha wasanii wa Kigoma ‘Kigoma All Stars’, mkoa huo yapo majina ya mastaa wengi waliotikisa katika soka kama Edibily Lunyamila, Seleman Matola, Wilfred Kidau, Said Sued “Scud”, Nteze John bila ya kusahau nyota wa zamani wa Simba na Yanga, Yusufu Macho Muso ingawa kwa majina halisi kwa mujibu wake ni Macho Yusufu Rwenda.

Macho aliyetisha katika eneo la kiungo Simba na Yanga pamoja na Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars, ndiye baba mzazi wa bondia wa ngumi za kulipwa na ridhaa, Zulfa Yusufu Macho.

Bondia huyo ana rekodi ya kucheza mapambano manne tu katika ngumi za kulipwa akiwa ameshinda yote kabla ya mwaka jana kuvutwa kwenye timu ya taifa ya ridhaa iliyoshiriki mashindano ya kuwania kufuzu Olimpiki kwa Ukanda wa Afrika nchini Senegal.

Katika mashindano hayo, Mtanzania huyo ambaye kwa sasa ni askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ‘JWTZ’ akitokea Ngome Lugalo, alishinda kwa pointi dhidi ya Grace Nankinga wa Uganda, kisha akachapwa na Adeyoya Oseji wa Nigeria.

Macho anatupasha awali alikuwa akivutiwa na mchezo wa Wushu ambao aliona watu wakiwa wanafanya mazoezi katika moja ya chuo cha mchezo huo kilichopo Mbagala kabla ya baadae kuanza kujifunza mchezo wa karate.

Bondia huyo anafafanua kwamba wakati anaendelea na mazoezi katika chuo hicho ambacho kilikuwa kikisimamiwa na Mwarami Mitete ambaye ni Mwenyekiti wa Wushu Tanzania, aliweza kubaini uwepo wa mchezo mwingine ambao unafahamika kwa jina la Sanja ukijumuisha mateke na ngumi.

“Huo mchezo ulivyo ni kama kick boxing lakini siku ya kwanza kufundishwa zile ‘stance’ za ngumi ndiyo nikajikuta naanza kupenda ngumi na pale chuoni kulikuwa na bondia anaitwa Venance Mponji na Juma Malenda waliokuwa wakinifundisha.

“Kiukweli pale chuo sikuweza kudumu sana kwa sababu nilikuwa nikifanya mazoezi kwa kuibia bila familia yangu kujua jambo lolote kama nimeingia kwenye michezo ya mapigano.

“Sasa nilivyotoka pale nikaingia kwenye gym za mitaani maana sikuwa na sapoti yoyote ndani ya familia lakini sikuhitaji wafahamu jambo lolote kutokana na misingi na maadili ya baba yangu alikuwa hapendi kabisa niwe kwenye makundi ya kimichezo.

“Wakati huo naendelea na mazoezi nikajikuta mchezo unakaa kwenye damu, nikawa ninaufuatilia hasa mabondia wa kike wa nje ndiyo nikamjua Claresaa Shield, nikawa namwangalia sana.

“Katika moja ya hizo Gym ndiyo nikajiunga na gym inaitwa Itafahamika ipo Mbagala Chamazi na pambano langu la kwanza kabisa nilicheza na Halima Vunjabei mwaka 2014, nikampiga kwa pointi.

“Lakini baada ya pambano nikatoka katika ngumi za kulipwa kwenda ngumi za ridhaa kwa kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa Mgulani na wakati huo sikuwa bondia mzuri kwa sababu bado nilikuwa sina misingi mizuri ya ngumi.

“Unajua nilianza kujifunza ngumi mwaka 2013 na pambano langu la kwanza nilicheza mwaka 2014, bado sikuwa na misingi mizuri ya mchezo huo.

“JKT nilikaa miaka mitatu, kwa bahati mbaya sikufanikiwa kupata ajira nikarejea mtaani na kujiunga tena na ngumi za kulipwa katika Gym ya Uwanja wa Kivita chini ya Kocha Kwame ndiyo nikaendelea kuwa imara.

“Baadae nikamchapa Flora Machela, kisha Alice Mbewe wa Zambia kabla ya kumpiga tena Halima Vunjabei katika pambano la kuwania Mkanda wa Ubingwa wa Dunia wa UBO katika uzani wa super fly, mwaka 2021.

Nini sababu ya baba kupinga harakati zako kwenye ngumi?

“Kiukweli ilichukua muda sana hasa upande wa familia ambayo natoka kwani ilikuwa na usimamizi mkali sana kutoka kwa wazazi  lakini nilikuwa naweza kutenga muda wa kufanya mazoezi bila ya wao kufahamu.

