INGEKUWA ni rahisi kushangaa iwapo Augustine Okrah angedumu Yanga kwa muda mrefu baada ya Kusajiliwa kwa mbwembwe katika dirisha dogo la usajili mwaka huu.
Lakini hili la kukaribia kupewa mkono wa kwa heri baada ya kuitumikia timu hiyo kwa muda usiozidi miezi sita, wala sio jambo la kushtua na lilitegemewa kutokea ndani ya Yanga.
Lilionekana lingetokea kutokana na historia ya mchezaji huyo kabla hajajiunga na Yanga, pia mazingira yanayoizunguka klabu hiyo katika miaka ya hivi karibuni.
Kumbukumbu zinaonyesha aliwahi kuichezea Simba kwa muda mfupi kisha akaonyeshwa mlango wa kutokea baada ya uongozi wa timu hiyo kutofurahishwa na mienendo yake ya nje ya uwanja ambayo kwa kiasi kikubwa ilichangia asitoe mchango mkubwa kwa Simba.
Kabla ya kusajiliwa na Simba akitokea Ghana alikokuwa akichezea Bechem ya huko, Okrah hakumaliza vyema msimu wa 2021/2022 kwani alijikuta akipewa adhabu ya kufungiwa mechi kadhaa kutokana na kosa la kupigana uwanjani.
Sasa historia hiyo ilipaswa kuifanya Yanga kutokumwekea dhamana Okrah na badala yake ingefanya uchunguzi wa kina ili iweze kujua kwa undani maisha na tabia zake kuona kama inapaswa kumsajili au la jambo ambalo halikuweza kufanyika hadi pale Mghana huyo aliposajiliwa.
Lakini ikafumba macho na kuziba masikio kisha kuamua kumsajili lakini mwishowe leo hii ndani ya muda mfupi inavuna kile ilichokipanda kwa Okrah kutotoa mchango mkubwa kikosini hadi kusababisha kuvunja naye mkataba baada ya kuitumikia kwa muda mfupi.
Yenyewe iliamini Okrah angebadilika kitabia akiwa na kikosi cha Yanga na kuinufaisha klabu hiyo ndani ya uwanja kwenye mechi za mashindano mbalimbali tofauti na alivyokuwa kwa waajiri wake wa zamani ambao ni Simba.
Lakini mambo yamekuwa tofauti kwani inatajwa kuwa kilichomfanya aachwe na Simba ndio kimeishawishi Yanga kuamua kumpa mkono wa kwa heri akiwa hajafikisha hata mwaka ndani ya timu hiyo.
Labda Yanga ililenga kufanya mauzo ya jezi kupitia usajili wa Okrah lakini kiufundi hakukuwa na kipya ambacho Mghana huyo angekileta kikosini.