Bulaya alia na mafao ya wastaafu, ataka Serikali ilipe deni la mifuko

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya ameitaka Serikali kulipa deni la Sh 2 trilioni inalodaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii ili kuiwezesha kuongeza kiwango cha mafao ya mkupuo kwa wastaafu.

Ameyasema hayo leo Alhamisi, Juni 20, 2024 wakati akichangia mjadala wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/2025 ya Sh49 trilioni.

Bulaya amesema uwekezaji usio na tija wa mifuko ya hifadhi ya jamii na madeni hayo ndio inasababisha wastaafu wapunguziwe mafao yao ya mkupuo.

Amesema Serikali ilipeleka bungeni Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) wa mwaka 2018, baada ya kubaini mifuko iko hoi na wanataka kuwadhulumu watumishi wa umma.

Amesema katika hotuba ya Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alisema wamerudisha kikokotoo kufika asilimia 40  kama zawadi kwa watu waliokuwa wakichukuwa asilimia 50 ya mafao kwa mkupuo.

Bulaya amesema watumishi hao walikuwa wakilipwa pensheni ya kila mwezi kwa miaka 15, lakini vyote hivyo Serikali imevipunguza.

Bulaya amesema kiini cha changamoto hiyo ni Serikali kuwekeza katika miradi isiyolipa kwa kuwa inatengeneza hasara badala ya faida.

“Nilitegemea mtaenda kulipa fidia katika fedha ambazo mumewekeza kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, nilitegemea mngesema Serikali mnadaiwa zaidi ya Sh2 trilioni muwalipe, ili waweze kujipangia. (Mliwalipa) wanaweza hata kulipa hata zaidi ya asilimia 60 mafao ya mkupuo,” alisema Bulaya.

Alisema Serikali imesema imesimamisha malipo ya awali na kwamba watalipa hadi mwaka 2029 na kuhoji wanalipa kama nani, wakati sheria inataja wenye mamlaka ya kuwalipa wastaafu ni mifuko ya hifadhi ya jamii.

Bulaya amesema Serikali inataka kuvunja sheria kwa kuwalipa wastaafu badala ya kushughulika na kiini cha changamoto hiyo, ambacho ni kulipa madeni na kulipa fidia kwenye maeneo waliyowekeza lakini hayazai faida.

Amesema wafanyakazi wanataka warudishe kiwango kanuni ya awali ya 1/540 badala ya 1/580 wanayoitumia kulipa sasa.

Anachokisema Bulaya juu ya uwekezaji wa mifuko ya jamii, kinafafanua na alichoeleza Rais Samia Suluhu Hassan Juni 12 kuwa baadhi mashirika hayana hesabu nzuri, lakini yana orodha ndefu ya miradi ya kutekeleza na historia ya kupata hasara.

“Labda niwe mwazi, utafiti uliopo PSSSF mpo hapa, utafiti unatwambia huo mfuko hauko vizuri. Na ule ni mfuko wa wafanyakazi, wakistaafu wanataka mafao yao.

“Tumekuja na wazo mfanyakazi alipwe hiki akistaafu, halafu miaka mingapi huko alipwe hiki (kikokotoo cha mafao ya wastaafu). Kwanini? (Ni kwa sababu) tunaokoa mfuko usife, lakini swali, aliyefanya mfuko kufikia hapo ni wafanyakazi?

“Wafanyakazi si wanachangia kila mwezi? Aliyefanya mfuko ufikie hapo ni nani? Ni menejimenti ya mfuko, si ndio? Pengine na Serikali, kwanini mzigo tunaushusha kwa wafanyakazi?” alihoji Rais Samia.

Alisema anashangaa kuona haohao wanaotaka kuwekeza fedha za mfuko ilhali tayari ipo miradi mingine iliyowekezwa siku za nyuma, yote haifanyi kazi au inafanya kazi kwa kiwango kidogo.

“Lakini nenda kaangalie orodha ya miradi wanayoweka wanataka kuwekeza, unajiuliza wanataka kuwekeza kwa fedha zipi? Nenda kachambue huo uwekezaji wenyewe ukaone fedha zilizofichwa huko ndani,” alisema.

Related Posts