Baada ya Korea Kaskazini, Putin atua Vietnam

Hanoi, Vietnam. Rais wa Russia, Vladimir Putin ametua nchini Vietnam na kukutana na Rais wa nchi hiyo katika mji wa Hanoi leo Alhamisi Juni 20, 2024 kwa ziara ya kiserikali.

Putin amekaribishwa na Rais mpya wa Vietnam, To Lam katika Ikulu ya Hanoi ambapo atafanya mazungumzo na Rais huyo.

Taarifa iliyochapishwa na Shirika la Habari la AFP imesema baadaye Putin atakutana na viongozi wengine wakuu wa Vietnam akiwemo Nguyen Phu Trong, Katibu Mkuu mwenye nguvu ndani ya chama tawala cha Kikomunisti.

Ziara hiyo ameifanya ikiwa ni siku moja baada ya kutoka nchini Korea Kaskazini alikofanya ziara ya kiserikali kisha kusaini mkataba wa ulinzi wa pande zote na mwenzake, Kim Jong Un.

Putin na Kim walisaini mkataba wa kimkakati katika mkutano wa kilele mjini Pyongyang ambao ulijumuisha kujitolea kusaidiana iwapo watashambuliwa. Kim pia aliahidi kuunga mkono kikamilifu vita vya Russia dhidi ya Ukraine, AFP imesema.

Wakati huohuo, Marekani na washirika wake wanaishutumu Korea Kaskazini kwa kusambaza risasi na makombora kwa Russia kwa ajili ya vita vyake nchini Ukraine na makubaliano hayo yamezidisha hofu.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema kuimarisha uhusiano kati ya Russia na Korea Kaskazini kunatia wasiwasi huku ofisa wa ngazi ya juu wa Ukraine akiishutumu Pyongyang kwa kuunga mkono mauaji ya raia wa Ukraine.

Nchi hizo mbili zimekuwa washirika tangu kuanzishwa kwa Korea Kaskazini baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na zimekuwa karibu zaidi tangu Urusi ilipovamia Ukraine mwaka 2022.

Katika ziara hiyo Rais Kim alimwita mwenziye Putin kwamba ni rafiki kipenzi wa watu wa Korea na akaapa kumuunga mkono na mshikamano juu ya vita vya Ukraine, ambavyo vimesababisha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Moscow.

Naye, Putin alimshukuru mwenyeji wake Kim ambaye nchi yake imekuwa chini ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa tangu 2006 kutokana na mipango yake ya silaha iliyopigwa marufuku.

Kwa taarifa zaidi kuhusu ziara ya Putin nchini Vietnam, endelea kufuatilia mitandao ya Mwananchi.

Related Posts