“Nilikuwa natumia usiri mkubwa, nakumbuka kipindi hicho naenda shule, nilikuwa naamka saa 11 alfajiri, nikimaliza kazi za nyumbani saa 11:30 naenda gym na nguo zangu za shule ila kwenye begi nakuwa na nguo za mazoezi ambazo nikifika nabadilisha.

“Baada ya mazoezi naoga tena kule kule gym kisha navaa nguo za shule kwenda shule na nikitoka shule ikawa pia nafanya hivyo kila siku ndiyo sababu iliwafanya wasijue.

“Lakini ilikuja kubainika siku moja kulikuwa na shoo pale Dar Live ambayo ilikuwa inahusisha michezo yetu na mmoja ya walioshiriki nilikuwa mimi ambaye ni msichana pekee, bahati mbaya aliyechukua video alikuwa baba yangu mdogo.

“Sasa alipoenda kutengeneza kwenye ofisi yake ndiyo siri yangu ilifichuka kutoka hapo na taarifa zilimfikia baba ambaye alichukia sana.

“Baada ya baba yangu kujua ndiyo alianza kunifuatilia kwa kuhakikisha naacha kabisa mambo ya ngumi, nimepitia changamoto nyingi sana za kukwazana na baba hadi ilifikia hatua akanifukuza nyumbani.

“Unajua familia yetu ipo kwenye misingi ya dini ndiyo maana kwake ilikuwa ngumu kuelewa kwani hata nilivyokuwa nataka kucheza soka aligoma, nakukumbuka alikuja hadi shule wakati nasoma kuwambia walimu hataki kusikia nacheza soka.

“Kiukweli kwenye soka baada ya misimamo yake ilinivunja moyo lakini ilivyokuja kutokea kwenye ngumi nikasimia kile ninachokiamini kwa upande wangu na sikutaka kumsikiliza mtu yeyote.

“Lakini nilimweleza nikimaliza shule nisizuiwe kucheza ngumi huku nikimsisitiza hata aliyetengeneza jina na maisha kupitia miguu yake hadi kutulea sisi, nikamweleza aniache nitumie mikono yangu inawezekana kuna siku nitakuja kuwalea.

“Baada ya kumwambia hivyo akaona aniache tu maana tayari yashatokea ya kutokea, kuna wakati nilitoroka nyumbani hakuna aliyejua naishi wapi.

“Niliondoka na kwenda kuishi nyumbani kwa rafiki yangu wa kiume anaitwa Shaban Mohamed ambaye alinipisha kwenye chumba chake, yeye hana kazi wala mimi sina kazi, kazi yetu ilikuwa mazoezi pekee.

“Yeye alikuwa mkubwa kwangu na nyumba tuliyokuwa tunakaa palikuwa kwao, ni wale wakongwe wa vijiwe, akawa anapambana huko anachukua pesa ndiyo tukawa tunakula.

“Wakati huo na mimi nilikuwa napambana maana nilikuwa msusi mzuri wa nywele, pia nilikuwa nachora, hivyo kilichokuwa kinapatikana tunakula, alinisaidia sana kwa kipindi cha mwaka moja na nusu nilipokuwa sipo nyumbani.

Ilikuwaje ukarudi nyumbani kumalizana na mzee?

“Kutokana na ukimya hatukuwa tukionana, akawa ananiona kwenye magazeti halafu nimemtaja jina lake, akawa anachukua na kutunza ndani, alikuwa anajisikia ufahari ingawa hakutaka kabisa niwe mtu wa hivi.

“Nashukuru hata hati yangu ya kwanza kusafiria yeye ndiye alitoa pesa ya kwenda kutengeneza na kitu kingine kilichofanya akubaliane na mimi baada ya kupata nafasi ya kwenda JKT maana hakuamini na alikuwa anasema sina ndugu mwanajeshi hivyo siwezi kufika popote.

Nini kilitokea ukarudi jeshini baada ya kurejea kwenye ngumi za kulipwa?

“Nadhani naweza kusema ni mipango ya Mungu ndiyo imesababisha kurudi nilipo sasa, nashukuru Mungu sasa ni askari ambaye ni bondia.

“Sasa hivi nacheza ngumi za ridhaa na za kulipwa ingawa za kulipwa ni muda mrefu sijacheza ila mashabiki wajue kama nipo ikitokea wakuu wangu wakitaka nicheze nitacheza kwani bado napigana.

Wewe na mzee sasa hivi mpoje?

“Nashukuru Mungu tupo sawa na nimekuwa nikimwambia yeye ndiye ‘role model’ wangu, jambo kubwa zaidi ni amekuwa akinipa sapoti ya kutosha sana,” anasema Macho.

Related Posts