Arusha. Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Dodoma, imewaachia huru watuhumiwa watatu katika kesi ya mauaji akiwemo Mwandu Kashinje aliyekuwa akituhumiwa kushirikiana na wenzake kumuua mama yake mzazi, Nshoma Salawa.
Mbali na Mwandu, washtakiwa wengine walioachiwa huru ni mshtakiwa wa kwanza Nkinga Maganga na mshtakiwa wa pili Kasule John.
Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo ilidaiwa kuwa Mwandu alikuwa anamtuhumu mama yake analoga watoto wake, hivyo kuwalipa watuhumiwa wenzake Sh800,000 ili wamuue mama yake mzazi.
Kesi hiyo ya mauaji namba 92/2022 ilikuwa ikisikilizwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Dk Juliana Masabo.
Hukumu hiyo imetolewa Juni 14, 2024 ambapo Jaji huyo alifikia uamuzi huo baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha kesi hiyo pasipo na shaka na kuwaachia huru washitakiwa hao.
Katika kesi hiyo, watuhumiwa wote watatu wanadaiwa kushirikiana kumuua Nshoma ambaye ni mama wa mshtakiwa wa tatu, Agosti 28, 2016 katika Kijiji cha Mwamaboku Hamlet, Kata ya Iyumbu wilayani Ikungi, Mkoa wa Singida.
Katika kesi hiyo Jamhuri iliwakilishwa na mawakili watatu wakiongozwa na Wakili wa Serikali, Michael Martin huku utetezi nao wakiwakilishwa na mawakili watatu wakiongozwa na Peter Ndimbo.
Katika kuthibitisha shitaka hilo, Jamhuri ilikuwa na mashahidi watano akiwemo mlinzi. Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Singida, Deodatus Patrick alirekodi maelezo ya ungamo ya ziada ya washitakiwa hao.
Daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili huo, alidai kubaini kuwa marehemu alikuwa na jeraha kubwa kichwani, jeraha kubwa la kukatwa kifuani na lingine mguu wa kulia.
Licha ya tukio hilo kuripotiwa Kituo cha Polisi Ikungi siku hiyo, washtakiwa hao walikuja kupatikana miezi 10 baadaye (Juni 29, 2017), ilidaiwa kuwa mshtakiwa wa kwanza na pili walikamatwa kwa mahojiano na kuwekwa rumande.
Ilidaiwa Julai 2, 2017 walipata taarifa za uwepo wa mshtakiwa wa tatu katika Kijiji cha Makungu, ambapo walikwenda kumkamata.
Shahidi wa pili alidai mahakamani hapo kuwa anakumbuka alimhoji mshtakiwa wa pili Juni 30, 2017 ambapo alidai mshtakiwa huyo alikiri kumuua Nshoma ambapo alidai kuwa mshitakiwa wa tatu aliamini kwamba mama yake alikuwa akiloga watoto wake.
Shahidi huyo alidai kuwa kutokana na sababu hiyo, walilipwa Sh800,000 ili kumuua.
Ilidaiwa kuwa kwa kutumia panga, mshtakiwa wa kwanza alimpiga marehemu sehemu tofauti za mwili wake ikiwa ni pamoja na kichwani, shingoni na kiunoni huku yeye, mshtakiwa wa pili akilinda mlango wa marehemu na kumulika eneo la tukio kwa mwanga wa tochi.
Mbali na kukiri mshtakiwa huyo, ilidaiwa katika maelezo ya ziada ya ungamo washitakiwa wote watatu walikiri kosa.
Kwa upande wa utetezi, kila mmoja alitoa ushahidi wake kwa kiapo na hakumwita shahidi, ambapo wote walikana kutenda makosa hayo na kudai wakati wa kuandikwa maelezo hayo walikuwa chini ya ulinzi wa polisi wakiteswa na kulazimishwa kukiri makosa hayo.
Baada ya kusikiliza pande zote mbili, suala lililosubiri kuamuliwa ni iwapo tuhuma za mauaji dhidi ya washitakiwa wote watatu zilithibitishwa na kuwa lazima vipengele muhimu vithibitishwe.
