Benki zachangia Sh3.9 trilioni kwenye kodi

Dar es Salaam. Ripoti mpya ya Sekta ya benki nchini Tanzania imeonyesha kuwa sekta hiyo imechangia zaidi ya Sh3.9 trilioni kwenye mapato yatokanayo na kodi katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2021 hadi 2023.

Hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Chama cha Mabenki Tanzania (TBA) uliohusisha benki 26 ukilenga kuonesha mchango wa taasisi hizo kwenye uchumi katika mapato yatokanayo na kodi ikiwa ni mara ya kwanza kufanyika.

Ilibainika kuwa mwaka 2021 michango ya kodi ilikuwa Sh1 trilioni ambayo baadaye ilikua kwa asilimia 30 hadi Sh1.3 trilioni mwaka 2022 na trilioni 1.6 mwaka 2023.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa TBA, Theobald Sabi amesema sekta ya benki imeendelea kukua na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika mapato ya kodi ya serikali kutoka asilimia 5.6 Januari 2021 hadi asilimia 6.6 Desemba 2023.

Sabi ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NBC Plc, amesema hatua hiyo ni matokeo ya athari chanya za sera nzuri katika upanuzi wa uchumi na ongezeko la michango ya kodi kwa Serikali.

“Pamoja na kujivunia mchango wetu kwenye mapato ya Serikali, tunajivunia zaidi mchango wa sekta ya kibenki kwenye uchumi kupitia mikopo na huduma mbalimbali za malipo.

“Tunaamini kuwa kadri uchumi unavyoendelea kukua kutokana na mazingira mazuri ya biashara, sekta yetu itaendelea kupanuka, na mchango wetu katika mapato ya Serikali, hasa katika suala la kodi, utaendelea kuongezeka,” alisema Sabi.

Kodi ilitozwa kwa benki 26 zilizoshiriki kwenye utafiti huo ilichangia asilimia 18 ya kodi ya jumla ya mapato ya kodi baada ya faida kati ya mwaka 2021 hadi mwaka 2023.

Kwa upande wake, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Sauda Msemo amesema Serikali inatambua juhudi zinazofanywa na sekta ya benki nchini na kuahidi kuendelea kuweka mazingira wezeshi ili kukuza zaidi biashara kwenye eneo hilo.

Amesema mbali na kuzalisha mapato ya kodi sekta hiyo imekuwa kichocheo cha ajira kwa kutengeneza ajira na kusaidia katika ukuaji wa uchumi.

“Tunaona kwamba benki sasa zinachangia kwa kiasi kikubwa uchumi, siyo tu katika suala la mapato ya kodi lakini pia kwa kuajiri watu na kusaidia kuongeza fursa za kazi katika nchi, jambo ambalo tunalithamini upande wa Serikali.

“Kwa mtazamo wa benki kuu na Serikali, tunaahidi kudumisha mazingira mazuri ya shughuli bora za biashara ili waweze kufanya vizuri zaidi. Kuna fursa nyingi bado ambazo naamini zikifanyiwa kazi zitawezesha sekta kuendelea kukua siku hadi siku na kuongeza mchango wake katika uchumi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla unaongezeka,” amesema Sauda.

Ripoti hiyo imeonesha sekta ya benki imeendelea kuwa mwajiri muhimu ambapo watu 16,731 waliajiriwa kufikia mwaka 2022 katika taasisi mbalimbali za kibenki.

Kutokana na ripoti hiyo, mchango wa PAYE katika sekta ya benki kuanzia mwaka 2021 hadi 2023 ulifikia Sh bilioni 673, sawa na asilimia 8.4 ya PAYE iliyokusanywa Tanzania.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo asilimia 39 ya benki zinazoshiriki zinakubaliana kwamba kuna ushirikishwaji wa wadau wa sekta hiyo katika mchakato wa kupitia na kubadilisha mfumo wa kodi.

“Hii inatekelezwa hasa kwa kushirikiana na TBA, hata hivyo, bado kuna shaka kama ushiriki huu unasababisha maoni ya wadau kuzingatiwa kwani maoni mengi ya wadau yanaonekana kutotekelezwa,” imeeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Related Posts