Kuhusiana na kosa la mauaji ambalo washtakiwa wanashtakiwa, alieleza inabidi ithibitishwe kuwa mtuhumiwa, kwa nia mbaya, alimuua marehemu kinyume cha sheria hivyo katika kesi hiyo kosa hilo linalodaiwa kutendwa na watu zaidi ya mmoja lazima lithibitishwe.
Jaji alieleza ili kuthibitisha kosa hilo na nia ovu ni wajibu wa upande wa mashtaka kuthibitisha kesi za jinai, kama ilivyoelekezwa katika kifungu cha 3(2) (a) cha Sheria ya Ushahidi, iliyosomwa kwa pamoja na vifungu vya 110 na 112 vya Sheria hiyo hiyo.
Jaji alieleza kuwa upande wa mashtaka na utetezi ulikubaliana kuwa kifo cha marehemu hakikuwa cha kawaida kwani kilitokana na majeraha mengi ya kukatwa mwilini mwake na kuvuja damu nyingi.
Jaji alieleza kuhusu washtakiwa kutenda kosa hilo, upande wa mashtaka uliegemea zaidi katika maungamo kama yalivyoainishwa katika maelezo ya mshitakiwa wa kwanza na maelezo ya ziada ya washtakiwa wote watatu.
Amesema mshtakiwa anayekiri kosa hilo anachukuliwa na sheria kuwa shahidi bora zaidi na kuwa ni muhimu pia kwamba kurekodi kwa ungamo kunapaswa kuendelea kwa kufuata kikamilifu matakwa ya kisheria ya utaratibu.
Amesema mshitakiwa wa pili katika utetezi wake, alidai maelezo hayo hayakutolewa kwa hiari ambapo katika ungamo hilo, mshtakiwa huyo alikiri katika tarehe na mwezi usiojulikana mwaka 2016, alilipwa na mshtakiwa wa tatu Sh800,000 ili amuue mama yake mzazi.
Alidai alikwenda nyumbani kwa Nshoma akiwa ameongozana na mshtakiwa wa kwanza (ambaye ni mdogo wake), wakiwa na fimbo na panga na baada ya kufika, mshtakiwa wa tatu aliingia ndani na kumshambulia bila huruma kwa panga kichwani, shingoni na kiunoni huku yeye akiwa ameshika fimbo akiwa mlangoni analinda.
Amesema katika kielelezo cha nne ambacho ni maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa kwanza, kilikuwa na jina tofauti la marehemu ambapo katika hati ya mashtaka ilikuwa inasomeka Nshoma Salawa lakini katika kielelezo hicho, lilikuwa Nshoma Salala huku ikiwa haionyeshi tarehe ya tukio kutokea.
Amesema katika maelezo ya ziada ya mshtakiwa wa pili, shahidi wa kwanza alijitambulisha kama ‘hakimu’ lakini jina halikutajwa, hivyo hakuna uhakika kama maelezo hayo yalirekodiwa na shahidi huyo wa kwanza.
Dosari nyingine ni kwamba haikuonyeshwa kama maelezo hayo yalisomwa kwa washtakiwa kabla ya kusaini, huku akinukuu kesi moja ya Mahakama ya Rufani ambayo ilisema kutokuonyeshwa kwamba hati ilisomwa kwa mrufani, jambo ambalo ni baya.
Amesema kutokana na sababu hiyo, maungamo hayo hayapaswi kuzingatiwa na baada ya kuziondoa, kielelezo cha tano cha Jamhuri ndiyo ushahidi pekee uliobaki ambao pia haujathibitisha tarehe ya kifo, kwani hakuna mahali inapoelekeza kifo kilitokea Agosti 28 na siyo 29, 2016 ambayo ni siku mwili ulifanyiwa uchunguzi.
“Kwa kuwa nimegundua kuwa kielelezo cha nne hakiwezi kuunga mkono hukumu kwa kukosekana kwa uthibitisho, kesi ya mashtaka imebaki bila uthibitisho. Katika matokeo yake, ninatupilia mbali shitaka hilo na kuwaachia huru washtakiwa wote watatu kwa kuwa hawakupatikana na hatia ya mauaji,” amesema.